Prof.Hoseah:Lengo langu kubwa, tunataka iwe taasisi ambayo inajiendesha yenyewe nimechoka utaratibu wa kuiendesha taasisi kwa kuwakamua wanachama

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ambaye anatetea kiti chake, Profesa Edward Hoseah ni kati ya viongozi ambao wamefanikiwa kushirikiana na wenzake kuiendesha taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa ndani ya mwaka mmoja.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuishawishi Mahakama Kuu ya Tanzania kurejeshewa tozo ya shilingi milioni 450 ambazo tangu Uhuru walikuwa wakilipa mahakama kama ada.

Pia kupitia uongozi wake amefanikiwa kupunguza ada ya uwakili kutoka shilingi 60,000 hadi shilingi 20,000, kupunguza gharama ya afya kutoka shilingi milioni 1,050,000 hadi shilingi 500,000, kuimarisha uhusiano baina ya taasisi hiyo na Serikali ambao umeonesha nuru kubwa na mengineyo mengi.

Licha ya uzoefu mkubwa katika uongozi na ubobezi wa kutosha katika sheria, Profesa Hoseah ni miongoni mwa Watanzania wanaoipenda TLS, anaamini kupitia uongozi wake kwa kushirikiana na wenzake wanaweza kuistawisha zaidi taasisi hiyo muhimu.
"Ninaposema Constructive engagement, simaanishi Mawakili wangu wasiende Mahakamani, lakini hii taasisi sera yangu kubwa ni kujenga mahusiano.

"Niliteuliwa kwenye kikosi kazi, kama Mwakilishi wa TLS, na baada ya kuteuliwa niliambia Kamati ya Katiba na Sheria wapeleke maoni yao, wakisema nimeingia kwenye Kikosi Kazi ni kinyume na TLS si sawa, mimi naendesha TLS kama taasisi,"amesema Prof.Hoseah.
"Kama TLS lengo langu kubwa, tunataka iwe taasisi ambayo inajiendesha yenyewe nimechoka utaratibu wa kuiendesha taasisi kwa kuwakamua wanachama wangu.

"Mimi ni mstaafu nina muda wa kutumika na wanachama wangu, ndiyo maana nagombea mwaka wa pili kwa sababu nataka kuwatumikia, tatizo la hawa wenzangu wanaweka mbele maslahi ya pesa kuliko utumishi.
"Haja yangu kubwa nataka niwasaidie wananchi wapate msaada wa kisheria bila ya kuwa kipato chochote na pesa tutapata Ruzuku kutoka Serikalini, na Serikali imekubali kutoa shilingi Bilioni 1.4," amefafanua Prof. Edward Hoseah.

Post a Comment

0 Comments