Rais Samia awataka vijana kuchangamkia fursa za TEHAMA

NA BENNY MWAIPAJA,New York

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka watanzania hususan Vijana, kuchangamkia fursa za maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Rais ametoa wito huo Mjini NewYork nchini Marekani, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati alipozindua Mtandao wa NALA (NALA APP) utakaotumiwa na watanzania waishio Marekani kutuma fedha nchini Tanzania kidijitali.

Alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NALA, Raia wa Tanzania, Bw. Benjamin Fernandes na Timu yake, kwa kubuni Application hiyo ambayo itarahisisha utumaji wa fedha kutoka nchini humo kwenda Tanzania hatua ambayo itasissimua uchumi wa nchi na kuharakisha maendeleo ya wananchi watakaofaidika na huduma hiyo.

“Benjamin Fernandes na Timu yako ni miongoni mwa vijana wabunifu waliojikita katika masuala ya teknolojia ambao Serikali inawaunga mkono hususan wakati huu ambapo nchi inajenga uchumi wa kidijitali ambao matokeo yake yanatarajwa kuwa ni kukuza ajira, kuchangia pato la Taifa na kukabiliana na changamoto zote za kiuchumi na kijamii,”alisema Dkt. Nchemba.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kulia) akishikilia Nembo ya NALA APP alipozindua rasmi huduma za kutuma fedha kidigitali kutoka Marekani kwenda Tanzania kwa kutumia Mtandao huo, kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, Jijini NewYork nchini Marekani. Kushoto ni Balozi wa Tanzania Nchini Marekani na Mexico Dr. Elsie Kanza, kushoto ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale – Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NALA Bw. Benjamin Fernandes.

Alisema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kujenga mkongo wa Taifa uliounganishwa na nchi nyingine za kiafrika zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya, Malawi, Uganda na Zambia na hivi karibuni nchi za DRC na Msumbiji zitaunganishwa.

Dkt. Nchemba alitoa wito kwa wawekezaji kwenye sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuwekeza nchini Tanzania na kufaidi mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo nchi imeweka ili kuvutia mitaji na teknolojia.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (kushoto) akiingia kwenye ukumbi kwa ajili ya kuzindua Mtandao wa NALA unaotumika kwa ajili ya kutoa huduma ya kutuma fedha kidigitali kutoka Marekani kwenda Tanzania kwa kutumia Mtandao huo, kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, Jijini NewYork nchini Marekani. Katikati ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Donald Wright na kulia ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale-Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-NeyYork).

Alifafanua kuwa hivi sasa mtu anayetaka kutoa huduma ya kibunifu analazimika kulipia leseni Benki Kuu ya Tanzania hata bila kuanza kufanyakazi hatua ambayo alisema inawakwaza vijana wengi kutimiza ndoto zao za kujiajiri na kuwaajiri watu wengine.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (kulia) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kidigitali ya NALA, baada ya kuzindua NALA APP inayotumika kutuma fedha kidigitali kutoka nchini Marekani na nchi nyingine duniani, kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, Jijini NewYork nchini Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)(katikati), akishikilia Nembo ya NALA APP alipozindua rasmi huduma za kutuma fedha kidigitali kutoka Marekani kwenda Tanzania kwa kutumia Mtandao huo, kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, Jijini NewYork nchini Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (kulia) akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kidigitali ya miamala ya Simu (NALA APP), baada ya kuzindua APP hiyo inayotumika kutuma fedha kidigitali kutoka nchini Marekani na nchi nyingine duniani, kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, Jijini NewYork nchini Marekani.

Aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizoainishwa na uongozi wa Kampuni hiyo katika masuala ya upatikanaji wa leseni za kuendesha shughuli za TEHAMA ili kuwatia moyo vijana wabunifu wawekeze kwenye teknolojia zinazoweza kuchangia ukuaji wa matumizi ya teknolojia katika kuongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nimefahamishwa kwamba Marekani imewekeza karibu dola bilioni 1.5 katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Barani Afrika, ninatamani kuona kuwa Tanzania inakuwa ni moja ya nchi zitakazonufaika na uwekezaji huo” Alisisitiza Dkt. Nchemba katika Hotuba yake akimwakilisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw.Benjamin Fernandes alisema kuwa Application iliyozinduliwa nchini Marekani, inafanyakazi katika nchini nyingine 9 duniani na aliibuni kwa ajili ya kusaidia utumaji wa fedha kwa nchi za Afrika.

Aidha, Bw. Fernandes aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza masharti ya leseni ya biashara ya mitandao ili kuwawezesha vijana wengi wabunifu wa TEHAMA, kuwekeza nguvu zao kwa kuwa itaongeza ajira na kukuza uchumi wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news