MAPATO:TEHAMA nyenzo muhimu, Janjajanja za mpito, namba watasoma

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

MATUMIZI sahihi ya Mfumo wa Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG) kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanatajwa kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu za kurahisisha na kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa wakati, mapato ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Licha ya TEHAMA, pia viongozi katika ngazi mbalimbali kuanzia mamlaka za mitaa hadi Taifa na katika taasisi au mashirika, wanahimizwa kuzingatia ubunifu ambao utaongeza ufanisi wa utoaji huduma bora kwa umma na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Pia kila mwananchi analo jukumu la kuhakikisha kila anaponunua au kuuza bidhaa yoyote anatoa au kupokea risiti halali ya kielektroniki ili kuimarisha kasi ya Serikali kukusanya mapato.

Katika mwendelezo wa kubuni vyanzo vipya na kuboresha vilivyopo vya mapato, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba amesema Serikali inakusudia kutoa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuanza kulipa kodi.

Amesema, ili kufikia azma hiyo wataanza kutoa TIN kwa kila mtanzania kuanzia umri wa kuanzia miaka 18 kwa utaratibu wa usajili wa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) unaomtaka kila mwananchi mwenye umri huo wa au zaidi kujisajili.

“Napendekeza kuwa wale wote wenye NIDA kwa sasa wapatiwe namba ya TIN na itumike kwenye miamala yote inayofanyika katika ununuzi na mauzo yanayofanyika ndani ya nchi,”amesema Mheshimiwa Waziri, Juni 14, 2022 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2022/23 bungeni jijini Dodoma.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kupitia shairi lake anakazia umuhimu wa kila mmoja kujituma kwa nafasi yake, kuonesha uadilifu na uwajibikaji ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato ya kutosha ambayo yatawezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini, karibu;

A:Kuyakusanya mapato, itatumika TEHAMA,
Kuhakikisha mapato, Serikali yayasoma,
Janjajanja za mpito, huko namba watasoma,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

B:Lengo kukomesha rushwa, inayofanya kukwama,
Waliko watafurushwa, wafike kwa mahakama,
Vitendo vyao twachoshwa, jinsi mapato yahama,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

C:Hatua nyingine nyingi, Waziri Nchemba kasema,
Wananchi walo wengi, umri ulosimama,
Hasa wale hawachangi, nako tuanze kugema,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

D:Miaka kumi na nane, jina lako linasoma,
Tayari wewe mnene, waziwazi twakusema,
Kipato chako tuone, kwenye kodi unasoma,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

E:Tapata namba ya TIN, ya kujulikana vema,
Wala sio ufitini, hizo hatua lazima,
Walipa kodi nchini, iwe kwa watu wazima,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

F:Uzalishaji wote halali, hata kama unalima,
Kulipa kodi dalili, unawajibika vema,
Ili yetu Serikali, vema iweze simama,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

G:Serikali imepanga, na Waziri amesema,
Wajibu sisi kuunga, kwa kufanya mambo mema,
Kwa vitendo si kuchonga, Uchumi ukue vema,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

D:Twataka maendeleo, nchi iweze kuvuma,
Kodi si upendeleo, kwa kila mtu mzima,
Haya yawe mapokea, kulipa bila kugoma,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

F:Hivyo ni jambo muhimu, sote tupeana hima,
Kila mtu yake zamu, ni kodi bila kukwama,
Tupate mambo matamu, nchi ipate simama,
Ukusanyaji mapato, TEHAMA nyenzo muhimu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments