Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia waandaliwa

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha na Mipango imesema kuwa, hadi Aprili 2022 imefanikiwa kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia kama ilivyopangwa na ushauri wa kitaalamu kwa miradi ya PPP 32 iliyowasilishwa na mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi mbalimbali za Serikali.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameyasema hayo leo Juni 7, 2022 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, Makadirio ya Mapato na Matumizi ambapo ameliomba Bunge kuiidhinishia wizara yake bajeti ya shilingi trilioni 14.94.

Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 13.62 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 1.32 ni matumizi ya maendeleo kwa mafungu yake nane kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2022/2023.

Amebainisha kuwa, hatua hiyo inatokana na mipango ambayo walijiwekea ya kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia 2021/22-2025/26.

Sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu miradi inayoibuliwa na kuandaliwa na Mamlaka za Serikali na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Mamlaka za Serikali.

"Kati ya miradi hiyo, mradi wa Uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Kwanza umepata mbia na maandalizi ya majadiliano ya uendeshaji wa mradi yanaendelea.

"Aidha, miradi minne ambayo ni ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne,ujenzi wa jengo la biashara katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere, Ujenzi wa Kiwanda cha kuzalisha Dawa na Vifaa Tiba na Kiwanda cha Kutengeneza Simu ipo katika hatua za ununuzi, mradi mmoja upo kwenye hatua ya mwisho ya upembuzi yakinifu,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Pia amebainisha kuwa, miradi saba ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu wa awali na miradi 19 ipo katika hatua ya andiko dhana.

Post a Comment

0 Comments