Waziri Balozi Dkt.Chana awapa faraja waraibu dawa za kulevya, atoa wito kwa jamii

*Asema wana fursa sawa ya kuneemeka kupitia asilimia 10 ya mikopo ya halmashauri nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.Balozi Dkt.Pindi Chana amewataka waraibu wa dawa za kulevya waendelee kutumia fursa za kliniki za kuponya zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ili waweze kurejea katika hali ya kawaida kwa ajili ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Pia amewataka wale ambao wanapata dawa saidizi hususani methadone kuendelea kuzitumia kadri wanavyoelekezwa ili kuepuka changamoto ya kurejea katika hali za awali iwapo watasitisha utumiaji wake.

Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana ametoa rai hiyo leo Machi 16, 2022 baada ya kufanya ziara katika Kliniki ya Methadone iliyopo katika Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala ambapo inasimamiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).

Amesema, kila mraibu akitumia kikamilifu dawa kulingana na miongozo ya wataalamu wa afya zitawawezesha kurejea katika hali zao za kawaida.

Pia amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa, vijana wote wakiwemo waraibu wanaopona wananufaika kupitia fursa mbalimbali ikiwemo kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

"Hata wale wenye changamoto, waraibu wanayo haki ya kujiunga katika vikundi wakapata fursa hii, na mikopo hii inatolewa pasipokuwa na riba ya aina yoyote. Hizi ni jitihada za Serikali yetu za kuwasaidia wanawake na vijana, hivyo fursa hizi zinatolewa katika vikundi, ni muhimu sana vijana wakajiunga katika vikundi, kwani umoja ni nguvu. Kikundi chenye ndiyo dhamana, ya kurudisha fedha hizo ili wengine wapate.

"Na vijana wanaokuja mbele ya safari nao waweze kuendelea kupata fursa, kwa hiyo hizi fedha zinazotengwa asilimia 10 na halmashauri zinaendelea kuzunguka ili kuweza kunufaisha wanufaika wengi zaidi. Na vituo vyote vya Methadone, tunayo maafisa wa ustawi wa jamii.

"Kupitia maofisa wa ustawi wa jamii, natoa wito waweke taratibu za vijana hawa kuwaunganisha na maafisa wanaoratibu utoaji wa mikopo kwa vijana na wanawake ili waweze kunufaika kupitia mikopo hiyo kwa ajili ya kwenda kuzalisha,"amesema Waziri Balozi.Dkt.Chana.

Mwananyamala

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela amesema kuwa, Kliniki ya MAT Mwananyamala inahudumia wateja zaidi ya 1,350 kila siku ambao wanafika kunywa dawa.

Amesema, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwemo kuwaelimisha vijana wote wanaopatiwa huduma ili baada ya kupona waweze kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali kwa manufaa yao, jamii na Taifa.

Ustawi wa Jamii

Naye Afisa Ustawi wa Jamii anayesimamia kliniki hiyo, Hafsa Rashid Mtwange anasema kuwa, miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyochangia vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na makundi, hali ya maisha na ndoa.

Amesema, mara nyingi kila anapokutana na watumiaji wa dawa hizo ambao huwa wanafika katika kliniki hiyo kwa ajili ya kutafuta uponyaji wamekuwa wakizitaja sababu hizo.

"Peer groups (makundi), hii ni moja wapo ya sababu kubwa ambayo vijana wengi wanaofika hapa wamekuwa wakitaja kuwa ndiyo chanzo cha wao kujikuta wanatumia dawa za kulevya, wengine wamekuwa wakisema, hali ngumu ya maisha nayo imechangia wao kujikuta kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya na migogoro ya ndoa,"amesema Bi.Mtwange.

Waziri atoa rai

Baada ya kumsikiliza Afisa huyo, Waziri Mheshimiwa Balozi Dkt.Chana amesema kuwa, kwa upande wa suala la ndoa viongozi wa dini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusaidiana na Serikali kuhakikisha wanandoa wanaishi wakiwa na hofu ya Mungu, hatua ambayo itasaidia kukabiliana na migogoro ya mara kwa mara.

Pia amewataka maafisa ustawi wa jamii kuwahamasisha vijana hao kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau wengine nchini baada ya kupona.

Aidha, ameishauri idara hiyo kushirikiana bega kwa bega na idara nyingine vikiwemo vitengo vilivyopo halmashauri kama Mwanasheria wa Halmashauri ili pale ambapo kuna uhitaji aweze kushiriki kikamilifu kutoa huduma.

DCEA

Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi amesema kuwa, wameendelea kufikia kundi kubwa la waraibu wa dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha wanapata tiba saidizi kupitia vituo mbalimbali.

Dkt.Mfisi anasema kuwa, hadi Desemba mwaka jana zaidi ya waraibu 10,600 walikuwa wamehudumiwa kupitia vituo vya tiba saidizi kwa waraibu, vikubwa kwa vidogo vilivopo hapa nchini.

Amesema, kwa sasa wana vituo 15 ambapo kuna vinne vidogo huku 11 vikiwa vikubwa kwa ajili ya kutoa tiba saidizi kwa waraibu kwa kutumia dawa.

Vituo hivi husimamiwa na Serikali na huhudumia waathirika wa dawa ya kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Waathirika wanaotibiwa kwenye vituo hivi hutibiwa kwa kutumia dawa mfano Methadone. Waathirika wanatakiwa kuhudhuria matibabu kila siku mpaka watakapomaliza matibabu. "Huduma ya MAT hutolewa bure chini ya uangalizi wa wataalamu,"amesema Dkt.Mfisi.

Amevitaja vituo hivyo kuwa ni Kliniki ya MAT Muhimbili iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam,
Kliniki ya MAT Mwananyamala iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Kliniki ya MAT Temeke iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Temeke jijini Dar es Salaam

Nyingine, Dkt.Mfisi anasema ni Kliniki ya MAT Mbeya iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda jijini Mbeya,Kliniki ya MAT Mwanza iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Sekou Toure jijini Mwanza, Kliniki ya MAT Itega iliyopo Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe jijini Dodoma

Pia amesema kuna, Kliniki ya MAT Bagamoyo iliyopo Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Kliniki ya MAT Tanga iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Bombo jijini Tanga, Kliniki ya MAT Tumbi iliyopo Hospitali ya Rufaa yaMkoa ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani

Aidha, Dkt.Mfisi amesema kuwa, kuna Kliniki ya MAT Arusha iliyopo Hospitali ya Mkoa ya Rufaa yaMkoa, Mount Meru- Arusha jijini Arusha, Kliniki ya MAT Tunduma iliyopo Kituo cha Afya cha Tunduma mkoani Songwe, Kliniki ya MAT Segerea katika Kituo cha Afya cha Segerea jijini Dar es Salaam.

Dkt.Mfisi ametaja nyingine ni Kliniki ya MAT Tegeta iliyopo Kituo cha Afya cha Tegeta jijini Dar es Salaam, Kliniki ya MAT Mbagala iliyopo Zahanati ya Round Table-Mbagala jijini Dar es Salaam, Kliniki ya MAT Kigamboni iliyopo Hospitali ya Vijibweni-Kigamboni jijini Dar es Salaam

Amesema kuna faida nyingi za tiba ya methadone ikiwemo kundoa utegemezi wa dawa za kulevya aina ya heroine,kupunguza hatari ya mtegemezi kuwa katika hali ya kupata maambukizi ya HIV, homa ya ini na kifua kikuu.

Pia amesema, inaimarisha mwili na kumfanya mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida na inaboresha mfumo wa mwili na kupunguza hatari za matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa kuzidisha kiwango ikiwemo kupunguza vifo vya ghafla.

Mtaalamu

Dkt.Miriam Kabanywanyi kutoka katika Kliniki ya MAT Mwananyamala anasema kuwa, wamekuwa na jukumu kubwa la kuwajenga kisaikolojia waraibu hao wa dawa za kulevya, kwani kila anayefika kituoni hapo ana changamoto zake kubwa ikiwa ni kuathirika kisaikolojia.

"Hivyo, tunatumia muda mwingi kuwajengea uwezo kwa kuwaandaa kisaikolojia ili waweze kuyakubali mazingira ya kupatiwa tiba na baada ya 'kugraduate' (kuhitimu) waweze kuwa watu mwema katika jamii na kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao na jamii kwa ujumla,"amesema.

Waraibu

Miongoni mwa waraibu wameeleza kuwa, changamoto kubwa ambazo wanakabiliana nazo baada ya kuhitimu hatua hiyo ya kupatiwa dawa na kurudi katika hali ya kawaida ni pamoja na kukosa kazi za kufanya, hivyo kujikuta wanajiingiza tena kwenye makundi mabaya.

Aidha, Waziri Balozi Dkt.Chana amewaondoa wasiwasi na kuwataka kutambua kuwa Serikali inawathamini na kila mmoja atapata fursa ya kushiriki katika maendeleo iwapo watajiunga katika vikundi vya maendeleo katika jamii inayowazunguka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news