Dkt.Grace awataka watumishi wa Afya kuzingatia maadili

NA OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Grace Magembe amewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi huku wakizingatia maadili na miongozo ya utendaji kazi.
Dkt.Magembe ametoa rai hiyo Juni 25, 2022 mkoani Kagera katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika mkoa huo pamoja na kukagua utoaji wa huduma za Afya.

Alisema, ni vyema watumishi wa sekta ya afya wakizingatia maandili na miongozo ili kutekeleza azma ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
“Hakikisheni mnatoa huduma bora kwa wananchi, sitapenda kusikia wananchi wanatamkiwa lugha isiyo nzuri wala kukaa muda mrefu hospitali kusubiri huduma.

"Hakuna kitu kizuri kuwepo mawasiliano kati ya watoa huduma na wananchi kama kuna dharura, mmetingwa na wagonjwa wengi au mnakabidhiana wagonjwa ni wajibu wenu kutoa taarifa kwa wananchi ambao wanasubiria huduma, mkikaa tu huko ndani hamsemi chochote mwananchi lazima alalamike,"alisema Dkt.Magembe.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inawekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za Afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kuajiri watumishi hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha anazingatia maadili ya kiutendaji kazi.

Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuimarisha utaratibu wa kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na kuweka bei za huduma zinazotolewa kwenye mbao za matangazo ili kuimarisha uwazi na kumpa urahisi mwananchi anapotaka kupata huduma.

Pia amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuhakikisha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 watumishi wote wa idara ya Afya wanapewa mafunzo elekezi ya nyenzo ya ukaguzi wa huduma za afya (Clinical audit tool) ili kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Dkt.Magembe pia amezielekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinazingatia ujenzi wa miundombinu jumuishi kwa watu wenye ulemavu wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuleta usawa kwa kila mwananchi wakati wa utoaji huduma.

Haya hivyo, Dkt. Magembe hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya afya inayotekelezwa katika Halmashauri ya Karagwe hususani jengo la wagonjwa wa dharura(EMD).

Kutokana na hali hiyo, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karagwe, Michael Nzyungu kuhakikisha anaimarisha usimamizi na kuhakiksha anakamilisha ujenzi wa jengo la dharura sio zaidi ya Juni 30 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments