Waziri Dkt.Nchemba:Tathimini inaonesha Deni la Serikali ni himilivu kwa miaka 20 ijayo

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha na Mipango imesema kuwa,matokeo ya tathmini ya Deni la Serikali yanaonesha uhimilivu katika kipindi cha muda mfupi, wakati na mrefu wa deni hilo.

"Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni kufanya tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali kwa miaka 20 ijayo, kuanzia 2021/22 hadi 2040/41. Matokeo ya tathmini yanaonesha kuwa, deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wakati na mrefu.
Hayo yamesemwa leo Juni 7, 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, Makadirio ya Mapato na Matumizi ambapo ameliomba Bunge kuiidhinishia wizara yake bajeti ya shilingi trilioni 14.94.

Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 13.62 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 1.32 ni matumizi ya maendeleo kwa mafungu yake nane kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2022/2023

"Mheshimiwa Spika, wizara imeendelea kusimamia deni la Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134. Kati ya Julai 2021 na Aprili 2022, Wizara imelipa deni lote lililoiva katika kipindi hicho la jumla ya shilingi trilioni 6.81,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Amefafanua kuwa, kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni shilingi trilioni 4.21, ikijumuisha riba shilingi trilioni 1.72 na mtaji shiling trilioni 2.49.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema,deni la nje ni shilingi trilioni 2.60, ikijumuisha riba shilingi trilioni 0.572 na mtaji shilingi trilioni 2.02.

Pia amesema, taarifa inaonesha kuwa, thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 31.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55.

"Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu, wananchi na wadau wote wa maendeleo kuwa taarifa kamili ya tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali inapatikana katika tovuti ya wizara ambayo ni www.mof.go.tz,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news