Waziri Mkuu:Tutaendelea kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kujenga mustakabali wa nchi yetu.Askofu Wolfgang John Pisa akiwa amelala kifudifudi katika ibada ya kusimikwa kwake kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi iliyofanyika kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alishiriki katika Ibada hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa kauli hiyo leo Juni 26, 2022 katika ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mteule Wolfgang Pisa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi katika viwanja vya Ilulu, Lindi.

“Maendeleo ya nchi hayawezi kuimarika kama tutakuwa wabinafsi. Tukiimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wa kila mtu, tutaleta maendeleo ya Taifa letu kwa haraka.” 

Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na dini zote katika kukuza ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii ili kuimarisha maisha ya kila Mtanzania na Taifa kwa ujumla. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Ibada ya kumsimika Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi Wolfgang John Pisa wakifuatilia ibada hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. Kushoto ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 

Amesema kwa kuzingatia hayo, Serikali imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi zikiwemo taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa. 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya viongozi wote wa dini. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kuwaongoza watu kiroho kwa kuwapa mafundisho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani. 

“Vilevile, mmekuwa mkiwasaidia watu katika shida mbalimbali hususan wale wenye uhitaji kama yatima na wajane sambamba na kutoa ushauri nasaha na malezi bora kwa vijana.” 
Baadhi ya washiriki wa Ibada ya kusimikwa Askofu Wolfgang John Pisa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi wakifauatilia Ibada hiyo kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga akitoa salamu za baraza hilo amesema Kanisa Katoliki limeahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika masuala yote ambayo Serikali imekusudia kuyafanya kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania. 

Rais huyo wa TEC ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya amesema hivi sasa kanisa hilo linawahamasisha waumini wake kushiriki katika zoezi la Sensa Watu na makazi litakalofanyika Agosti 23, 2022. 

Askofu Nyaisonga ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iendelee kuliunga mkono kanisa hilo katika shughuli mbalimbali linazozifanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo ikiwa ni pamoja na suala la elimu na huduma nyingine za kijamii. 
Baadhi ya Mapadri walioshiriki katika Ibada ya kusimikwa Askofu Wolfgang John Pisa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi wakifauatilia Ibada hiyo kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Naye, Askofu Pisa baada ya kusimikwa amewashukuru wana-Lindi ambao wamempokea na kuonesha umoja na ushirikiano bila ya kujali madhehebu yao, hivyo amesema hatua imempa moyo na imani kwamba atafanyakazi kwa kushirikiana na wananchi wote. 

Amesema kwa sasa jamii imevamiwa na utandawazi ambao umepokelewa na watu wengi na kuleta athari kubwa kiimani, utamaduni na mila, hivyo kuchangia mmomonyoko wa maadili hususani kwa vijana. “Nawaomba Watanzania wenzangu tubaki katika mila na utamaduni wetu wa asili na tusizolewe na upepo wa utandawazi.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news