Wabunge wajifunza namna ya kukabiliana na wanyama wanaovamia makazi ya wananchi, washauri

NA DIRAMAKINI

KAMATI ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imewashauri wananchi wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wanaokabiliwa na changamoto ya kuvamiwa na tembo, kuendelea kutumia mbinu zinazofundishwa na wataalamu ili kukabiliana na kadhia hiyo wakati Serikali inaendelea kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo.
Ushauri huo umetolewa Juni 26, mwaka huu na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Ally Makoa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini wakati wa ziara yao wilayani Mvomero kwa ajili ya kujifunza mbinu za kukabiliana na tembo, mafunzo yaliyofanyika katika Kijiji cha Doma wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Mara baada ya mafunzo hayo, kamati hiyo iligundua kuwa wananchi walio wengi wilayani humo hawaoneshi mwitikio wala nia ya dhati ya kujifunza mbinu za kukabiliana na tembo hao zinazotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (TAWIRI) na kuwashauri kukubali kujifunza na kutumia njia hizo wakati Serikali inaendelea kutafuta njia sahihi na ya kudumu ya changamoto hiyo.
Wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo nao wametoa michangao ya mawazo yao pamoja na kupendekeza mbinu mbadala za muda katika kutatua kero hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na kifaa kama darubini ya kuangalia mienendo ya tembo katika maeneo yenye kero, kuongeza magemu, pamoja na kujenga uzio wa umeme.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema, suluhu ya kudumu ambayo inaendelea kufanyiwa kazi na Serikali ni kufanya upimaji wa maeneo yote ambayo ni mapitio ya wanyama hususan tembo hao yaani upimaji na kuyatambulisha kwa watanzania ili maeneo hayo yasiweze kutumika kwa matumizi yoyote ya shughuli za kibinadamu. 

Kuhusu kifuta jacho na kifuta machozi kwa ndugu waliopatwa na maafa, Waziri Pindi Chana ameahidi kulifanyia kazi suala hilo huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kupeleka orodha ya wananchi wanaotakiwa kulipwa kifuta jacho na kifuta machozi hicho ili waweze kulipwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela pamoja na kuishukuru kamati hiyo kutembelea mkoani humo kwa lengo la kutatua kero ya uvamizi wa mnyama tembo katika Kijiji cha Domana Wilaya ya Mvomero kwa jumla, yeye amejikita kuimarisha mawasiliano na mahusiano baina ya maafisa wa wanyama pori na wananchi wa maeneo yenye migogoro mingi mingi ili pale wananchi wanapotoa taarifa basi wataalamu waweze kufika kwa wakati.
Naye Diwani wa Kata ya Doma, Abdallah Elimu Kisuguru ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ameiomba Serikali pamoja na mbinu zote zinazoendelea kuwafundisha, ameishauri kujaribu kutumia mbinu ya wahenga wao ya kutumia magemu akiamini kuwa njia hiyo ndio itakuwa mwarobaini wa changamoto hiyo.

Akiwakilisha wananchi wenzake Mariam Mnamba ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugono amekiri kuwa pamoja na kutumia mbinu zinazofundishwa na wataalamu hao bado juhudi hizo hazijazaa matuda na tembo wameendelea kusumbua katika kijiji chake huku akimwomba Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwatazama kwa jicho la pekee kwani mwaka huu hawapata mavuno yoyote kutoka masahambani mwao kwa sababu ya hao tembo.

Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Antoni amesema, katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2021/2022 Wizara hiyo imepokea jumla ya taarifa 3,289 kupitia fomu za maombi ya kifuta jasho na kifuta machozi ambapo taarifa z3,256 nia uharibifu wa mashamba, 3 vifo vya mifugo, 11 watu kujeruhiwa na 19 vifo vya watu.
Aidha, amesema katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2020/2021 jumla ya shilingi 601,875,500 zimetumika kulipa familia za waathirika kama kifuta jasho na kifuta machozi.

Moja ya mbinu walizojifunza waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi na Maliasili ni pamoja na urushaji wa vilipuzi, matumizi ya oil chafu iliyochanganywa na pilipili, matumizi ya tochi, matumizi ya ving’ora mbinu ambazo ameonesha hawakuridhika kutaka Serikali kuendelea kutafuta njia mbadala ikiwa ni pamoja na kukaa na wananchi kuwasikiliza mapendekezo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news