83,514 waomba ajira kupitia mfumo wa ajira TAMISEMI kwa siku tano, yatoa maelekezo 11

NA DIRAMAKINI

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imesema kwa sasa mfumo wa ajira unafanya kazi vizuri kwa kasi ya kutosha na hadi kufikika Aprili 25,2022 saa nne usiku waombaji wa Kada ya Ualimu walikuwa 69,813 na Kada ya Afya ni 13,683.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Aprili 26,2022 na Idara ya Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

"Jumla ya waombaji wote ni 83,514. Waombaji wote hawa wameomba kupitia mfumo ajira.tamisemi.go.tz kwa muda wa siku tano tu. Hivyo ni takribani waombaji 16,703 huwasilisha maombi kwa siku,"amesema.

UFAFANUZI WA MASUALA YA AJIRA KADA YA ELIMU NA AFYA
Ofisi ya Rais - TAMISEMI ilitoa Tangazo la Ajira 9,800 kwa Kada ya Ualimu na 7,612 kwa Kada ya Afya, Tangazo lilitolewa mnamo tarehe 20.04.2022.

Kufuatia Tangazo hilo, waombaji wa ajira hizi wamewasilisha changamoto mbamblimbali ambazo ambazo ufafanuzi wake ni kama ifuatavyo:

1. Mfumo wa Ajira kutofunguka - Kwa sasa mfumo wa ajira unafanya kazi vizuri kwa kasi ya kutosha na mpaka tarehe 25.04.2022 saa nne usiku waombaji wa Kada ya Ualimu walikua 69,813 na Kada ya Afya ni 13,683. Jumla ya Waombaji wote ni 83,514. Waombaji wote hawa wameomba kupitia mfumo ajira.tamisemi.go.tz kwa muda wa siku tano tu. Hivyo ni takribani waombaji 16,703 huwasilisha maombi kwa siku.

Waombaji ambao bado wanakutana na changamoto mbalimbali kama ni za kimfumo waangalie zaidi mtandao wanaotumia, eneo walilopo na taarifa wanazoingiza kwenye mfumo. Aidha, wahakikishe kuwa taarifa zao ni sahihi na wanatumia mtandao wenye kasi wakati wa uingizaji wa taarifa katika mfumo..

2. Kigezo cha Mwaka kwa ajira za Kada ya Ualimu kuanzia mwaka 2015-2021 - Hii ni kwamba wahitimu wa miaka ya nyuma wengi waliajiriwa moja kwa moja Serikalini na wale waliokuwa wamebakia na wana sifa waliajiriwa kwenye Ajira zilizotangazwa mwaka 2018 - 2020 hivyo kwa sasa tunaendelea na wahitimu ambao walianza na mfumo wa kutoajiriwa moja kwa moja Serikalini ambao ulioanza kufanya kazi mwaka 2015.

3. Kugonga Muhuri vyeti vya Kitaaluma - Hiki sio kigezo muhimu katika uombaji wa ajira hizi unaweza kuomba bila kugonga muhuri kwa Mwanasheria na maombi yako yakapokelewa na kufanyiwa kazi.

4. Lugha inayotumika kuandika barua ya maombi - Waombaji wanaweza kutumia lugha yeyote (Kiswahili au Kingereza)kutuma maombi yao.

5. Wasifu - Hakuna sehemu ya kuweka wasifu kwenye mfumo wa ajira hivyo waombaji wote wafuate maelekezo yaliyopo kwenye mfumo.

6. Waombaji kujisajili upya - Waombaji wote wanatakiwa kujisajili na kufungua akaunti mpya hata kama alishawahi kuwa na Akaunti aliyotumia kuomba ajira zilizopita ndio aendelee na maombi ya ajira za mwaka 2022.

7. Kutoonekana kwa baadhi ya Mikoa na Halmashauri wakati wa kuchagua kituo cha kazi - Kwa sasa Mikoa na Halmashauri zote zenye uhitaji wa watumishi wa Kada ya Ualimu na Afya zinaonekana kwenye mfumo: Kwa wale waliokutana na changamoto hii hapo awali wanaweza kujaza tena kipengele hiki.

8. Baadhi ya kozi kutokuwepo kwenye mfumo – Kwa sasa kozi zote za vyuo vilivyosajiliwa TCU na NACTE zimewekwa kwenye mfumo kama utaendelea kukutana na changamoto hii wasiliana na kituo cha huduma kwa mteja kwa msaada zaidi.

9. Kutoonekana kwa somo moja la kufundishia - Kwa mujibu wa kibali cha Ajira masomo yote yaliyopata kibali yameingizwa kwenye mfumo kama utakua huoni somo la pili la kufundishia itakua somo hilo halipo kwenye kibali cha Ajira.

10. Kufuta taarifa uliyoiweka kimakosa/uliyokosea - Kama umeweka taarifa ambayo unadhani unataka kuifuta mfumo umewezeshwa kuweza kuondoa taarifa hiyo na kuweka nyinginge mpya.

11. Unapopata ujumbe wa something went wrong contact the system admin wakati wa kutumia mfumo – Ujumbe huu unatokana na shida ya mtandao. Muombaji anashauriwa abadili mtandao/network na kujaribu tena. Mara nyingi huwa si tatizo la kuduma iwapo mawasiliano yatakuwa vizuri

Maombi yote ya Ajira hizi ni bure na yanaombwa kwenye mfumo kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz.

Endapo utapata changamoto yeyote piga Kituo cha Huduma kwa Mteja kupitia Namba 0735-160210 au 0262-160210 au tuma barua pepe kupitia huduma.tamisemi.go.tz.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

2 Comments

  1. Mtakao waajiri mjina yao mtatoa lini?

    ReplyDelete
  2. Changamoto ya kukosea email au kuhifadhi nakala haifunguki na pia hata kwa sms kutokupata tovuti na nywila tufanyaje

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news