Serikali yatangaza ajira 17,412 leo, Waziri Bashungwa atoa maagizo

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Bw. Innocent Bashungwa amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2021/22 Serikali inatarajia kuajiri watumishi 17,412 ambapo nafasi 9,800 ni za walimu na 7,612 ni za kada za afya.
Ameyasema hayo leo Aprili 20,2022 wakati akitoa maelezo kuhusu hoja za wabunge zilizojitokeza wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya OR-TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2022/2023 bungeni jijini Dodoma.

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 kwa OR-TAMISEMI ni Shilingi Trilioni 8.8 kwa ajili ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Fungu 56, Tume ya Utumishi wa Walimu Fungu Na. 2 na Mafungu 26 ya mikoa yanayojumuisha halmashauri 184.

"Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kwa kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa idhini ya ajira za watumishi wa Sekta ya Elimu na Afya 17,412 ambapo nafasi 9,800 ni za walimu na 7,612 ni za kada za afya ambao wataajiriwa katika mwaka huu wa Fedha 2021/22.

"Naomba kutoa taarifa rasmi kuwa Watanzania wenye sifa wanaelekezwa kuanza kuomba kuanzia leo. Aidha, napenda kuwaelekeza kuwa maombi ya ajira hizi ni bure na yanafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki ambao maelekezo yake yatakuwa katika tangazo la ajira.Asilimia tatu ya ajira hizo ni kuajiri watu wenye ulemavu kulingana na sheria,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Pikipiki 68

Mheshimiwa Bashungwa amelieleza Bunge kuwa, Aprili 14, 2022 aliwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais–TAMISEMI kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo latika eneo la utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi Rais-TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2021/22, sehemu ya Huduma za Ustawi wa Jamii alisoma kwamba, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imefanya ununuzi wa pikipiki 68 aina ya Boxer zenye thamani ya shilingi milioni 789.9 kwa ajili ya Maafisa Ustawi wa Jamii.

"Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa taarifa kwamba, idadi ya pikipiki 68 iliyotajwa kwenye hotuba yangu sio sahihi na hii imetokana na makosa ya kiuandishi. Usahihi ni kwamba pikipiki 68 zimenunuliwa na wadau kwa gharama ya shilingi milioni 227.50 ambao walikuwa wanatekeleza miradi ya “USAID Kizazi Kipya” katika baadhi ya halmashauri katika mikoa 21 ambazo zilinunuliwa na kusambazwa mwezi Septemba, 2021.

"Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya pikipiki kwa Maafisa Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliona inunue pikipiki 200 aina ya Boxer ambazo kwa sasa zipo katika hatua ya mwisho ya manunuzi,"amefafanua Mheshimiwa Bashungwa.

Amesema kuwa, pikipiki hizo zinanunuliwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19 kwa gharama ya shilingi milioni 562.40.

Pia amesema, pikipiki hizo zitasambazwa kwenye maeneo ambayo hayakupata mgao wa pikipiki 68.

"Hivyo, jumla ya pikipiki 268 zitanunuliwa kwa gharama ya shilingi milioni 789.90. Aidha, taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba OR-TAMISEMI imenunua pikipiki moja kwa shilingi milioni 11 sio sahihi. Taarifa sahihi ni kwamba kila pikipiki kati ya pikipiki 68 ilinunuliwa na mdau wa maendeleo kwa shilingi milioni 3.34,"ameweka sawa Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru Manaibu Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi mzuri kwenye kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge, hoja zilizotolewa na waheshimiwa wabunge amesema zimejikita katika maeneo mbalimbali.Miundombinu ya Machinga

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema kuwa,katika kuboresha miundombinu ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo (machinga), Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa tija.

Hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuwapanga Machinga kwenye maeneo rasmi kwa utulivu pasipo kutumia nguvu katika halmashauri zote zilizokuwa na machinga wengi kupitia ofisi za wakuu wa mikoa.

Hatua nyingine iliyochukuliwa ni Serikali kutoa Shilingi bilioni 5.0 kwa ajili ya kuboresha maeneo ya kufanyia biashara machinga katika Halmashauri 11.

"Mheshimiwa Spika, hatua nyingine inayoendelea ni kuwepo kwa majadiliano na Wizara ya Fedha na Mipango ili kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 ili kuruhusu sehemu ya fedha za Mikopo ya asilimia 10 kutumika katika kuboresha miundombinu ya Machinga.

"Marekebisho ya Sheria hii yanapendekezwa kufanyika kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022. Majadiliano hayo yakikamilika, tunatarajia kiasi cha Shilingi bilioni 38.01 zitapatikana kupitia mlango huo kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya wafanyabiashara wadogo (Machinga),"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Amefafanua kuwa, chanzo kingine cha mapato kinachotarajiwa ni kupitia asilimia 10 ya fedha zilizotengwa kwenye miradi ya maendeleo za mapato ya ndani ya halmashauri. Kupitia chanzo hiki, Waziri Bashungwa amesema, kiasi cha shilingi bilioni 36.82 kinakadiriwa kupatikana.

Pia anasema, mapendekezo ya kutumia asilimia 10 ya fedha za miradi ya maendeleo zinalenga kuhusisha halmashauri zenye mapato yanayozidi shilingi bilioni 5 pamoja na halmashauri nyingine ambazo zimejumuishwa kwenye mpango wa kuboresha maeneo ya machinga.

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23 kupitia vyanzo hivyo, Halmashauri zitakusanya jumla ya shilingi bilioni 74.83 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya machinga. Aidha, jumla ya fedha itakayotumika katika kuboresha miundombinu hiyo itakuwa Shilingi bilioni 79.83 ikijumuisha Shilingi bilioni 5 ambazo zimekwishatolewa.

"Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa kundi hili katika kukuza uchumi, hivyo, ninapenda nitumie fursa hii kuwaelekeza viongozi wote wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha vitendo vya kuwanyanyasa machinga na kutumia nguvu katika kuwaondoa na kuwapanga ikiwemo kuharibu bidhaa zao kama ilivyotokea kwa Jiji la Mwanza vinakomeshwa,"ameeleza na kutoa angalizo Waziri Bashungwa.

TARURA

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Bashungwa akizungumzia kuhusu Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) amewashukuru wabunge pamoja na Wajumbe wa Kamati ya USEMI kwa pongezi walizotoa kufuatia utekelezaji wa agizo la TARURA kuanza mapema ununuzi wa mikataba ya utekelezaji wa miradi ya barabara.

Katika mwaka wa fedha 2022/23, amesema ununuzi wa kazi utaanza mwanzoni mwa mwezi Mei, 2022. "Utaratibu huu umetokana na mapendekezo ya Kamati ya USEMI pamoja na waheshimiwa wabunge wa Bunge lako tukufu. ninaagiza mameneja wa TARURA wa mikoa na wilaya wawashirikishe wadau ikiwa ni pamoja na waheshimiwa wabunge wakati wa kuainisha vipaumbele.

"Mheshimiwa Spika, ili kuboresha ugawaji wa rasilimali fedha TARURA inafanya mapitio ya fomula itakayotumika katika kugawa rasilimali fedha za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara kulingana na hali ya maeneo husika,"amefafanua Mheshimiwa Bashungwa.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa,Ofisi ya Rais-TAMISEMI watapima utendaji kazi wa Mameneja wa TARURA ngazi ya Mikoa na Wilaya kupitia Ufuatiliaji na Tathmini (Uratibu katika ngazi ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri).

Ufuatiliaji


Pia amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika ngazi ya Makao Makuu, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Katika kuimarisha usimamizi kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Rais amemteua Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Sekta za Uchumi na Uzalishaji kama ilivyo kwa Sekta za Elimu na Afya.

"Kuimarisha mifumo ya TEHAMA ambayo inasaidia kazi ya ufuatiliaji wa fedha zinazokusanywa na kupelekwa katika Halmashauri, kufuatilia matumizi ya fedha pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imeongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kutoka Shilingi bilioni 57.44 hadi Shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hizo, ikiwemo ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Aidha, muundo wa Sekretarieti za Mikoa umehuishwa kwa kuboresha iliyokuwa Seksheni ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa Seksheni ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ambayo ina jukumu la ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.


Amefafanua kuwa, katika ngazi ya halmashauri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imepanga kuendelea kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani na Watendaji katika ngazi ya Halmashauri na Kata ili waweze kupata uelewa wa kusimamia ukusanyaji wa mapato na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

"Mheshimiwa Spika, aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeimarisha mfumo wa kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu (KPI) vikiwemo ukusanyaji wa mapato ya ndani, upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, matumizi sahihi, usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi.

"Mheshimiwa Spika, matokeo ya upimaji yatatoa tafsiri ya utendaji wa viongozi wengine katika ngazi ya mkoa na wilaya ambao wana jukumu la kuhakikisha kuwa mamlaka za Serikali za Mitaa zinatimiza majukumu yao.

"Hivyo, nitoe rai kwa Viongozi wote katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutimiza wajibu wao kwa kuwa utendaji wao utapimwa kwa kutumia viashiria hivyo. Miradi ya Afya na Elimu nje ya ile ya UVIKO-19 ikamilike ifikapo tarehe 30 Mei, 2022. Hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Mikoa simamieni hii deadline,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.


Wakati huo huo, Ofisi ya Rais – TAMISEMi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imeanza kuboresha mfumo huo ili uweze kutumika kwa urahisi kwa vituo vyote 5,934 vya Serikali hususan vilivyopo vijijini, uweze kuunganika na kusomana na mifumo ya kitaifa ili kupata taarifa na takwimu ngazi ya Taifa na kuhakikisha usalama wake.

Amesema, lengo la Ofisi ya Rais -TAMISEMI ni kuweka mfumo huo kwenye vituo vyote ifikapo mwaka wa fedha 2024/25. Kazi hii itafanywa kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo na kusimamiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

Nidhamu

Waziri Bashungwa amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI katika kusimamia masuala ya nidhamu na maadili ya kazi katika ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, imekuwa ikichukua hatua za kinidhamu kwa Watumishi wanaokiuka Sheria na taratibu za kazi ikiwa ni pamoja na ubadhirifu, uzembe, ukiukwaji wa maadili ya kazi na taaluma zao.

"Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha 2021/22 OR-TAMISEMI imewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanne, imewashusha vyeo Waganga Wakuu wa Mikoa wawili (2), Waganga Wakuu wa Halmashauri 14, Afisa Elimu Mkoa mmoja, Maafisa Elimu ngazi ya Wilaya tisa (9), na Wakuu wa Vitengo vya Manunuzi ngazi ya Halmashauri 24.

"Natoa wito kwa watumishi wote wa umma kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma. Aidha, nazielekeza Mamlaka za nidhamu kuhakikisha zinachukua hatua stahiki kwa wale ambao wamebainika kukiuka taratibu. Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kukiuka taratibu na maadili ya kazi na taaluma zao,"ameagiza Waziri Bashungwa.

Ujenzi wa Vituo vya Afya

Amesema, Ofisi ya Rais -TAMISEMI inatambua umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika uendelezaji wa miundombinu sambamba na kuiwezesha kutoa huduma za afya kwa kuwa na Vifaa Tiba na watumishi.

Katika kutekeleza hilo, Mheshimiwa Bashungwa amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeweza kufanya tathmini ya uhitaji wa vituo vya afya 428 ambavyo vitajengwa kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia Mwaka wa Fedha 2023/24 ambavyo vitajengwa katika tarafa zisizokuwa na vituo vya afya na kata za kimkakati.

Pia amesema, katika mwaka wa Fedha 2022/23 Serikali itatafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali, bajeti ya Serikali na Halmashauri kutumia Mapato ya Ndani.

Ukarabati

Waziri Bashungwa amesema kuwa, kwa mwaka 2015/16 mpaka 2021/22 OR-TAMISEMI imeweza kufanya ukarabati wa Shule Kongwe za Sekandari 89 kati ya shule 92.

Kwa mwaka wa fedha 2022/23, OR-TAMISEMI imepanga kufanya ukarabati wa Shule za Msingi Kongwe.

Jumla ya shule za msingi zilizoanza kabla ya mwaka 1961 ni shule 2147. Shule hizi anasema, zitakarabatiwa kwa awamu baada ya kukamilisha tathmini ya gharama za ukarabati.

"Ukarabati huu ni endelevu. Katika mwaka wa fedha 2022/23 jumla ya vyumba vya madarasa 1700 vya shule za msingi kongwe ambavyo vimetengewa jumla ya Shilingi bilioni 34 vitakarabatiwa.

"Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Afya ya Msingi kwa mwaka 2022/23 OR-TAMISEMI imepanga kufanya ukarabati wa Hospitali za Halmashauri Kongwe 19 kati ya Hospitali 77 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 16.55 zimetengwa.

"Aidha, ofisi ya Rais TAMISEMI itafanya zoezi la kutambua Vituo vya Afya na Zahanati zilizojengwa kati ya mwaka 1961 hadi1970 ili kuweka mkakati wa kuvikarabati,"amesema.


Ukamilishaji wa Miradi

Mheshimiwa Bashungwa amesema, Ofisi ya Rais -TAMISEMI inakubaliana na hoja za waheshimiwa wabunge za kuwepo kwa miradi iliyoanzishwa miaka ya nyuma na bado haijakamilika.

"Ninapenda kuwaelekeza wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya kina kuhusu miradi na gharama zake za ukamilishaji ili Ofisi ya Rais TAMISEMI iweze kuitambua miradi hiyo na kuweka mikakati ya ukamilishaji. Taarifa hiyo iwasilishwe kabla ya tarehe 30 Juni, 2022,"amesema.

Vifaa na Vifaa Tiba

"Mheshimiwa Spika, nakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu ukosefu wa Vifaa na Vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyokamilika kujengwa.

"Kuanzia Mwaka wa Fedha 2018/19 hadi mwaka 2021/22 Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 82.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba katika ngazi ya afya msingi, ambapo Shilingi bilioni 15 zimetumika kununua vifaa na vifaa tiba na kuvisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.


Aidha, vifaa vingine manunuzi yake yanaendelea. Vifaa hivi vinajumuisha Vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya utoaji wa huduma za upasuaji na huduma za Mionzi. Aidha, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2022/23 imetenga Shilingi bilioni 47.70 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye Vituo vya Afya 159.

Amesema, Ofisi ya Rais TAMISEMI inafuatilia Vifaa na Vifaa tiba ambavyo tayari vimeshalipiwa fedha kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuondoa changamoto ya Vituo vya Afya vilivyokamilika na kukosa huduma hiyo.


Mapato

Amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kuzisimamia halmashauri ili ziongeze wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuwajengea uwezo maafisa wanaokusanya mapato, kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na utambuzi wa fursa na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato.

Aidha, amesema utendaji wa halmashauri utapimwa kwa kuzingatia upelekaji wa asilimia 40/60 na 70 kwa halmashauri chache zenye makusanyo makubwa zinazotokana na makusanyo ya mapato ya ndani yasiyolindwa katika miradi ya maendeleo, utoaji wa mikopo ya asilimia 10.

Ni kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, na urejeshaji wa mikopo na ujibuji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ili kuleta tija na kuimarisha utoaji wa huduma.

"Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 halmashauri ziliidhinishwa kukusanya Shilingi bilioni 863.85 kutoka katika vyanzo vya Mapato ya Ndani. Hadi Februari, 2022 zimekusanywa Shilingi biliioni 586.07 sawa na asilimia 68.

"Fedha zilizoiidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Shilingi bilioni 331.08, hadi Februari 2022 Shilingi bilioni 216.11 sawa na asilimia 65.27. Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapelekwa kwa wakati katika miradi husika,"amefafanua Waziri Bashungwa.

Usimamizi wa POS

Amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI katika mwaka wa Fedha 2022/23 imepanga kuongeza mapato ya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kufika Shilingi Trilioni 1.01 sawa na ongezeko la asilimia 17.18.

Mafanikio haya yatafikiwa kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake, kufanya ufuatiliaji mara kwa mara, fedha zote zinazokusanywa kuingizwa benki kabla ya matumizi, vyanzo vyote kuwa na PoS katika kukusanya mapato, kufanya tathmini ya wadaiwa na kuweka mikakati ya kukusanya madeni hayo, na matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki ikiwemo LGRCIS/TAUSI na GoTHOMIS katika vituo vya kutoa huduma za afya.

"Mheshimiwa Spika, matumizi sahihi ya Mashine za kukusanya mapato (PoS) ni muhimu, hivyo ninaelekeza kila Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya yafuatayo,

"Kuhakikisha PoS zote hasa zile za zamani kabla ya Mwaka 2019, zinawekewa toleo jipya la APK Toleo la 4.9.9.6.49 ili kuondoa mianya ya kupoteza mapato.

"Kufanyika kwa ukaguzi wa PoS kila mwezi ili kubaini PoS zipo ngapi, zipo wapi, ngapi zipo online na ni nani wanazotumia. Kuhakikisha POS zote ambazo haziko hewani (offline) kutokana na ubovu au kutojulikana zilipo zinafifishwa kwenye Mfumo (deactivate).

"Kufanya “Job rotation”, kuzungusha wanaosimamia ecosystem nzima ya ukusanyaji wa Mapato (ICTO, Wahasibu na wengine).

"Kuhakikisha mapungufu ya POS kwenye maeneo ya ukusanyaji yanabainika na mkakati wa kununua POS unawekwa kukidhi mapungufu hayo ili kuongeza mapato. Kuhakikisha rejista zote za POS zinahuishwa kuendana na taarifa za mfumo kwa usahihi. Na kutoa hamasa ya kudai risiti kwa kila huduma kutoka kwa mkusanya mapato,"amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI inahuisha Mfumo wa ukusanyaji wa mapato (LGRCIS/TAUSI) ambao utafanya yafuatayo:-

i.Usimamizi wa PoS (POS management)

ii.Usimamizi wa Float ili kuondoa matumizi ya fedha mbichi na kuondoa madeni (Float Management)

iii.Kuhamasisha malipo ya kodi, tozo na ushuri kwa kielektroniki bila kufika ofisi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Online payment – cashless),

iv.Kujifanyia tathmini ya kiasi mlipaji anachopaswa kulipa (Online assessment)

v.Kutoa leseni na vibali vya kielektroniki (Digital Licence and Permit)

vi.Kuunganisha Mfumo na Mifumo ya TRA kupata mapato ghafi ya wafanyabiasha kwa ajili ya kupata kodi halisi ya huduma (service levy)

"Mheshimiwa Spika, Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mamlaka ya Serikali Mtandao inaendelea kuboresha mfumo wa GoTHOMIS ili uweze kutumika na vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya ngazi ya msingi haswa maeneo ya vijijini.

"Maboresho yatazingatia maelekezo yaliyotolewa na Mhe Rais kuhusu kuimarisha mifumo ili izungumze. Mfumo huu unasaidia kusimamia na kudhibiti madawa na vifaa tiba, kutoa taarifa ya magonjwa na ugonjwa na kusimamia mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma.

"Mfumo kwa sasa upo kwenye vituo 1,161 na utawekwa kwenye vituo vyote vya afya ifikapo Mwaka wa Fedha 2015/16,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Posho za Madiwani


Amesema,Waziri mwenye Dhamana na Serikali za Mitaa alishatoa Waraka wenye Kumb. Na. 215/443/01/50 wa tarehe 23/12/2014 juu ya posho za mwezi za madiwani.

Aidha, posho za vikao za Waheshimiwa Madiwani zimeelekezwa katika waraka Kumb. Namba CHB/443/01 wa tarehe 26/11/2007 na kusisitizwa katika waraka Kumb. Na PM/P/1/567/59 wa terehe 16/08/2012 ambapo ni shilingi 40,000.

"Hivyo, posho za Waheshimiwa Madiwani si hisani ya Mkurugenzi wa Halmashauri. Kwa sasa Serikali inaandaa Mwogozo juu ya utaratibu wa ulipaji wa Posho za Vikao kwa Madiwani ambao utapaswa kutumika kwa halmashauri zote,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Ukaguzi


Akizungumzia kuhusu Kamati ya Fedha peke yake kukagua miradi katika halmashauri, Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa, Kanuni ya 77(5-6) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri inaeleza kuwa,

“Kamati za Kudumu za Halmashauri, zinaweza kutembelea miradi ya maendeleo au shughuli yoyote inayotekelezwa na au kwa niaba ya Halmashauri na ambayo inaihusu Kamati husika ’’Kanuni ya 77(1-4) ya kanuni za kudumu za Halmashauri inaelekeza Madiwani kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika meneo yao,"amesema.

Hata hivyo,amesema katika halmashauri nyingi Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ndio imebeba jukumu hilo peke yake kitu ambacho ni kinyume na Kanuni za Kudumu za Halmashauri.

Mikopo ya Asilimia 10

Amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI inatambua changamoto ambazo zimejitokeza katika usimamizi wa Mikopo ya asilimia 10.

"Tayari tumefanya tathmini hadi Machi, 2022 na maoni na ushauri wa Kamati ya USEMI na michango ya wabunge itasaidia usimamizi thabiti ikiwemo utumiaji mfumo wa kielektroniki,"amesema.

Miji Midogo

"Mheshimiwa Spika, kuhusu namna bora ya kushughulikia Mamlaka ya Miji Midogo ili kubaini ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaunda timu kwa ajili ya kufanya tathmini kuhusu uendeshaji na ufanisi wa Mamlaka ya Miji Midogo,"amesema Waziri Bashungwa.

Kuhusu Mshitiri

"Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nimshukuru Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwa jinsi anavyofuatilia suala la uapatikanaji wa dawa na kupelekea kupatikana kwa taarifa hii muhimu.

"Kwa kuwa usimamizi wa dawa na vitendanishi ni kipaumbele cha OR-TAMISEMI, taarifa hii tumeichukua kwa umuhimu mkubwa na nikuhakikishie kwamba tutaifuatilia kwa umakini mkubwa,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Aidha, amesema OR-TAMISEMi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuendelea kuimarisha mfumo wa Prime Vendor System (Mshitiri) ili kuhakikisha inakomesha upotevu na wizi wa dawa na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma ngazi ya msingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news