KMC FC:Tunaelekea Kanda ya Ziwa kuzikusanya alama sita

NA DIRAMAKINI

KIKOSI cha wachezaji 24, benchi la ufundi pamoja na viongozi wa KMC FC wataondoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Kagera kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Jumapili ya Aprili 17 katika uwanja wa Kaitaba mkoani humo.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari na Mawasiliano wa KMC FC, Bi.Christina Mwagala.
Mbali na mchezo huo, KMC FC pia itakuwa ugenini dhidi ya Geita Gold FC Aprili 23, mchezo ambao utapigwa katika uwanja wa Nyankumbu ambapo hadi sasa,Mwagala amesema, maandalizi yapo vizuri chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana ya kuzisaka alama sita muhimu katika timu hizo zilizopo Kanda ya Ziwa.

Amesema, katika mchezo huo dhidi ya Kagera Sugar, KMC inaendelea kujiimarisha ikiwa ni mara baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Namungo ambao ulichezwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Aprili 3, mwaka huu.

Pia amesema, timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imejipanga kwenda kufanya vizuri kwenye michezo hiyo kwa Kanda ya Ziwa licha ya kwamba Kagera na Geita ni timu nzuri na kwamba zimekuwa zikifanya vizuri kwenye michezo yake.

“KMC tunakwenda Kanda ya Ziwa, kutafuta alama sita kutoka kwenye timu ya Kagera Sugar pamoja na Geita, tunafahamu kuwa timu hizo ni nzuri na zimekuwa na matokeo mazuri kwenye michezo yao, lakini hiyo haituzuii Manispaa ya Kinondoni tukashindwa kupata alama zote kwa sababu zipo ndani ya uwezo wetu.
“Tunawachezaji bora na wenye uwezo wa kuipa timu matokeo kwenye mazingira yoyote yale, siku zote timu yetu ni imara, haijalishi hatujapata matokeo mazuri hivi karibu kwenye michezo mitatu iliyopita, hivyo tunahitaji ushindi kwenye michezo yetu, tunakwenda kwa tahadhari kubwa huku tukimtanguliza mwenyezi Mungu,"amesema.

Wakati huo huo, kwa upande wa afya za wachezaji, amesema wote zipo vizuri, "wana hari na morali, licha ya kwamba tutakuwa ugenini, lakini tunakwenda kuipambania timu yetu, tunahitaji kuwapa furaha mashabiki wetu, manispaa yetu ya Kinondoni, na Watanzania wote ambao wanatusapoti, na kikubwa zaidi hatufikirii michezo ambayo ilishapita badala yake 'tuna focus' kwenye michezo iliyopo mbele yetu,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news