NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo Januari 16, 2022 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ikulu inayojengwa katika eneo la Chamwino, Jijini Dodoma na kusema ameridhishwa na kasi ya ujenzi na ubora wa majengo hayo na amemtaka mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika mwezi Mei,mwaka huu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Januari 16, 2022. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Mosses Kusiruka na kulia kwake ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali, Rajabu Mabele.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Daudi Kondoro (kulia) ambaye alitoa maelezo mafupi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, wakati Waziri Mkuu alipokagua ujenzi huo,
Waziri Mkuu amewasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati na kuwapongeza wote wanaohusika na ujenzi. “Tunataka kumuwezesha Mheshimiwa Rais kufanya kazi katika eneo lake maalum na afanye kazi katika mazingira mazuri na kwa ufanisi.”
“Nimefurahishwa na taarifa kwamba ujenzi huu umefikia asilimia 91 na hatua iliyobaki hizi asilimia 9 ni kazi ndogondogo kama uwekaji wa milango, njia za mifumo ya hewa na umeme na zote zinaenda vizuri.” Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pia anatarajia kuona ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Muonekano wa Jengo la Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma linalojengwa na SUMA JKT ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza ujenzi huo kwa ufanisi. “Ramani iliyoko hapa iko sawasawa na jengo la Ikulu lililoko Dar es Salaam, Wakandarasi wetu mmefanya kazi kubwa sana, Hii imedhihirisha kuwa nchi yetu ina wataalam wa kutosha kujenga aina yoyote ya majengo.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kizungumza na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Ikulu), Dkt. Mosses. Kusiruka (wa tatu kulia), Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja General Rajabu Mabele (wa pili kulia) na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mhandisi Daudi Kandoro (kulia). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mhandisi Daudi Kondoro amemhakikishia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba mradi huo utakamilika na kukabidhiwa mwezi Mei kama inavyotarajiwa kwani sasa uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Tags
Habari