Ziara ya Mtendaji Mkuu wa TARURA yaleta faraja kwa wananchi Kaseke

NA RAPHAEL KILAPILO

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff ameleta faraja kwa wakazi wa Kaseke baada ya kutembelea daraja la Kaseke lililoharibiwa na maji ya mvua na kumuagiza meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Innocent Mlay kujenga daraja la muda kwa haraka ili wananchi wasipate usumbufu wa kupita.
Mhandisi Seff ametembelea daraja hilo linalounganisha Vijiji vya Kaseke, Mbugani na Itenka Kata ya Kaseke, Mpanda katika ziara yake Mkoani Katavi na kukuta wananchi wakikipishwa kiasi cha kati ya shilingi 100 - 500 kwa siku kuvuka katika kivuko kilichojengwa na baadhi ya wanakijiji.

Amewataka kusitisha maramoja tozo wanayowalipisha wananchi nakumuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi Mhandisi Mlay kurudisha gharama ya shilingi 1,500,000 waliyodai ni pesa iliyotumika kujenga kivuko hicho ili wananchi wavuke bila kulipa.

“Nimesikitishwa kuona wananchi hasa wakinamama wanalipishwa kuvuka hapa, sasa msitishe maramoja kuwalipisha na Meneja atarudisha hizo gharama mlizosema,” alisema Mhandisi Seff.

Kwa upande wao wananchi wa Kaseke wameushukuru uongozi wa TARURA kwa kutembelea eneo hilo, na kuleta suluhisho la adha kubwa walizokuwa wanazipata.

“Tunakushukuru sana kiongozi ulivyofika hapa, kwa kweli adha tunazopata ni kubwa sana, wakina mama hapa tunapata shida ya kwenda zahanati na watoto na tukivuka hapa tunalipishwa, sasa tunafurahi umesema tusilipe na pia mnatujengea daraja hilo la muda,” alisema mama Elizabeth Milambo, mkazi wa Kaseke.

Post a Comment

0 Comments