MAPAMBANO YA VITENDO:Sisi tuloaminiwa, tukachapa kazi kweli, Pazuri patafikiwa

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

JUNI 14, 2022 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba amewasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23.

Bajeti hiyo inawasilishwa kwa mujibu wa Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 23 (3) cha Sheria ya Bajeti, Sura 439 pamoja na Kifungu cha 124 (4) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni 2020.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23 yameandaliwa kwa kuzingatia nyaraka na miongozo mbalimbali ikiwemo Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26 ambao umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020, Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki 2050, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030,Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeyaridhia.

Hii ni miongoni mwa bajeti nzuri ambazo zimegusa katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi ili kuwezesha ustawi ubora wa maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Bw.Lwaga Mwambande ambaye ni mshairi wa kisasa, anakupitisha katika baadhi ya mambo mazuri yaliyomo ndani ya makadirio hayo kwa njia ya shairi ambayo anasema, kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa manufaa ya Taifa, mambo yatasonga mbele kwa kasi, endelea;

a:Maisha ya unafuu, bajeti ya serikali,
Mambo matano makuu, yameshatajwa kamili,
Hapa ninayanukuu, yaingie kwa akili,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

b:Waziri Fedha Mipango, katoa hotuba kali,
Inavyo vingi vigongo, hapa nakupa usuli,
Ili tufikie lengo, maendeleo ya kweli,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

c:Katika bajeti yetu, ile iliyo halali,
Sera za mapato yetu, kipaumbele adili,
Pia matumizi yetu, ufanisi yatajali,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

d:Mapambano ya vitendo, ili rushwa kukabili,
Pia kuongeza mwendo, uzalishaji wa kweli,
Kutoa mafindofindo, tuweze kufika mbali,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

e:Kutengeneza ajira, hilo jambo zuri kweli,
Wingi vijana ishara, muhimu kwa serikali,
Ile nguvu kazi bora, isizidi saga soli,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

f:Idadi vijana wetu, ni kama nusu kamili,
Hivyo ni muhimu kwetu, kuzijali zao hali,
Wasibaki kukaa tu, wafanye kazi halali,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

g:Hatua zachukuliwa, kwa vile hatuna hali,
Jinsi tunatibuliwa, vita vile kule mbali,
Athari twaingiliwa, maisha yawa aghali,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

h:Kama tukifanikiwa, hatua hizi kwa kweli,
Sisi tuloaminiwa, tukachapa kazi kweli,
Pazuri patafikiwa, tuwe na njema kauli,
Tumesikia asante, kazi na iendelee.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments