SANTE SANA SERIKALI:Watoto kazi moja,Msijeleta vioja, matokeo yawe ziii

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)
 
MBALI na kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanua wigo zaidi wa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata haki ya kusoma kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita bila malipo yoyote.

Hayo yamedhihirika, Juni 14, 2022 bungeni jijini Dodoma baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba kupendekeza kufutwa ada kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita ili kuwapunguzia gharama za masomo nchini.

"Napendekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Kwa hatua hiyo, elimu bila ada ni kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita,”amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Mheshimiwa Waziri ameyasema hayo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2022/2023.

Amesema, kwa sasa wanafunzi wa Kidato cha Tano ni 90,825 na kidato cha Sita ni 56,880 na mahitaji ya fedha ni shilingi Bilioni 103.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande ana jambo la kukushirikisha baada ya kupata taarifa njema kutoka serikalini, ungana naye katika shairi hapa chini ujifunze jambo;

1:Ada vidato vya juu, sasa haitakuwepo,
Watoto wa huko juu, ni elimu peke ipo,
Hili kweli jambo kuu, kwa wazazi wengi tupo,
Sasa anza chekechea, sekondari bila ada.
Sasa anza chekechea, sekondari bila ada,

2:Msingi yote pokea, sekondari bila shida,
Vidato vyote pokea, masomo kwa zote kada,
Sasa elimu kwa wote, hadi kidato cha sita.
Sasa elimu kwa wote, hadi kidato cha sita,

3:Chekechea pita wote, msingi mtaipata,
Na msingi soma wote, sekondari yawaita,
Kidato cha Nne peta, nenda zako Eilevo.
Kidato cha Nne peta, nenda zako Eilevo,

4:Masomo utayapata, walimu toka vitivo,
Hao si wa kuokota, walipita Eilevo,
Ni Serikali tayari, inakwenda kulipia.

5:Ni Serikali tayari, inakwenda kulipia,
Awamu ya Sita nzuri, yake Rais Samia,
Imeongeza sukari, nyuma tulikoanzia,
Toka Kidato cha Nne, sasa Kidato cha Sita.

6:Toka Kidato cha Nne, sasa Kidato cha Sita,
Imekuja kivingine, nyayo za nyuma kufwata,
Sisi sote tuungane, shangwe iweze kupata,
Kwa sasa ni mwendokasi, elimu kwa kwenda mbele.

7:Kwa sasa ni mwendokasi, elimu kwa kwenda mbele,
Zikitokea nafasi, ni watoto kwenda shule,
Hakuna mwenye mkosi, abakie pale pale,
Serikali ni sikivu, kwa mahitaji ya watu.

8:Ni sikivu Serikali, kwa mahitaji ya watu,
Inakuwa shida kweli, hasa hasa badhi yetu,
Kuweza pata shekeli, wasome watoto wetu,
Sasa kazi kwetu moja, ni sare na daftari.

9:Sasa kazi kwetu moja, ni sare na daftari,
Watoto moja kwa moja, waweze funga safari,
Wakakutane pamoja, kupata elimu nzuri,
Maboresho ya huduma, kweli yanaendelea.

10:Maboresho ya huduma, kweli yanaendelea,
Jinsi watu wanasema, serikali yapokea,
Na vyema inajituma, neema tunapokea,
Watoto ni kazi moja, ya kusoma kwa bidii.

11:Watoto ni kazi moja, ya kusoma kwa bidii,
Sikiliza jenga hoja, kwa akili na utii,
Msijeleta vioja, matokeo yawe zii,
Sasa tulolipa ada, sasa tutarudishiwa?

12:Hivi tulolipa ada, sasa tutarudishiwa?
Changamoto nazo shida, bado bado twazidiwa,
Isijechukua muda, kwani tulishaishiwa,
Sante sana Serikali, hili la ada kuona.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments