BRELA yawataka wamiliki wa makampuni kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa

NA LANGO LA HABARI

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wamiliki wa makampuni kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa (Beneficial Owners) ili kutambua wamiliki halali kwa mujibu wa sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi na Kaimu (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wadau walioshiriki katika Warsha ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za wamiliki manufaa (beneficial owners) iliyofanyika leo Juni 02, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Benki Kuu Mkoani Mwanza. 

Akizungumza leo Juni 2, 2022 katika warsha ya siku mbili kuhusu uhamasishaji wa wadau kutoa taarifa hizo inayo fanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Benki Kuu jijini Mwanza, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kampuni na Majina ya Biashara, Meinrad Rweyemamu amesema kuwa taarifa hizi zinapaswa kuwasilishwa kwa mujibu Sheria Ili kupata taarifa muhimu na sahihi za mmiliki halali wa kampuni.

Rweyemamu amesema kuwa, taarifa za Mmiliki Manufaa zinatakiwa ili pia kumfahamu mtoa maamuzi katika kampuni kwa lengo la kupunguza mianya ya utakatishaji fedha na kutambua vyanzo vya fedha vya wamiliki wa kampuni kwa usalama wa Taifa na uchumi kwa ujumla.
"Kuna baadhi ya wamiliki wa kampuni wanaonekana katika mfumo Ila katika uhalisia siyo wamiliki halali, hivyo ni vyema taarifa hizi zikawakilishwa kwa Msajili Ili Mmliki Manufaa atambulike, kwani kuna uwezekano mkubwa kuwa mtu anamiliki kampuni lakini hataki kujulikana, hivyo taarifa hizi zitasaidia kumjua Mmliki Manufaa ni nani katika kampuni," amefafanua Rweyemamu.

Amesema kuwa, awali mfumo ulikuwa unapokea taarifa bila kujali kinachofanyika, mtaji unatoka wapi, hivyo suala hilo likawa chanzo cha mianya ya rushwa na tishio la kiusalama, ndiyo maana Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha ikapitishwa hivyo, kampuni zikatakiwa kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa ili ifahamike chanzo cha fedha wanazomiliki.
Baadhi ya wadau walioshiriki katika Warsha ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za wamiliki manufaa (beneficial owners) iliyofanyika leo Juni 2, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Benki Kuu mkoani Mwanza.

“Dhana hii ni nzuri na ni lazima ifahamike kwa wadau na wamiliki wa kampuni, kwani inatoa wigo kwa Serikali kufanya maamuzi sahihi kama kuzuia masuala ya utakatishaji fedha, rushwa, kupanga kodi, pamoja na kuzuia mianya ya ugaidi, Dunia nzima inaelekea huko, hatuna budi kuelekea huko,"amesema Bw.Rweyemamu.

Aidha, ameowaomba wadau walioshiriki warsha wakiwemo Mawakili na Wawakilishi wa wamiliki wa kampuni kutoa mwanga kwa wadau wengine Ili dhana hiyo iwe yenye kujenga taifa la Tanzania.

Awali akifungia Warsha ya mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amewapongeza wadau kujitokeza kwa wingi na kuomba waendelee kutoa ushirikiano kwa BRELA ili Kufanikisha dhana nzima ya urasimishaji biashara nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi katika Warsha ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za wamiliki manufaa (Beneficial Owners) iliyofanyika leo Juni 2, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Benki Kuu Mkoani Mwanza.

Amesema kuwa, taarifa za Wamiliki Manufaa zinapaswa kuwasilishwa kwa wakati kwani muda wa uwasilishaji uliongezwa na Serikali hadi Juni 30, 2022, Ili kufanikisha suala hilo.

Hata hivyo, ameitaka BRELA kuendelea kutoa elimu hiyo ili kuwafikia wamiliki wa kampuni wengi zaidi.
Afisa Sheria wa Brela, Vicensia Fuko (kushoto), Afisa usajili Jacob Mkuye (katikati) na Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Makampuni kutoka Brela, Leticia John Zavu wakiwa katika Warsha ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za wamiliki manufaa (beneficial owners) iliyofanyika leo Juni 02, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Benki Kuu Mkoani Mwanza.(Picha zote na Samir Salum, Lango la habari).

Wakala Wa Usajili Wa Biashara na Leseni (BRELA) imeanza kutoa mafunzo katika ya siku mbili ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za wamiliki manufaa (Beneficial Owners) yalioanza leo Juni 02, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Benki Kuu Mkoani Mwanza na kufikia tamati kesho Juni 3, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news