WAZIRI MKUU AAGIZA PASI ZA KUSAFIRIA ZA WAKANDARASI ZIKAMATWE

*Ni za Wakorea wanaojenga meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu

*Akagua daraja la Busisi-Kigongo, aagiza watumishi walipwe stahiki zao

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa kwa pasi za kusafiria za wataalamu wa kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini wanaojenga meli ya MV Hapa kazi Tu jijini Mwanza hadi wakamilishe kazi yao.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumamosi, Mei 7, 2022 wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa mkoa huo mara baada ya kukagua ujenzi wa meli hiyo katika eneo la Mwanza South, wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza.

"Nimemwagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa akamate pasi zao mara moja na ahakikishe hakuna mtu anatoka nje ya mkoa huu hadi hii kazi ikamilike. Nimeambiwa wako saba, lakini hapa wako watatu. Watafuteni hao wengine wako wapi.”

Wenye pasi hizo ni Mkurugenzi wa GAS Entek, Bw. Dong Myung Kwak, na wasaidizi wake Bw. Kyunghan Choi na Bw. Kyuh Yun Kwak ambaye ni mtoto wa Mkurugenzi huyo.

“Nimeingia ndani kukagua kazi ya ujenzi lakini sijaridhika nayo. Katika maelezo yao nimebaini kuwa kampuni tuliyoingia nayo mkataba ya GAS Entec imeuza share zake bila Serikali kuarifiwa. Waliouziwa, walipokuja walishangaa kuona ujenzi wa meli kwa sababu suala la ujenzi liko nje ya mauziano yao."

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mwanza kwa ziara ya siku moja, amesema Serikali imeshalipa asilimia 80 ya gharama za ujenzi wa meli hiyo lakini kazi iliyofanyika kwa mujibu wa mkataba ni asilimia 65 tu. Amesema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa wafanyakazi walikuwa 118 lakini sasa wamebakia 22 t

"Haiwezekani tuwalipe hela hiyo, kazi haiendi kama ilivyopaswa. Tena wamepunguza Wafanyakazi kutoka 118 hadi 22, tunajuaje kama kesho watawaondoa hao 22 na wao wenyewe wapande ndege kurudi kwao, au waende Nairobi kupanda ndege."

Amesema ameshawasiliana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ameridhia hatua hiyo. “Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia hatua hii.”

“Hawa watu wasiondoke hadi kazi ikamilike na kama wataondoka basi atakayewadhamini ni Balozi wao. Serikali tutaendelea kuwasiliana na Balozi wa Korea Kusini na tunaamini kazi hii itakamilika. Wizara husika simamieni na kuhakikisha kazi inakamilika kwa mujibu wa mkataba.”

Waziri Mkuu amesema hakuna mradi wa kimkakati ambao utakwama. “Mheshimiwa Rais ameagiza tusimamie hii miradi, nasi ndiyo maana tuko tuko barabarani kila siku Ninawaomba Watanzania muamini kuwa Serikali yenu iko imara. Na pia niwahakikishie viongozi wa Chama cha Mapinduzi mliopo hapa kwamba Ilani yetu itatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90,” amesema.

Mapema, Mkurugenzi wa GAS Entek, Bw. Kwak alimweleza Waziri Mkuu kuwa amelazimika kupunguza wafanyakazi kwa sababu ana makontena matatu bandarini ambayo anataraji yataanza kutoka baada ya wiki mbili.

Kauli ya Bw. Kwak ilikanushwa na Meneja Mradi ambaye pia ni Mhandisi Mkazi, Lt. Col. Vitus Mapunda kwamba makontena matatu ni sehemu ndogo sana ya kazi iliyobakia na ambayo inatakiwa kuwa imefikiwa.

Gharama za ujenzi wa meli hiyo ni dola za Marekani milioni 39 sawa na sh. bilioni 80

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa baada ya kukagua ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu alielekea kwenye eneo la Kigongo Busisi kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la JPM lenye urefu wa kilomita tatu.

Akiwa katika eneo hilo ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikutane na watendaji wa Idara ya Kazi mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha watumishi katika mradi huo wanalipwa stahiki zao ipasavyo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mbunge wa Sengerema, Bw. Hamisi Tabasamu aliyedai kuwa licha ya mradi huo kuendelea lakini watumishi wamepungua na wanakimbilia katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

"Mkandarasi aimarishe utendaji kazi ili ujenzi wa daraja hili ukamilike. Pia wananchi nawaomba mtoe ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi iendelee vizuri."

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Mhandisi Benjamin Michael alisema awali kulikuwa na wafanyakazi 813 na sasa wamebaki 744 baada ya wengine kuacha kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news