Wanafunzi Mbondole waiomba Ilala isikie kilio chao kuhusu barabara

NA ANNETH KAGENDA

WANAFUNZI katika Shule ya Sekondari Mbondole iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali kuwarekebishia barabara kutokana na ubovu uliokithiri, jambo linalopelekea wakati mwingine mvua zikinyesha kushindwa kupita huku walimu wakishindwa kupita kwa usafiri wa bodaboda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na DIRAMAKINI jijini Dar es Salaam kwa masikitiko wanafunzi hao wamesema, ubovu wa barabara ni kilio kikubwa kwao, hivyo wanaomba msaada wa kukarabatiwa kwa barabara hizo.

Irene Gabriel, Mathayo Peter, Muslim Issa na Patrick Mush wamesema mazingira wanayosomea shule ni mazuri, bweni zuri, asubuhi wanasoma na jioni wanachangamana na kuendelea na masomo, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni ubovu wa barabara.

Mmoja wa wanafunzi hao wa kike Irene na wa kiume Issa walisema,"kusema ukweli barabara imekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwetu wanafunzi japo shuleni hatuna matatizo makubwa ila tatizo kubwa tulilonalo ni hilo na mengine ni ya kawaida,"amesema.
Walisema kutokana na hali hiyo wanaiomba Serikali kuendelea kushirikiana na uongozi wa shule katika kutatua changamoto walizonazo ili waweze kuendelea kufanya vizuri zaidi tofauti na ilivyokuwa awali huku ikiendelea kulishughulikia suala la barabara.

Aidha walisema wanaishukuru Bodi ya Shule kwani imekuwa ikiwajali na kuwasaidia wanafunzi hao kama wazazi wao na kuiomba kuendelea kuwatatulia matatizo yao kwa wakati.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbondole, Juma Boniface Orenda alikiri kuwepo na ubovu wa barabara uliokithiri na hasa pale mvua zinapokuwa zimenyesha.
Alisema, hali ya barabara siyo mzuri jambo linalopelekea hata watendaji husika wakiwemo walimu kuchelewa kazini, kwani hakuna usafiri wa daladala hivyo mwalimu asipokuwa na hela ya bodaboda analazimika kutembea hivyo kumfanya kushelewa eneo lake la kazi.

Alisema mbali na changamoto ya barabara kuwa mbovu kupindukia, lakini baabdhi ya changamoto zingine ni mwamko mdogo wa wazazi kwenye usimamizi na ufuatiliaji maendeleo ya watoto kitaaluma ikizingatiwa na shule hiyo kuwa katikati ya wafugaji na wakulima pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo na kwamba kutokana na aina yao ya utafutaji wanashindwa kufuatilia maendeleo ya watoto.

"Lakini miundombinu hafifu ya barabara inaongeza gharama za usafiri kwa watumishi na wanafunzi kutokana na kwamba hakuna daladala, hivyo watumishi kulazimika kutumia bodaboda na kama hana fedha basi hulazimika kutembea kwa miguu huku wanafunzi wakitembea umbali mrefu hivyo kuwafanya wafike mashuleni wakiwa wamechoka sana au kusababisha utoro na kuchelewa,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news