Rais Dkt.Mwinyi:Muungano wetu unazidi kuimarika zaidi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa unatimiza miaka 58 bado unaendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasma hayo wakati akitoa salamu zake za kusherehekea miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kupitia vyombo vya habari Ikulu jijini Zanzibar.

Katika salamu zake hizo Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado wananchi wake wako pamoja hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa ndani ya miaka 58 ya Muungano huo.

Amesema kwamba, Tanzania bila ya Muungano sio kitu ambacho kinaweza kufikiriwa kwani Watanzania walio wengi wamezaliwa ndani ya kipindi cha Muungano hivyo, alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuuezi na kuudumisha kwa faida ya kizazi kiliopo na kijacho.

Aliongeza kuwa, Muungano uliopo hivi sasa ni wa damu zaidi kuliko Muungano wa vitu kwani wananchi walio wengi wana uhusiano wa Zanzibar na Tanzania Bara hivyo, wote ni wamoja.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kwamba licha ya wananchi wake kuchanganya damu pia, kuna mafanikio makubwa yaliopatikana kupitia Muungano hususan biashara kwani bidhaa nyingi zinazotumika Zanzibar zinatoka Tanzania Bara.

Alisema kuwa mbali ya muunganiko wa watu na biashara pia, kumekuwa na mafanikio makubwa katika suala zima la ulinzi na usalama ambapo katika kipindi chote cha miaka 58 ya Muungano kumekuwa na amani na usalama.

Amesema kuwa, mafanikio hayo yameweza kupatikana kutokana na wananchi wenyewe kuwa ni watu wa amani pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo vinahudumia sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba suala la Muungano nalo lina nafasi kubwa katika Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio dira ya uchumi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba eneo lote la bahari ni la Muungano ambayo pia, ni kiunganisho kati ya Zanzibar na Bara.

“Zanzibar kama kisiwa haiwezi kuleta maendeleo ikiwa peke yake tunawahitaji wenzetu na kwa kiwango kikubwa tunawahitaji wenzetu wa Bara kwa mambo yote yanayohusu uchumi wa buluu kwa mfano matumizi ya rasilimali za bahari kwenye uvuvi bahari yetu ni moja kwani eneo la uvuvi wa bahari ni la Muungano hivyo, bila shaka uchumi wa Buluu utafanikiwa Muungano ukiendelea kuwepo,”alisema Rais Dkt. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa kunahitajika mashirikiano ya pamoja hasa katika matumizi ya rasilimali za bahari katika uvuvi kwani inaonesha wazi kwamba eneo lote la uvuvi wa bahari ni la Muungano hivyo, uchumi wa buluu utafanikiwa iwapo Muungano utaendelea kuwepo.

Alieleza kwamba bandari kubwa inayotarajiwa kuanzishwa Zanzibar kwa kiasi kikubwa itategemea biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara hivyo, ni muhimu sana kuendeleza Muungano uliopo kwa manufaa ya pande mbili hizo.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa ni muhimu kuendeleza Muungano kwa manufaa ya pande mbili za Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania na kusisitiza kwamba Zanzibar itafanya vizuri zaidi kiuchumi iwapo itaendelea kuwa katika Muungano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news