'Nyongeza ya mishahara si neema kwa watumishi tu, hata sisi wajasiriamali na bodaboda, asante Mheshimiwa Rais Samia'

 NA DIRAMAKINI

SIKU moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuridhia nyongeza ya mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, wafanyabiashara na waendesha bodaboda jijini Dar es Salaam wamepongeza hatua hiyo.
Wamesema, uamuzi wa Rais Samia utaongeza morali kwa wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na kuimarisha mzunguko mkubwa wa fedha kwa wananchi.

Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti leo Mei 15,2022 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI ambapo wamesema, hatua ya Rais Samia kuridhia nyongeza ya mishahara kwa asilimia 23.3 kwa watumishi wa umma inaonesha ni kiongozi mahiri anayethamini 

Sambamba na kuheshimu juhudi zao thabiti wanazozifanya katika kuchochea maendeleo, hatua ambayo pia itaimarisha mzunguko wa shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na wananchi wa makundi mbalimbali.
Boniventure Charles ni mkazi wa Tabata amesema kuwa, hatua hiyo imeleta motisha kwa wafanyakazi na kwamba itaondoa uduni wa maisha kwa wafanyakazi wa Serikali, kwani ongezeko hilo litasaidia wafanyakazi wa serikali kuweza kukidhi mahitaji yao ya kila siku ikiwemo chakula, usafiri na mahitaji mengine ya msingi na kuimarisha mzunguko wa fedha kwa wananchi wanaofanya biashara zao.
"Hatua ya Rais ni ya kupongezwa sana, jambo alililofanya ni zuri mno, sisi tunategemea wafanyakazi wa Serikali, Serikali inapotoa mishahara kwa wafanyakazi mzunguko wa fedha unaongezeka na biashara zinachangamka,"amesema Charles.

Naye Abukabar Seif Shaban ambaye ni mwendesha bodaboda katika Kituo cha Ubungo Mawasiliano amesema kuwa, Rais amefanya jambo ambalo linapaswa kupongezwa kwani wafanyakazi wana mchango mkubwa katika kuwezesha mzunguko wa fedha na hivyo kitendo cha Rais Samia kuwaongezea mishahara kunawezesha neema kwa wananchi.
"Mfanyakazi anaposhika fedha anakuwa na shughuli zake mbalimbali anazofanya,kwa sababu hiyo anaweza kuhitaji bodaboda kutokana na ongezeko alilonalo. Lakini mshahara ukiwa mdogo angeona gharama zimezidi kuwa kubwa na asingechukua bodaboda angeweza kupanda daladala au angetembea kwa miguu, hatua ya Rais ni nzuri sana,"amesema Shaban.

Post a Comment

0 Comments