Waziri Bashungwa atoa maagizo kwa wakuu wa mikoa,wilaya nchini

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini kusimamia kikamilifu utoaji wa huduma ya dharura katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuondoa urasimu unaochelewesha mgojwa kupata huduma.
Bashungwa ametoa maelekezo hayo mkoani Tabora katika warsha ya Sema na Mama wakati akijibu hoja na kero ya ucheleweshwaji wa huduma kwa wagojwa katika huduma ya dharura katika zahanati, vituo vya afya na hospitali mkoani humo.

“Utoaji wa huduma za dharura katika vituo vya kutolea huduma za afya itolewe kama dharura, unaweza kumuhudumia mgojwa wakati utaratibu wa kujaza taarifa na maelezo unaendelea ili kuokoa maisha yake, hivyo nawaelekeza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia utoaji wa huduma hiyo katika maeneo yao,”amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema Serikali inatambua Machinga kuwa ni sekta rasmi ndio maana imeelekeza kuwapanga katika maeneo rafiki na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara ambapo itakuwa rahisi kuwafikia na kuwapelea huduma mbalimbali.

Amesema, tayari Serikali imewaelekeza wakuu wa mikoa yote kushirikiana na viongozi wa wafanyabishara wadogo kujadili na kutafuta namna bora ya kuwapanga kulingana na mazingira mkoa husika yatakayowaezesha wateja wao kuwafikia.

Vile vile, Bashungwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa nafasi ya upekee kwa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali kama utoaji wa mikopo na ajira ambapo asilimia tatu na nafasi za ajira zinazotolewa zimeelekezwa kwa watu wenye ulemavu.

Pia, amesema Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 za halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na sasa wakurugezi watapimwa kwa namna wanavyotenga fedha hizo kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa kuzigawa bila upendeleo kwa kuwanufaisha wahusika.

Warsha ya Sema na Mama iliwakutanisha viongozi wa Serikali na makundi mbalimbali ya wananchi wa Mkoa wa Tabora ambao ni Machinga, wakulima, bodaboda, walemavu na watu wenye mahitaji maalum na kupata nafasi ya kusikilizwa na kujibiwa moja kwa moja na viongozi hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news