Maumivu ya Simba SC si ubingwa wa Yanga tu, bali kuwekwa 'sero' na maafande

NA DIRAMAKINI

WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu NBC Tanzania Bara, Yanga SC wakitua jijini Dar es Salaam leo wakitokea jijini Mbeya walikokabidhiwa taji lao la msimu huu, watani wao Simba SC wamejikuta wakiwekwa 'sero' na maafande wa Tanzania Prisons baada ya kutandikwa bao moja huko huko Mbeya walikotokea wenzao. 
Mashabiki wa Yanga SC wakiwa katika mapokezi ya kombe lao (kushoto), kulia ni Simba SC wakitoshana nguvu na Tanzania Prisons leo huko Sokoine jijini Mbeya. (DIRAMAKINI)

Wenyeji Tanzania Prisons wametumia vyema uwanja wake wa Sokoine jijini Mbeya baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC.

Bao pekee la Prisons limefungwa na beki wake Benjamin Asukile dakika ya 54 baada ya piga nikupige kwenye lango la Simba SC na kumshinda kipa Beno Kakolanya.

Matokeo haya yanakuwa na faida zaidi kwa Prisons, kwani baada ya mchezo huo inasogea hadi nafasi ya 14 na alama 29 na kuishusha Biashara United iliyopo nafasi ya 15 na kwa alama 28 baada ya timu zote kucheza michezo 29 hadi sasa.
Aidha,huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Prisons dhidi ya Simba SC ikiwa nyumbani, kwani mara ya mwisho walipokutana katika Uwanja wa Nelson Mandela Oktoba 22, 2020 ilishinda pia bao 1-0.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliozikutanisha timu hizi Februari 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilishinda bao 1-0.

Huu unakuwa ni mchezo wa tatu kwa Simba kupoteza baada ya kufungwa bao 1-0 na Mbeya City Januari 17 na Kagera Sugar Januari 26,2022.

Juni 25, 2022 mshambuliaji, Shiza Ramadhani Kichuya ameifungia mabao matatu Namungo FC ikitoka nyuma na kuichapa timu yake ya zamani, Mtibwa Sugar 4-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara katika uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Kichuya alifunga mabao hayo dakika za 24, 51 na 66 huku bao lingine la Namungo likifungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 73, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Nzigamasabo Steve kwa penalti dakika ya sita na George Makang’a dakika ya 10.

Namungo FC inafikisha alama 40 baada ya ushindi huo na kusogea nafasi ya tano, wakati Mtibwa Sugar inabaki na alama zake 31 nafasi ya 12 baada ya wote kucheza mechi 29 hadi sasa.

Post a Comment

0 Comments