Polisi aliyefutwa kazi, kunusurika kifo kwa utumiaji dawa za kulevya alivyogeuka kuwa nuru kwa Waraibu Tanzania-4

NA GODFREY NNKO

“Basi ndugu zangu wakawa wananishawishi niende Arusha kwa ndugu, lakini Anko wangu akasema hata akipelekwa huko watamkamata ni karibu, bora apelekwe jela wakati huo huo watu walishazingira nyumbani, siwezi kutoroka tena.

“Likaja gari la Noah wakanipakiza humo, wakanunua mafuta ya petroli na kibiriti wakanipeleka mpaka Kituo cha Polisi, wakanirushia hapo na mafuta wakasema tulitaka kumchoma moto, siku hiyo nakumbuka ilikuwa Jumapili ya tarehe 14 siku wanamzika Mandela Rais wa Afrika Kusini mwaka 2013,nimekaa pale kituoni vikaletwa vile vitu tulivyoviiba usiku maana tuliviacha nje basi nikaendelea kukaa pale kituoni na mwili ukapelekwa mochwari Mawenzi;

Bw. Twaha Amani ambaye alifukuzwa kazi ya uaskari na baadaye ualimu shule ya sekondari kutokana na matumizi ya dawa za kulevya anasema,petroli waliyonunua pamoja na kibiriti ile ilikuwa ni kumsingizia kuwa alikuwa anataka achome moto nyumba wanayoishi kama gia tu ya kumpeleka jela.

“Na mimi nilikaa pale mpaka Krisimasi ikanikutia pale maaana hapakuwa na mtu wa kuja kutoa maelezo, nikapelekwa Gereza la Karanga, nikakaa miezi sita ilikuwa 2013 nikatoka 2014 nikiwa nimependeza sana, maana huko jela nilikutana na waliotuhumiwa kumuua Erasto (Bilionea wa madini ya Tanzanite, marehemu Erasto Msuya) waliposikia naitwa Teacher. Endelea sehemu ya nne...
"Sasa kuna mmoja wao anaitwa Sharifu aliyekuwa kwenye kabineti ya waliotuhumiwa kumuua akaniomba niwe ninamfundisha, basi nikaanza kumfundisha, nikawa ninakula chakula chao maana hao jamaa ni matajiri sana, walikuwa wanaletewa chakula kila siku mpaka nikahamia kwenye sero yao, lakini lazima ufuate masharti yao ya kuswali na uwe Muisilamu, lakini kwa kuwa nilikuwa napenda kusali nikawa naswali huku ninamfundisha.

Safari ya Sobber House

“Sasa baada ya kukaa pale jela miezi sita, nikaenda mahakamani siku hiyo nikaambiwa kesi yangu imefutwa, mama yangu alinitoa gerezani kumbe alishaongea na hakimu maana ile kesi ilikuwa ni ya nyumbani, lakini mbali na kunitoa nikarudi nyumbani kuanza kuvuta tena unga.

“Wakati naendelea kuvuta unga maskani kuna mabwana walitoka Zanzibar, wakawa wamekuja Moshi kule Bomang'ombe, wakafungua Sobar House kama hii ya kwangu, awali wakawa wanahangaika mtaani wanafanya outreach, wakawa wanatafufa watu wenye uwezo ili waweze kuwasaidia kuwalipia.

Nyumba za upataji nafuu (Sober House) ni nini?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ni sehemu ambayo huwasaidia waraibu ambao bado wako kwenye matumizi ya vilevi kuachana navyo au kupata nafuu kwa kutumia hatua 12 za upataji nafuu pamoja na unasihi.

Huduma katika nyumba za upataji nafuu huendeshwa na asasi za kiraia ambapo waraibu wa dawa za kulevya wanapata huduma kwa kupitishwa kwenye hatua hizo bila kutumia dawa ya aina yoyote.

Matibabu haya hutolewa kwa malipo kwa waraibu wa dawa zote za kulevya kwa muda usiopungua miezi minne.

Serikali inaratibu uanzishwaji na kusimamia uendeshwaji wa Nyumba za Upataji Nafuu kwa kutumia Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Nyumba za Upataji Nafuu Tanzania Bara.

Hadi kufikia mwezi Februari 2022, kulikuwa na jumla ya nyumba 45 zinazotoa huduma hiyo katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Dares Salaam,Pwani, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mwanza, Kagera, Tabora na Arusha.

Katika huduma hii watumiaji wa dawa za kulevya husaidiana wenyewe kwa wenyewe ambapo waraibu waliopata nafuu (kuacha matumizi ya dawa hizo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja) huwaongoza waraibu wanaojiunga kushiriki mikutano ya Ustiri wa Mihadarati, (Narcotic Anonymous) ambapo hupitishwa kwenye hatua kumi na mbili za upataji nafuu pamoja na unasihi.

Waraibu wanaojiunga huweza hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali, kazi za mikono pamoja na kushiriki katika shughuli za michezo.

“Wakaulizia wakaambiwa kwetu kwa akina Twaha maana kwetu ni familia maarufu na tulikuwa na uwezo kidogo wakafika nyumbani, wakawaeleza kuwa ninaweza kwenda hapo basi mimi nilikuwa shamba nikapigiwa simu kupitia namba ya mfanyakazi wa shamba niongee na Anko wangu akaniambia niende nyumbani, kwani kuna watu wananitafuta, nikajua nilishaharibu nikakataa kwenda.

“Baadae wakapiga tena nikakataa nikasema nimeshaharibu maana ukiwa unavuta unga (heroine) kila kitu unashtuka basi jioni kabla ya kwenda nyunbani nilikuwa namtafuta kijana anayejua kukwea minazi mirefu ili akwague nazi nazipeleka kwa anayeuza unga (heroine) ninampatia ananipa unga, navuta,basi usiku nilirejea nyumbani ninaenda kinyatunyatu…

"Nilipofika nikamfuata Anko wangu kwenda kumuuliza usiku ili nijue akina nani walikuwa wananitafuta au nimeshaharibu nini? Akaniambia kuna jamaa wamefungua Sober House walikuwa wananitafuta wanataka niende huko akaniuliza kama nipo tayari, nikasema nipo tayari.

Atoroka Sober House

“Kweli bwana, nimekaa...mama yangu akawa amerejea kutoka kazini, wakampa hizo taarifa akazipokea akaridhia niende, tumekaa kama siku nne hivi maskani navuta unga mara ghafla nikawaona wanakuja tena wakanieleza faida, basi nikakubali kuondoka nao tulifika huko Bomang'ombe kwenye Sober yao, lakini mazingira sikuyaelewa maana kama walikuwa hawajajipanga, hapakuwa na magodoro, nikaona ni mazingira magunmu, nakumbuka ilikuwa siku ya Kombe la Dunia nikawadanganya nataka nikaangalie mpira wakaniambia kwa kuwa hawana TV, watakuwa wanatupeleka nje kuangalia na kurudi.

“Sasa ikabidi niruke ukuta niende kuvuta unga, nikaenda mpaka kazini kwa mama akashangaa nikamdanganya mama kwamba wale jamaa ni matapeli, hapaeleweki mama alichukia sana na ukizingatia alikuwa hajalipa, alitaka nimalize mwezi,basi alinipa elfu tano niende nyumbani ila mimi nikapita mtaani nikavuta unga nikaenda nyumbani.

Hali yabadilika

“Nikiwa nyumbani hali ilianza kuwa ngumu zaidi ya mwanzo, nikapata mateso makubwa ikawa kama laana kabisa, nikakaa kama miezi mitatu baadae ikabidi nirudi mwenyewe kule Sobar kuomba msaada, basi nilikuta kumebadilika sana, kuna viti,magodoro yameongezeka na watu wameshafikia 16 na tulikuwa watatu mwanzoni.

“Ilipofika mwaka 2016, nikiwa pale Sobar House, kama mwaka mzima na nusu kukatokee kama ugomvi na mwenye Sober akaniambia niondoke, akanifukuza...basi nikarudi nyumbani nikaanza kuvuta tena unga kwa sababu sikutoka hapo kwa wema,"anasema Bw.Amani.

Anasema, kipindi hicho ambacho alikuwa nyumbani alianza kufuatilia vyeti vyake ambavo aliviweka bondi kuanzia mwaka kule Mwanza 2012.

"Kwa bahati nzuri yule bwana kule Misungwi Vijijini mkoani Mwanza aliyekuwa na vyeti vyangu alikuwa na duka hapo kijijini karibu na barababrni nilimkuta ila alinishangaa sana kwa sababu miaka ilikuwa imepita mingi.

"Kwanza kabla ya yote nilitaka nipate uhakika kutoka kwake kama veti anavo au la,kwa kweli jibu lake lilinishangaza aliniambia anavyo na kuna mtu alishawahi kumshawishi ampe milioni moja ili ampe vile veti, lakini yule jamaa akagoma,akasema kwa kuwa alinikopesha 30,000 na miaka imepita mingi basi alihitaji nimpe, laki moja ili anipe vyeti vyangu, nami nilifanya hivyo, wakati huo nipo na kaka yangu ninayemfuata ndiye alinisindikiza, basi nikachukua vyeti vyangu tukarudi Moshi,"anasema Bw.Twaha.

Wizi kupitia kazi ya Mjomba

“Nilikuwa na stress (msongo) basi mama yangu akaniambia niwe na Anko wangu ana magodauni ya kusaga mpunga na kuuza mpunga na mashamba, sasa akanipa kitengo huko, nikaanza kuuza michele ya watu basi nikaanza kuvuta unga (heroine) na kuanza kuiba vitu vya watu.

“Nikaja nikapata matatizo nikaenda kuiba kwenye nyumba moja nikafuatwa hapo hapo mashine, wakasema huyu mchana yuko mashine, usiku anaenda kuibia watu walinipeleka wakanipiga kweli, ila Anko wangu akapigiwa simu kumwambia ninapigwa, akafika hapo akakuta napigwa sana akaanza kuwagombeza kwa nini mnampiga si mngepeleka polisi?.

“Basi nikapelekwa nyumbani mama yangu aliponiona akawa amechanganyikiwa ikabidi awapigie wale wa Bomang'ombe akawabembeleza nirudi huko, basi wale jamaa wakisikia mtu karudia wanafurahi ili wapate hela, basi akaja msaidizi wake akawa ananisema kama anafurahi kurudia kuvuta akaniambia ulijifanya unaondoka mbona yamekushinda, umeanza kuvuta na umerudi huku.

Arejeshwa Sober House

“Basi niliporudi hapo Sober 2016 nikaanza upya na kwa kuwa nilikuwa nimekaa sana nikaanza kuwa nafundisha watu mambo yakawa mazuri. Kwa sababu nilikuwa nimesoma ninajua mambo mengi kuliko wahusika wa hiyo Sober wote wameishia darasa la saba, kwa hiyo nilikuwa ninaandika barua nyingi, najua matumizi yanakwendaje na barua kwenda kwa viongozi tayari nikawa na cheo,"amesema.

Katika hiyo Sober anasema Mwendeshaji alikuwa amemaliza kidato cha nne huku Meneja wa Nyumba hiyo ya upataji nafuu akiwa ameishia darasa la saba na yeye Bw.Twaha Amani ambaye alikuwa Meneja Msaidizi alikuwa amefika hadi ngazi ya chuo.

“Baada kama miaka mitatu nikataka kuondoka,mmiliki wa Sober akakataa, akaniomba nikae hapo na atanilipa na marupurupu jumla laki moja, nikaona ni pesa ndogo ila nikaendelea kufanya kazi, sasa wakati nipo Sober kulikuwa na dada jirani ambaye alikuwa analeta kuku tumchinjie, maana kwao walikuwa ni Waislamu.

Itaendelea chapisho lijalo hapa DIRAMAKINI BLOG...

Post a Comment

1 Comments