OR-TAMISEMI yazipa halmashauri siku saba kutoa taarifa

*Ni zile zilizopatiwa fedha kujenga shule za sekondari za wasichana

NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.David Silinde ameziagiza halmashauri zote nchini zilizopatiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kuandika taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya ujenzi wa shule hizo na kuziwasilisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI ndani ya siku saba.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Kibaigwa leo Aprili 5, 2022 Mhe. Silinde amesema kuwa, halmashauri hizo zinatakiwa kuleta taarifa ya kina inayoonyesha matumizi ya thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo.

Mhe. Silinde amesema kuwa jumla ya shule za wasichana 15 zinajengwa katika halmashauri nchi nzima ambapo kila shule ilipelekewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo. 

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaigwa Mhe. Silinde amesema, hakuridhishwa na ubora wa majengo yaliyojengwa katika shule hiyo, matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi huo na thamani ya fedha zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambayo hadi sasa haijakamilika.
"Sijaridhishwa na ujenzi wa shule hii, kwa kuwa majengo yanaonekana kwa nje yamekamilika, lakini ndani hayajakamilika, ujenzi wa majengo hauridhishi kabisa, hii ni hujuma ya kutaka kuwaonyesha wananchi kuwa Serikali haikamilishi miradi yake kwa wakati,"amesema Mhe. Silinde.

Mhe. Silinde amesema kuwa, hatasita kuwachukulia hatua wale wote ambao watashindwa kukamilisha ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kwa wakati kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha elimu bora inatolewa katika mazingira bora.
Aidha, Mhe. Silinde amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuhakikisha wanatafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa shule hiyo kwa kuwa Serikali haipo tayari kutoa kiasi cha shilingi milioni 464.5.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt.Omary Mkulo ameeleza kuwa, kiasi cha shilingi milioni 464.5 zinahitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa shule hiyo ambayo hadi sasa imefika asilimia 68. 14 ujenzi na fedha iliyotumika ni shilingi milioni 993.8.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news