Polisi aliyefutwa kazi, kunusurika kifo kwa utumiaji dawa za kulevya alivyogeuka kuwa nuru kwa Waraibu Tanzania-6

NA GODFREY NNKO

"Mwaka 2021 nikiwa hapo hapo Sober Bomang'ombe (Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro) baada ya kuona majukumu yameshakuwa mengi mtoto anakuwa na chumba kimoja hakistahili tena,ikabidi nijaribu kwenda tena Mwanza katika Halmashauri ya Misungwi kwenda kufuatilia ajira yangu niliyoajiriwa mwaka 2012 ila baada ya kukutana na Afisa Elimu alinikutanisha na Afisa Utumishi.

"Nikaongea nae kwa kina na kumwambia matatizo ambayo niliyapitia alinisikiliza vizuri sana mpaka mwisho akaniambia...daaah pole sana, Endelea sehemu ya sita..

Hakuna kazi tena

"Sasa ipo hivi (Afisa Utumishi anamweleza Twaha Amani), wakati Magufuli (hayati Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli) anaingia madarakani 2015 alifanya mabadiliko makubwa sana kwenye wafanyakazi hewa, mishahara hewa pamoja na vyeti feki, kwa hiyo ni bora nianze ku-apply upya,basi baada ya kuniambia hivyo ikabidi nirudi zangu Moshi, kule Bomang'ombe Sober kwa kuwa huko ndipo nilikuwa nikifanya kazi na kupata riziki, huku nikiwa nimepanga chumba kimoja mimi na familia yangu.
Mkufunzi na Mkurugenzi wa Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda (Himo) Sober House mkoani Kilimanjaro,Bw.Twaha Amani akitoa mafunzo kwa waraibu ambao wapo katika kituo hicho ili waweze kujinasua katika janga hilo. (DIRAMAKINI).

"Kwa hiyo nikawa ninaendelea kutafuta kila namna ili kupata riziki ya kusaidia familia yangu,kwa sababu tayari kulikuwa kuna watu wawili wananitegemea, mtoto anakuwa, ikanilizamu kutafuta vyumba viwili, pale pale ikabidi nitafute vyumba viwili kwa shilingi 120,000, ile shilingi 100,000 ambayo nilikuwa ninalipwa pale Sober House ikawa haitoshi. Mambo yanazidi kuwa magumu.

Maisha magumu

"Watu wanatakiwa wale, kununua gesi, umeme, kulipia king'amuzi (DSTV) ile hela ikawa haitoshi chochote, nikamuomba bosi wangu aniongezee, lakini hataki, anasema nitakuongezea nitakuongezea... hakawa hataki, ikaonekana amekuwa mbinafsi kupita kiasi.

"Basi tukaendelea hivyo hivyo, mambo yakazidi kuwa magumu kwangu. Ilipofika mwaka 2021, kwa sababu tayari nimeshakuwa na uzoefu wa kutosha wa hii programu wa kufundisha watu, nikapata fedha yangu mahali kama shilingi milioni 10, ndiyo na mimi nikasema nije kufungua Sober yangu huku Njia Panda (Himo).

Kufungua Sober

"Baada ya kupata mhamko wa kuja kufungua Sober yangu huku Njia Panda, kuna Bwana tulikuwa tunafanya naye naye kazi pale Sober, nikampa taarifa awali alikuwa ananiambia kuwa Twaha, bwana tuko hapa tunafanya kazi, lakini hatupati kitu chochote, maisha yanazidi kuwa magumu.Nikamwambia ninataka kwenda kufungua Sober Njia Panda, je? Upo tayari tukafanye kazi.

"Kumbe yule Bwana ninamueleza mambo yangu na yeye ananizunguka, akaenda kwa bosi wangu akamueleza kila kitu ili nifukuze ili aweze kukaimu nafasi ya assistant manager (meneja msaidizi) ambayo nilikuwa nayo, sasa nikiwa nyumbani ilikuwa tarehe 31, mwezi wa 10 siku ya Jumapili, mwaka 2021 ndiyo naenda Sober,ambapo nilikuwa naenda kugawa dawa, ninafika Sober.

"Nilipofika getini nje nikaona kama kuna hali ya tofauti, wana kikao chao, walishanijadili tangu jana ili nikifika pale wanifukuze, basi yule bosi wangu akaanza kunitukana matusi yote ya nguoni na kunifukuza akisema kumbe unataka kufungua Sober bwana, nikamwambia sasa kufungua Sober yangu ndiyo unitukane na kunifukuza. Shida ipo wapi hapo?

"Akaniambia ondoka sikuhitaji hapa, na hata nilikuwa sijapata hata nyumba ya kupanga wala sijaandaa chochote na wakati nilitaka nikishafanikiwa ndipo nitoe taarifa kwa bosi wangu.

"Basi ilibidi niondoke nirudi nyumbani kwa uchungu na mawazo, nilipofika nyumbani mke wangu akaona sipo sawa kabisa, nikamwambia nimefukuzwa, akaniambia nilikwambia usiwe unamwambia mtu mambo yako, angalia sasa hata hujafanya chochote.

Kazi inaanza

"Nikiwa nyumbani na mawazo ikabidi nianze kwenda Njia Panda kufuatilia mambo yangu ya nyumba na mambo mengine niliipata nikalipia kila kitu na baadae nikaenda Arusha kumtafuta mwana sheria kwa ajili ya kunitengenezea taarifa.

"Hali hiyo ikanisaidia kufanya mambo yangu vizuri, maana pale Sober nilikuwa nabanwa ,nilikuwa wa kwanza kufika na wa mwisho kutoka hapo Sober (Bomang'ombe) lazima niwape watu wote dawa.

"Ndipo safari ikaanzia hapo ila kuna dada mmoja yuko Wizara ya Maendeleo ya Jamii ana cheo cheo huko akanipigia simu, akaniambia Twaha unaweza kuanza kukusanya watu kwa kuwa mchakato wa leseni yako unaendelea vizuri, haina shida, haikuzuii uko kwenye 'process' nzuri, hizi nyumba za Sober House zinaruhusiwa kuanza

"Nikaanza taratibu watu wachache, mara wanane mpaka watu kumi sikukata tamaa. Mchakato ulianzia hapo, nashukuru Mungu mpaka sasa nina clients 27 na yule jamaa niliyekuwa naye Tabora alikuja kunipigia simu baada ya kujua nimefungua kituo kwani alishindwa kuacha unga ilibidi aje ambapo tuko wote hapa,"amesema Bw.Twaha Amani.

Wito wa Twaha

"Vijana tuachane na makundi ambayo hayana umuhimu kwetu, tujikite katika mambo ambayo yanalenga kutuwezesha kuzifikia ndoto zetu, kufanya kazi kwa bidii, kuachana na vishawishi ambavyo havina tija.

"Mimi nilianguka, sasa nimesimama tena nikiwa imara, nitasonga mbele kwa kuhakikisha ninashirikiana na jamii, Serikali ili kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kuelvya tunaishinda, Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana,"anasema Bw.Twaha ambaye kwa sasa ni mkufunzi na Mkurugenzi wa Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda (Himo) Sober House mkoani Kilimanjaro, lakini pia shuhuda mzuri wa yale aliyopitia.

Wanamzungumziaje

Bw.Nongwe S. Nongwe ni miongoni mwa watu ambao wanamfahamu kwa karibu, Bw.Twaha Amani kutoka Pasua mkoani Kilimanjaro anasema kuwa, miaka zaidi ya 15 iliyopita walisoma pamoja katika Kidato cha Tano na Sita Shule ya Sekondari Singe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara.

"Ili uwe mwalimu, lazima uwe umepitia ama unakijua unachokifundisha.Wakati ninamfahamu, tulikuwa kidato cha tano Singe High School, moja ya kitu ninakikumbuka alikuwa mtanashati sana (smart) muda wote, aliijua dini, lakini pia alikuwa akivuta bangi.

"Tulikuwa watano tukijiita GoatFaceFamily (GFF) japo kwenye matumizi ya bangi hakupata mshirika, japo hatukumtenga kwenye mambo mengine ya kijamii.

"Baada ya kumaliza, pamoja na mambo mengine aliamua kuwa mlevi sana, lakini pia akawa mvuta unga mahiri sana (drug user).Kwa umahiri huo, ulimsababishia kufukuzwa kazi ya upolisi ambao alidumu kwa miaka miwili, lakini pia ualimu ambao aliutumikia kwa mwaka mmoja tu.
"Mama yake mzazi ni miongoni mwa waathirika sana na uteja wake (Twaha Amani),ukiacha fedheha aliyompa, pia alimfilisi kwa kumuibia vitu vya ndani na pesa.

"Baada ya kuishi miaka mingi ya uteja, na kupitia magumu aliamua kuingia Sober House ambapo alikaa zaidi ya mwaka mmoja, na kuamua kubadilika na kuwa mtu poa, na baadae kuwa moja ya wanafunzi wazuri, na akabakizwa chuo (Sober House) kama mkufunzi amapo aliweza kuwasaidia wengine wenye hali aliyopitia.

"Huyo ndiye Twaha ambaye baadae aliamua kufungua Sober House yake, na kupitia hiyo amekuwa akisaidia watu tofauti, wenye addiction (vilevi) tofauti kama madawa ya kulevya (dawa za kulevya), uvutaji wa bangi na ulevi wa pombe akiwa kama, Mkurugenzi, Mkufunzi wa Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda (Himo) Sober House lakini pia shuhuda mzuri wa yale aliyopitia.

"Baada ya miaka 15, nilimtembelea nyumban kwake, kazini kwake nimeshuhudia jinsi Mungu alivyombadilisha Twaha Amani ambaye kwa sasa anaishi na familia yake (mke na mtoto) pia ni mcha Mungu sana. 'God bless you Twaha (Mungu akubariki Twaha), lipo la kujifunza,"anasema Bw.Nongwe.

Mama afunguka

Katika mahojiano maalumu na DIRAMAKINI BLOG, mama mazazi wa Bw. Twaha Amani, Bi.Hadija Shayo anasema kuwa, anamshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kumvusha katika kipindi cha miaka zaidi ya 10 chenye mapito magumu ya kupanda na kushuka milima na mabonde isiyokuwa na nuru kwa mtu ambaye ang’ekata tamaa katika maisha yake.

“Ni kipindi ambacho ilifika mahali nikakata tamaa, lakini nikafikia hatua nikajiuliza nikakata tamaa kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa mimi, niliamua kujipa moyo nikaamua kujitolea kwa hali na mali ili kumuokoa mwanangu katika tabu alizokuwa anapitia.

“Nilitumia rasilimali fedha,hekima, maarifa na akili nyingi kuhakikisha ninafanya kila linalowezekana ili kumuondoa mwanangu Twaha katika uraibu wa dawa za kulevya,wakati mwingine nilihisi nimefanikiwa kumnasua huko, lakini kumbe ninapojipa moyo nimemnasua huko, naye ananizunguka anaendelea kuyavuta,yaliharibu kabisa mipango ya maisha yake,”amesema Bi.Hadija Shayo ambaye pia aliwahi kuwa mtumishi wa umma katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro kabla ya kustaafu hivi karibuni.

Bi.Hadija anasema kuwa, Bw.Twaha uvutaji wa unga (heroine) ulianza kuchachamaa tangu alipoanza ajira ya uaskari wa Jeshi la Polisi mkoani Tabora mwaka 2008, ingawa kumbe hakuwa na taarifa kama tabia za uvutaji dawa za kulevya zilianza miaka ya nyuma akiwa shuleni.

Anasema, kama angefahamu kuwa, mwanaye alikuwa anjihusisha na dawa za kulevya mapema angetumia kila mbinu kuhakikisha anakaa naye ili kujifunza na kufahamu vishawisi ambavyo vilikuwa vinamhamasisha aweze kuyatumia, lengo likiwa ni kumtenganisha navyo ili aweze kuziendea ndoto zake.

“Ilikuwa ni ndoto yangu, mwanangu aweze kuwa na kazi nzuri, itakayomuwezesha kuendesha maisha yake, Twaha ni mtoto wangu, mwenye moyo wa huruma na upendo, mchapa kazi na bidi. Lakini kutokana na ile hali iliyomkuta alijikuta ghafla amefifisha malengo yake, nililia, nilikata tamaa, nilisemwa na kunyooshewa kidole.

"Kwa sababu familia yangu ni ya watu maarufu sana hapa mjini Moshi, lakini machozi yangu niliyaelekeza kwa Mwenyenzi Mungu mwingi wa rehema, nilimkabidhi Twaha mbele zake, nilitoa sadaka maalumu kwa ajili ya maombezi kwake ili tu, aweze kurejea katika hali yake ya kawaida,na baada ya miaka zaidi ya 10 Mwenyenzi Mungu alisikia kilio changu, akatoa jawabu.

“Ninamshukuru sana Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema kwa namna ambavyo aliweza kunipigania na kunipa ujasiri katika kipindi chote cha mapito magumu,si kwa uwezo wangu wala kwa nguvu zangu, bali kwa msaada wa Mungu,”amesema Bi.Hadija Shayo ambaye alikuwa anazungumza huku akionekana kutokwa na machozi.

Alipoteza vitu

Bi.Hadija anasema, wakati wa kuhakikisha kijana wake, Bw. Twaha anarejea katika hali yake ya kawaida alitumia rasilimali fedha nyingi ikiwemo kulipia gharama kwa ajili ya Sober House,kumtoa katika vituo vya polisi na mahakamani ili aweze kurejea nyumbani.

“Wakati mwingine, mwanangu aliponea kuuawa kutokana na wizi wa mali za watu ili aweze kupata fedha kwa ajili ya kununulia hayo madude machafu (unga-heroine),Fedha ambazo nilikuwa ninatumia ilikuwa ni sehemu ya mshahara wangu, nilijikuta ninashindwa kutimiza malengo mengine kwa ajili ya maendeleo katika familia ili kuhakikisha ninamsaidia,”anasema Bi.Hadija.

Anasema, jambo ambalo lilkuwa linamsononesha ni pamoja na wakati mwingine, Bw.Twaha alifikia hatua ya kumuibia hadi kanga zake, nguo na mashuka kwa ajili ya kwenda kuziuza ili akanunulie unga.

“Sasa unajikuta katika wakati mgumu sana katika maisha, maana fedha unazopata unazitumia kwa ajili ya kumuwezesha aweze kundoka huko alipo, lakini wakati huo huo kile kinachopatikana na chenyewe kinachukuliwa, ilifika hatua hata akitandikiwa shuka, unakuta ameshalichukua na kuondoka nalo, ilikuwa tabu sana, ila ninamshukuru Mwenyenzi Mungu,”amesema.

Waenda mbali zaidi

Kutokana na matendo ambayo yalikuwa yanafanywa na Bw.Twaha, mama yake amesema kuna wakati ulifika wakaamua kwenda mbali zaidi wakiamini labda chanzo kinatokana na mizimu ya kifamilia.

“Tuliamua kwenda kwa upande wa familia ya baba yake ili kuangalia kama matendo ambayo alikuwa anayatenda yanatokana na mizimu ya upande huo, baada ya wazee kuangalia wakaona hamna kitu, tukarejea kwa upande wa familia yangu, wazee wakaangalia wakaona hamna kitu. Kikubwa ambacho nilibaini kilimfanya Twaha kujikuta katika uraibu hatari namna hiyo ilikuwa ni ushawishi na makundi ambayo alikuwa anakutana nayo,”amesema.

Wito

Bi.Hadija ameiomba Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuongeza nguvu kubwa ya kudhibiti biashara ya dawa hizo kuanzia mijini hadi vijijini na kuhakikisha wanayazuia kuanzia nchi kavu, angani na baharini ili yasiweze kupenya kuingia nchini Tanzania.

“Kwa sababu, dawa za kulevya ni kati ya matishio makubwa ya usalama wa rai na mali zao, uvutaji huo unashawishi mambo mengi ikiwemo wizi, uharibifu wa mali na kudhoofisha utendaji kazi, hivyo kuwafanya vijana kudhoofika kiafya na kushindwa kufanya kazi za kuwaingizia kipato na hata kulitumikia Taifa,”anasema Bi.Hadija.

Anasema, wazazi ambao wana watoto waliopitia au wanapitia mapito kama yake, hawapaswi kukata tamaa bali wajitolee kuwaombea kwa Mungu na kusaidia kwa hali na mali ili kuwaondoa katika uraibu.

Pia amesema, elimu dhidi ya masuala yahusuyo dawa za kulevya inapaswa kuwa ndani ya mitaala au somo la lazima kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu ili vijana na watoto waweze kujifunza kuhusu athari za kujiingiza katika biashara, utumiaji au kwa namna nyingine yoyote kwa lengo la kukiandaa kizazi kinachotoa kisogo kwa dawa za kulevya na kujikita katika mambo ya msingi kwa ajili ya maisha yao, jamii na Taifa kwa ujumla kabla na baada ya masomo.

“Tukifanikiwa kuhusu somo linalohusu dawa za kulevya kuwa la lazima katika shule za msingi hadi vyuo vikuu, tutakuwa tumeokoa vijana wengi ambao wanapotea kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya hapa nchini kwa sasa,”anasema Bi.Hadija.

Ombi

Pia ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kuona namna ambavyo inawatumia vijana kama Twaha ili kuwa mabalozi wema wa kutoa elimu kwa jamii na vijana kuhusu athari za dawa za kulevya nchini.

WANASEMAJE?

Kwa nyakati tofauti baadhi ya waathirika wa dawa za kulevya ambao wapo chini ya uangalizi wa nyumba ya upataji nafuu (sober house) ya Free at Last iliyopo mjini Morogoro wamesema, unyanyapaa ni moja wapo ya sababu kubwa inayowafanya waumie nafsi zao.
Mmoja wa waraibu, Abel Leonard ambaye anaendelea na uangalizi kutoka mkoani Mbeya anasema kuwa, hawafurahi kuwa katika hali hiyo, kwani hata yeye alijikuta ameangukia katika janga hilo baada ya kupoteza wazazi wote na kukosa marafiki wema wa kumuongoza.

Amesema, anajutia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kwani yamemvurugia mfumo wa maisha yake na anaamini akipona ataenda kuwa balozi mwema huko mtaani, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo hayana faida badala yake amepoteza muda na kila kitu.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliokuwa katika kikao kazi cha siku tatu kuanzia Novemba 10 hadi 12, 2021 cha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) mjini Morogoro.

Ziara hiyo ya Novemba 11, 2021 ilikuwa sehemu ya mafunzo ambapo msimamizi wa nyumba ya Free At Last, Michael Cassian amesema, jamii ikifanikiwa kuushinda unyanyasaji na unyanyapaa kwa waathirika wa dawa za kulevya huo utakuwa ni uponyaji tosha kwao.

Pia amesema, ukosefu wa elimu sahihi kwa jamii kuhusu watu waliothiriwa na dawa za kulevya umesababisha kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji kwa waathiriwa hao ikiwemo kuigizwa na kuitwa majina yasiyofaa kama vile mateja na mengine mengi jambo ambalo halipaswi kuungwa mkono.

"Huko mitaani jamii inatuita majina ya kila aina na wengine hata wanatuigiza jambo ambalo siyo sahihi kwani linazidi kutukandamiza sisi waathiriwa,mimi nadhani hii inatokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu tatizo la uraibu wa dawa za kulevya,"amesema.

Mraibu anapelekwa jela?

Kamishna wa Tiba na Kinga wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Dkt.Peter Mfisi amesema, sheria inatambua kuwa uraibu ni ugonjwa, hivyo hukumu pekee ni kumpeleka mraibu hospitali na siyo jela kama jamii inavyofikiria.
Dkt.Mfisi anasema kuwa,Jeshi la Polisi limekuwa likitumia weledi mkubwa wanapowakamata waraibu wa dawa za kulevya ambapo hushirikiana na familia zao kuwasainisha matibabu ya lazima ya kuondokana na uraibu kwa muda wa miezi sita.

"Jambo la kushangaza,wengi wao wamekuwa hawafuati adhabu hiyo na kurudi kwenye matumizi ya dawa hizo haramu,"amesema.

Tuleteeni taarifa

"Mamlaka tunafanya kazi kutokana na jamii. Kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya niwahakikishie kuwa, mtu au watu ambao wataleta taarifa zao katika mamlaka zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, tutazipokea kwa uaminifu wa hali ya juu na tutamtunzia siri, hivyo msiwe na hofu yoyote kama mna taarifa, tuleteeni taarifa,"Anasema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Bi.Florence Khambi.
Kwa sheria ya Tanzania, mtu ukifanya kilimo cha dawa za kulevya mfano ukilima bangi na mirungi (dawa za mashambani) au ukikutwa na mbegu zake, ukikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 na kosa hili halina dhamana.

Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 ambayo ilianza kutumika kuanzia Mwezi Septemba 2015 na kurejewa mwaka 2019.

Wakati huo huo, Khambi amesema kuwa, dira yao kama mamlaka ni kujenga jamii ya Tanzania isiyotumia dawa za kulevya au kushiriki katika biashara ya dawa hizo na hivyo kuchangia lengo kuu la kuwa na maisha bora nchini kama ilivyochagizwa kwenye Malengo ya Maendeleo ya 2025.

"Na dhima yetu ni kujenga mfumo bora wa kudhibiti na kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kuendeleza ushirikiano katika hatua mbalimbali za udhibiti wa dawa za kulevya na kujenga uwezo wa taasisi na asasi zisizo za kiserikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya,"amefafanua.

DCEA yakoleza moto

Ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama bila dawa za kulevya,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, imedhibiti uingizwaji wa tani 120.5 za kemikali bashirifu aina ya yabisi, pamoja na lita 40 za kemikali hiyo aina ya kimiminika ambazo zilikuwa zikiingizwa nchini.

Mamlaka hiyo katika kipindi hicho pia, iliweza kukamata wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya 11,716 ambao walidaiwa kukutwa na kilo 35, 227. 25 za dawa za aina mbalimbali.

Akitoa taarifa ya mwaka mmoja ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya, amesema pia wameteketeza ekari 185 za mashamba ya bangi katika maeneo mbalimbali nchini, na mashamba ya mirungi ekari 10 ambapo katika zoezi hilo, wapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea kusikilizwa.

"Katika kipindi hicho jumla ya watuhumiwa 100 walikutwa na dawa aina ya Cocaine, lakini pia katika kipindi hicho watuhumiwa 588 walikamatwa wakiwa wanajihusisha na biashara na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya Heroine, watuhumiwa 9,484 walikamatwa wakijihusisha na dawa za kulevya aina ya bangi, watuhumiwa 1,395 walikutwa wafitumia na kufanya biashara ya mirungi, katika kipindi hicho mashamba 132 ya watuhumiwa 132 wa mashamba ya bangi walikamatwa,"amesema.
Kusaya amesema, kufuatia Tanzania kufanya vizuri kwenye udhibiti wa kemikali hizo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu-UNODC imeiteua Tanzania kuwa nchi kinara katika udhibiti wa kemikali bashirifu, na kuipa jukumu la kutoa elimu kuhusu udhibiti wake katika nchi tisa barani Afrika.

"Watanzania wenzangu, kutokana na taasisi yenu kufanya vizuri sana kwenye udhibiti wa dawa bashirifu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu-UNODC imeiteua Tanzania kutoa elimu kuhusu udhibiti huo kwa nchi za Rwanda, Burundi, Madagascar, Zambia, Malawi, Ethiopia, Msumbiji, Eritrea na Mauritius," amesema Kusaya.

Aidha, amebainisha kuwa DCEA kwa kushirikiana na taasisi na za Serikali za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bohari ya Dawa (MSD) na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya wanasaidiana katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali bashirifu.

Lengo ni kuondokana na dawa za kulevya ambapo wameanzisha mradi wa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi 27 za kemikali hiyo, na vyama viwili vya dawa za binadamu, ambapo wametia saini mkataba wa makubaliano ya udhibiti huo.

Post a Comment

0 Comments