Serikali yadhamiria makubwa huduma bora ya maji mijini, vijijini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI kupitia Wizara ya Maji imesema inafanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ya kuhakikisha kuwa huduma ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini inaboreshwa.

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso ameyasema hayo leo baada ya kushuhudia tukio la kusaini hati ya makubaliano kati ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Wizara ya Maji, kupitia idara za maji kuhusu utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya mabwawa ya maji kwenye maeneo yanayoratibiwa na RUWASA.

''Hatuwezi kukubali kuona nchini kwetu Tanzania mvua nyingi inayonyesha maji yanapotea tu baharini, hapana. Hatuwezi kukubali kuona mvua nyingi inanyesha inaharibu miundombinu ya maji ilihali wananchi hawana maji.

‘’Tunatambua maji yapo juu ya ardhi na chini ya ardhi. Na takribani mita za ujazo zaidi ya bilioni 126. Bilioni 105 maji yako juu ya ardhi. Na bilioni 21 maji yaliyo chini ya ardhi. Haipendezi na wala haifurahishi mvua kwetu inakuwa maafa badala ya kuwa fursa. Tunaweza kujenga mabwawa tukaihifadhi maji na maji yale yakatumika kwa mifugo, umeme, kilimo na kutumika katika katika kada nyingi tu,’’ amesema Waziri Aweso. 
Pia amesema jukumu la wizara hiyo ni kuhakikisha rasimali za maji zinavunwa na kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama. 

"Tunaweza tukaungana sekta mtambuka ili kuhakikisha tunajenga bwawa kubwa ambalo litasaidia uvunaji wa maji na kutumika katika maeneo mbalimbali,’’ amesisitiza Waziri Aweso. 

Akizungumzia changamoto iliyojitokeza kwenye miradi ya vyanzo vya maji, Mkurugenzi wa Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo amesema, vyanzo vilikauka hivyo ikapeleeka wao kufanya utafiti na kubaini kuwa hawakutumia wataalam wao ndani ya sekta katika kutafuta vyanzo.

‘’Tuliona kitu cha kwanza kuingia makubaliano na wenzetu rasilimali za maji ili shughuli ya kutafuta chanzo cha maji. Na kuhitimisha kwamba hiki kinafaa na tujenge miundombinu na tukasema hii kazi ifanywe na ofisi za mabonde,’’amesema Mhandisi Clement.

Naye Mkurugenzi Rasimali za Maji, Dkt. George Lugomela amesema Kitengo cha Mabwawa cha Idara ya Rasimali za Maji kilianzishwa kwa Sheria Na. 11 ya mwaka 2009 na lengo mahususi likiwa ni kudhibiti mabwawa.

Pia wizara hiyo imesema itaendelea kuboresha huduma bora ya maji kwa watanzania wote waishio mijini na vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news