Rais Dkt.Mwinyi apiga kura ya kumchagua Balozi wa Shina, atoa wito kwa wanaCCM

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wana CCM kuhakikisha wanawachagua viongozi makini katika chaguzi za mashina zilizoanza rasmi, kwani hao ndio viongozi wapambanaji katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.
Rais Dkt. Mwinyi ambaye pia ni a Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ameyasema hayo Aprili 22,2022 mara baada ya kushiriki kikamilifu katika upigaji wa Kura za Mabalozi na Wajumbe katika Shina namba Moja la Migombani Mjini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dkt. Mwinyi, alieleza kwamba ni vyema wakachaguliwa watu makini ambao wanaweza kusaidia kufanya kazi ndani ya chama hicho na wasidharau chaguzi hizo kwani katika hatua hiyo viongozi wa shina ndio wapambanaji na ndio wenye watu.
Alisema kuwa, uchaguzi rasmi umeanza katika chama hicho cha CCM ambayo ni hatua awali katika ngazi za Mashina zoezi ambalo litaendelea katika ngazi zote kuanzia Shina, Wadi, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Rais Dkt. Mwinyi alitoa shukurani kwa kupewa fursa hiyo ya kushiriki kikamilifu katika kumchagua Balozi wa Shina hilo namba moja la Migombani ambapo alitumia nafasi hiyo kukiombea Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kiweze kufanikiwa katika chaguzi zake zote zinazoendelea.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi aliwashukuru wanaCCM wa Shina hilo namba moja la Migombani kwa kumpokea vizuri akiwa mwanachama mpya wa Shina hilo kwani tokea baada ya uchaguzi wa Dola uliopita amekuwa mkaazi rasmi wa Shehia ya Migombani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Tawi la CCM Kilimani shina namba moja Shehia ya Kilimani Jimbo la Mpendae Zanzibar. (Picha na Ikulu)

“Hili ndio Shina langu na leo nimefurahi kushiriki uchaguzi katika Shina hili...tutambue kwamba tunaowachagua mwaka huu ndio watakaokuwa wapambanaji wetu katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025,”alisisitiza Rais Dkt. Mwinyi.

Nao wanachama wa CCM wa shina hilo walitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kushiriki katika uchaguzi huo ambapo waliahidi kufanya uchaguzi wa haki na wenye amani na usalama kwa azma ya kukiendeleza na kukiimarisha chama chao ili kiendelee kushika Dola.

Katika uchaguzi huo wanowania nafasi za Mwenyekiti wa Shina ni Tatu Simai Faki na Canada Moris Marekani pamoja na Wajumbe watano kwa nafasi nne za Ujumbe wa Shina hilo zilizopo.
Uchaguzi wa Mashina ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeanza rasmi kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho na baada ya kumaliza chaguzi hizo uchaguzi unaofuata ni wa Matawi na hatimae kuendelea katika ngazi nyengine hadi ngazi ya Taifa.

Post a Comment

1 Comments

  1. hivi na kiongozi mkubwa kama huyu unaweza kupata nafasi ya kwenda kumumba kura kama tunavyopitaga kwa wanachama wa kawaida?

    ReplyDelete