Rais Dkt.Mwinyi awatoa machozi ya furaha wananchi

NA GODFREY NNKO

"Mheshimiwa Dkt. Mwinyi (Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi) ni kati ya viongozi wachache sana waliosalia katika karne hii ya 21, kwanza ni kiongozi muungwana sana, msikivu, ana utu, asiyekuwa na majivuno,hekima aliyonayo haielekezeki. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi. (Picha na Maktaba).

"Ni mtu safi na asiyependa kuona mwenye nacho anatumia uwezo wake kumuumiza mwengine (mwingine). Ni kwa sababu anajali sana utu, itoshe tu kusema Mwenyenzi Mungu amjalie heri, afya na baraka tele, juhudi zake tunaziona;

Ameyasema hayo Mtumwa Idd ambaye ni miongoni mwa wananchi ambao walizungumza na DIRAMAKINI BLOG katika mahojiano maalum yaliyofanyika jijini Zanzibar.

Mahojiano hayo baina ya wananchi na DIRAMAKINI BLOG yalilenga kupata ufahamu ni kwa namna gani ambavyo wananchi wanaielewa Dhana ya Uchumi wa Buluu na wanavyomuelezea mwasisi wake ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kupitia Serikali ya Awamu ya Nane.

Sambamba na namna ambavyo wanaielewa na kuitumia Programu Tumishi ya Kuwasiliana na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi moja kwa moja (APP ya Sema na Rais Mwinyi-SNR MWINYI ) ili kuwasilisha jambo lolote ambalo wanatamani Serikali ilipatie ufumbuzi wa haraka.

Uchumi wa Buluu

Juma Said, Mussa Makame, Mtumwa Idd na Hassan Hassan wakiwa katika maeneo ya Soko Kuu katika Mji Mkongwe (Soko la Darajani) jijini Zanzibar walionesha kufurahishwa zaidi na uongozi wa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi huku wakisisitiza kuwa, licha ya uadilifu, unyenyekevu ni kati ya viongozi wabunifu ambao katika maisha yao,wanatembea kifua mbele na wanajivunia kufanya kazi kwa bidii kwa sababu wanaongozwa na kiongozi sahihi wanayempenda.

"Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipotangaza dhana ya Uchumi wa Buluu mara moja nilipata picha pana sana, picha ambayo ilivikusanya visiwa vyote vya Zanzibar na kuitazama mara mbilimbili. Nilipata jibu moja tu, Mheshimiwa Rais ametujia na uchumi unaojali.

"Ni uchumi unaojali kwa sababu, unapozungumzia Uchumi wa Buluu unagusa kila kinachohusiana na bahari na kukichambua, kukipangilia, kukielekeza na kukiratibu ili kiweze kugusa kila kundi. Uchumi wa Buluu au uchumi wa bahari unajumuisha mambo mengi ikiwemo shughuli za uvuvi, viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji samaki.

"Pia kilimo cha mwani, utalii wa fukwe, michezo ya baharini ambayo imeendelea kushika kasi sana hapa nchini pamoja na hilo jambo kubwa ambalo tunalitarajia siku za usoni liwe la heri kwetu kwa maana ya mafuta na gesi,"amesema Mussa Makame katika mahojiano maalum na DIRAMAKINI BLOG jijini Zanzibar.

Ameongeza kuwa, Rais Dkt.Mwinyi kwa namna ambavyo anajitolea maisha yake kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu na kujishusha,atarajie thawabu nyingi mbele za Mwenyenzi Mungu.

SNR MWINYI 

Kwa upande wake, Juma Said amesema kuwa, Programu Tumishi ya SNR MWINYI ni ubunifu mwingine ambao umemsogeza karibu Rais Dkt.Mwinyi na wananchi, hivyo amempongeza kwa ubunifu huo.

"Programu ya Sema na Rais Mwinyi ni njia nyingine ya haraka zaidi katika kuwasiliana na Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi na kuwasilisha changamoto yoyote ambayo inakukabili au inawakabili katika maeneo yanayowazunguka, jambo la kufurahisha ni kwamba, ukiwasilisha kero, Mzee anaipatia ufumbuzi wa haraka sana, nimpongeze sana mheshimiwa Rais kwa juhudi hizi,"amesema Said.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wasaidizi wa Rais kuanzia ngazi za chini hadi juu kufanya kazi kwa bidii kwa sababu mafanikio ya nchi ni mafanikio ya wananchi.

"Wafanye kazi kama siafu, asiwepo wa kujiona yeye ni mkubwa zaidi ya mwingine, ushirikiano katika Serikali ya Awamu ya Nane ni jambo kubwa sana, tuache kufanya kazi kwa mazoea, kila mmoja awajibike kwa nafasi yake ili kuharakisha maendeleo,"ameongeza Said.

Hongera Rais Mwinyi

Wakati huo huo, wananchi wamempongeza Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi thabiti ambao umewezesha kurejesha uhusiano na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Zanzibar na Ujerumani.

"Ujerumani ilipositisha uhusiano na ushirikiano wa kimaendeleo kwetu Zanzibar lilikuwa ni pigo kubwa sana, ikizingatiwa kwamba, Zanzibar haina ardhi kubwa, inategemea zaidi shughuli za utalii na ushirikiano mwema na wadau wakubwa wa maendeleo ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kutuletea maendeleo wananchi.

"Busara na hekima za uongozi wa Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi zimewashawishi Wajerumani wamerejea tena, asante sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi uliotukuka,"amesema Khamis Mohamed mkazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi jijini Zanzibar. 

Zanzibar na Ujerumani

Hivi karibuni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania,Mheshimiwa Regine Hess walishiriki katika hafla maalum Ikulu jijini Zanzibar iliyoangazia uhuwishaji wa uhusiano baina ya Zanzibar na Ujerumani baada ya kusitishwa mwaka 2015.

Hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani. Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa, Serikali ya Ujerumani imewapa heshima ya kipekee kwa hatua yake ya kurejesha uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar wa muda mrefu na utakuwa wa kimaendeleo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, kurejesha ushirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Ujerumani kutaimarisha maendeleo Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar katika visiwa vyake vyote vya Unguja na Pemba.

Alisema kuwa, Ujerumani ina historia kubwa ya kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar na pia, ni nchi ambayo ilianzisha uhusiano wake na kusaidia Zanzibar tokea mwaka 1965 ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makazi, maarufu nyumba za Mjerumani zilizopo Kikwajuni Mjini Zanzibar, nyumba za maendeleo za Bambi, kusaidia maendeleo ya Mji Mkongwe Zanzibar pamoja na kusaidia huduma mbalimbali za kijamii.

Pia alisema, Ujerumani imekusudia kusaidia kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo miradi kadhaa ya maendeleo kama vile miradi ya maji, afya, michezo pamoja na kuunga mkono Dira ya Uchumi wa Buluu.

Kwa upande wa sekta ya afya, Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, Ujerumani imekusudia kuiunga mkono Zanzibar katika kutoa huduma za bima ya afya kwa wote ambapo utaratibu maalum utawekwa.

Pia, kwa upande wa maji, Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa, hatua ya nchi hiyo kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu, kuchimba visima vipya, vyanzo vipya vya maji pamoja na vifaa kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa huduma hiyo kutokana na kuwepo changamoto katika upatikanaji wake.

Kwa vile Ujerumani imeahidi kuisaida Zanzibar katika sekta ya michezo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza michezo hasa ikifahamika kwamba michezo ni ajira, afya na pia, michezo huondoa vitendo viovu kwa vijana sambamba na kueleza hatua za kuwepo uongozi makini kwenye sekta hiyo.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi alitoa shukurani kwa Serikali ya Ujerumani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani kwa hatua yake hiyo ya kurejesha upya uhusiano na ushirikiano na Zanzibar hali ambayo itaweza kusaidia katika mpango wa miaka mitano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naye Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Regine Hess alieleza kufarajika kwake na hatua hiyo na kusisitiza kwamba nchi yake inaimani kubwa na uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi pamoja na serikali yake anayoiongoza ya Umoja wa Kitaifa hatua ambayo imepelelea Zanzibar kuendelea kuwa na amani na utulivu mkubwa.

Balozi huyo aliahidi kwamba miradi yote iliyoahidiwa na Ujerumani itatekelezwa ipasavyo, kwani nchi hiyo ina historia kubwa ya kuisadia Zanzibar katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news