RC KUNENGE AWAAGIZA WANANCHI KULIPA FIDIA ENEO LA SANZALE BAGAMOYO KAMA ILIVYOAMRIWA NA MAHAKAMA,WAITIKIA NA KUOMBA UTARATIBU

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewaagiza wananchi wa Kitongoji cha Sanzale kilichopo Kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo kuhakikisha wanalipia fidia ya eneo walilojenga kama ilivyoamriwa na Mahakama.
Wananchi hao wamejenga eneo hilo kinyume na utaratibu kwa kuwa wameuziwa viwanja kitapeli na watu tofauti bila msimamizi Salim Mgombeo kushirikishwa.

Mgombeo amekuwa msimamizi wa mirathi wa eneo hilo kutoka familia ya mzee Ramadhani Heri aliyefariki miaka mingi iliyopita ambapo alikwenda mahakamani baada ya eneo lake kuvamiwa na hivyo kushinda kesi.

Kufuatia mgogoro huo ,Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amefika katika eneo hilo mapema leo kwa ajili ya kufanya mkutano na wananchi wa eneo hilo na kutoa maagizo mbalimbali.

Miongoni mwa maagizo ya Kunenge kwa wananchi hao ni kuhakikisha kila mwananchi aliyejenga katika eneo hilo kuwa alipe fidia kama maamuzi yalivyotolewa na Mahakama.
Aidha, Kunenge amemuagiza Mkuu wa wilaya, hiyo Zainabu Abdallah kuhakikisha anaendesha msako wa kuwakamata matapeli wote waliohusika katika eneo hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Kunenge amesema kuwa, nchi hufanya kazi kwa kuzingatia mihimili yake mitatu ikiwemo Bunge,Mahakama na Serikali huku akisema mihimili hiyo haiingiliani maamuzi yake.

Amesema kuwa,jambo ambalo limeamriwa na Mahakama hakuna anayeweza kutengua wala kuingilia isipokuwa hatua nyingine ya Kimahakama (Rufaa) na kwamba kinachotakiwa ni utekelezaji wa Mahakama.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo katika kuwasaidia wananchi na ndio maana amefika eneo hilo kutatua mgogoro huo kwa kuzingatia taratibu na misingi ya kisheria.

"Kuna mambo yanatatuliwa kiutawala na kama mnadhani kuna mtendaji anakiuka utaratibu basi naweza kulishughulikia, lakini jambo la Mahakama lazima liheshimiwe,"amesema Kunenge.

"Naishukuru familia ya marehemu kwa kugoma kubomoa nyumba za wananchi hawa, lakini namuagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia kwa karibu ili wakishakubaliana watu hawa wafanyiwe mpango wa kupewa hati za umiliki,"amesema.

Kunenge amesema, mbali na maagizo hayo lakini pia atafanya kikao na baadhi ya wawakilishi wa wananchi, msimamizi wa mirathi,familia na Mkuu wa Wilaya ili kuona namna ambavyo wananchi hao watalipa kwa utaratibu maalum na wenye kufaa.
Amesema kuwa,baada ya utaratibu huo kukamilika wananchi hao watapata huduma zote muhimu ikiwemo maji na umeme huku akiwasisitiza wananchi kufuata sheria na taratibu pale wanapotaka kununua na hata kujenga nyumba zao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sanzale, Mbaraka Omary amesema kuwa, aliletewa barua ya kusaini lakini aligoma na hatimaye kuchukua maamuzi ya kumuita ofisini mzee Mgombeo.

Omary amesema kuwa, walikubaliana na mzee huyo kulipa fedha hizo kwa wakati lakini ikatokea sintofahamu ya wengine kulipa na wengine kugoma ambapo alimuomba Mkuu wa Mkoa asaidie jambo hilo.

Naye msimamizi wa mirathi hiyo, Salim Mgombeo,amesema kuwa anachotaka yeye ni kuwa wale waligoma kulipa waondoke, lakini waliokubali kulipa wabaki na kwamba mgogoro huo ni mkubwa.

Baadhi ya wananchi hao akiwemo Amina Azizi na Hassan NG'anzi,wamesema wao wapo tayari kulipa na wameomba Serikali iweke utaratibu maalum ambao utawawezesha kulipa bila usumbufu.

Post a Comment

0 Comments