Wizara ya Fedha yajivunia hatua njema Sekta ya Fedha

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha na Mipango imesema kuwa, hadi Aprili 2022 imefanikiwa kuhuisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Bima, kuzindua Mpango wa Kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma wa mwaka 2020/21-2024/25 pamoja na nyenzo ya kufundishia.

Sambamba na kuandaa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa lengo la kutoa elimu ya fedha kwa umma, kuandaa rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Sekta ya Benki na Mkakati wake,kuandaa Mkakati wa Upatikanaji wa Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati na kuzindua Mkakati wa Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Njia Mbadala (Alternative Project Financing-APF Strategy).
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameyasema hayo leo Juni 7, 2022 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, Makadirio ya Mapato na Matumizi ambapo ameliomba Bunge kuiidhinishia wizara yake bajeti ya shilingi trilioni 14.94.

Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 13.62 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 1.32 ni matumizi ya maendeleo kwa mafungu yake nane kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2022/2023.

Amesema kuwa, wizara imeendelea kushirikiana na taasisi na mamlaka za usimamizi na udhibiti katika kusimamia na kuendeleza sekta ya fedha.

"Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Mali Zinazohamishika Sura 210, kwa lengo la kujumuisha masuala ya mikopo salama na masijala ya dhamana pamoja na mapendekezo ya uendelevu wa Mifuko ya Dhamana kwa Wajasiriamali Wadogo na Mauzo Nje ya Nchi (SME na Export Credit Guarantee Scheme),"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Masoko

Waziri Dkt.Nchemba akizungumzia kuhusiana na Masoko ya Mitaji, Dhamana na Bidhaa katika mwaka 2021/22, wizara ilipanga kuongeza bidhaa 38 ili kuimarisha ukwasi katika masoko ya mitaji, kuboresha kanuni za soko la hisa na kutoa leseni 150 kwa watendaji na washauri wa uwekezaji katika masoko ya mitaji.

Hatua nyingine amesema ilikuwa ni kuongeza idadi ya wataalamu wa masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya Kimataifa kutoka 601 hadi 650 na kutoa elimu kwa umma.

"Hadi Aprili 2022, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana imefanikiwa kutoa leseni 154 ikilinganishwa na leseni 144 zilizotolewa katika kipindi kama hicho mwaka 2021,ikiwa ni ongezeko la asilimia saba na kuongeza idadi ya watendaji wa masoko ya mitaji wanaotambulika kimataifa kutoka 601 hadi 667, sawa na ongezeko la asilimia 11,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Aidha, amefafanua kuwa idadi ya bidhaa katika masoko ya mitaji ambazo zinajumuisha hisa, hatifungani na mifuko ya uwekezaji wa pamoja zimeongezeka kutoka 599 na kufikia 637 sawa na ongezeko la asilimia 6.

Waziri Dkt.Nchemba akizungumzia kuhusu Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) amesema, lilipanga kuboresha Mfumo wa Uuzaji na Malipo kwa Njia ya Kielektroniki, kuandaa Sera ya TEHAMA, Sera ya usalama wa Mifumo ya TEHAMA na kuandaa miongozo ya mauzo ya bidhaa.

Mheshimiwa Waziri anasema, hadi Aprili 2022, "imefanikiwa kuboresha Mfumo wa Mauzo kwa Njia ya Kielektroniki na hivyo kuwa na uwezo wa kuuza mazao zaidi ya saba, kuandaa Sera ya TEHAMA na Sera ya Usalama ya TEHAMA kama sehemu ya kulinda mifumo inayotumika katika soko la bidhaa kwa ujumla na kuandaa miongozo ya mauzo ya zao la chai.

"Mifugo hai, ngozi,viazi, vitunguu na pilipili manga ambayo itaanza kutumika kuuza mazao hayo kupitia soko la bidhaa mara baada ya maandalizi ya Stakabadhi za Ghala kukamilika,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Benki

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa, wizara imeendelea kusimamia taasisi za benki ili kukuza mitaji, amana na ukwasi na hivyo kuchochea kasi ya utoaji wa mikopo kwa ajili ya uwekezaji na biashara katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Benki Kuu ya Tanzania

"Mheshimiwa Spika, shabaha ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa ni asilimia 5.0 mwaka 2021 na mfumuko wa bei kubaki ndani ya wigo wa kati ya asilimia 3.0 na 5.0. Ili kufikia azma hiyo, Benki Kuu ilipanga kukuza wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) kwa asilimia 10.0.

"Ukuaji wa fedha taslimu (M0) wa wastani wa asilimia 9.9, wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kwa asilimia 10.6 na kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi minne,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Amesema, hadi Aprili 2022 wastani wa fedha taslimu uliongezeka kwa asilimia 13.8 ikilinganishwa na asilimia 2.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2021, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikuwa kwa wastani wa asilimia 13.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.

Pia amesema,ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.4 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.3 kwa mwaka 2021.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema,akiba za fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.46 kiasi ambacho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.8 ikilinganishwa na lengo la nchi la miezi 4.0 na miezi isiyopungua 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Benki za Maendeleo

Waziri Dkt.Nchemba anasema kuwa, wizara inasimamia benki mbili za maendeleo ambazo ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Benki ya Maendeleo (TIB).

Amesema, kwa mwaka 2021/22, TADB ilipanga kutoa mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 203.50 kwa miradi ya uchakataji wa mazao, ununuzi wa mazao, ununuzi wa pembejeo, uwezeshaji wa wakulima wadogo kupitia vyama vya msingi (AMCOS), ununuzi wa zana za kilimo, kutoa dhamana kwa wakulima wadogo na SMEs na kufungua Ofisi ya Kanda ya Kusini na ofisi ndogo Morogoro.

"Hadi Aprili 2022, TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 116.36 kwa miradi 181 iliyowanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa 1,527,175 na kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa toka benki ilipoanza kufikia shilingi bilioni 364.50.

"Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizotekelezwa na TADB ni pamoja na kutoa mikopo ya shilingi bilioni 54.37 kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS) na kufanya mikopo iliyotolewa na mfuko huo kufikia shilingi bilioni 144.04 tangu ulipoanza rasmi udhamini wa mikopo mwaka 2018,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Amefafanua kuwa, mikopo hiyo imewanufaisha wakulima 987, biashara ndogo na za kati za kilimo (SMEs), na vyama vya msingi (AMCOS) katika mikoa 26 nchini.

Vilevile, amesema TADB imefungua Ofisi ya Kanda ya Kusini iliyopo mkoani Mtwara na ofisi ndogo mkoani Morogoro ambapo ofisi ya Kanda ya Kusini itahudumia mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

TIB

"Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo (TIB) ilipanga kutoa mikopo ya shilingi bilioni 54.59 katika sekta ya kilimo,viwanda, maji, nishati, utalii, na elimu na kukuza mizania ya benki kufikia shilingi bilioni 775.5.

Anasema, hadi Aprili 2022, Benki ya Maendeleo (TIB) imefanikiwa kutoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 17.91. Sekta zilizonufaika na mikopo hiyo ni maji, utalii, madini ya dhahabu na ujenzi. Waziri Dkt.Nchemba anasema kuwa,mizania ya benki ilikuwa na kufikia shilingi bilioni 625.78.

Benki ya TCB

Waziri amesema, katika mwaka 2021/22, Benki ya TCB ilipanga kuboresha mifumo ya benki ya kuzalisha mapato na utoaji huduma. "Hadi Aprili 2022, benki imefungua akaunti 29,488 za vikundi vya kawaida na kusajili vikundi 43,236 kupitia simu za mkononi kwa kushirikiana na Vodacom.

"Aidha, benki imebuni mradi wa vikundi vilivyombali na huduma za kifedha, ambapo jumla ya akaunti 16,558 zimefunguliwa.

"Vilevile, benki imefanikiwa kukusanya amana zenye thamani ya shilingi bilioni 937 na kutoa mikopo ya shilingi bilioni 736, ambapo shilingi bilioni 1.4 ni mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Taasisi za Bima

Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika mwaka 2021/22, wizara kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) ilipanga kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kusimamia vipindi 10 vya redio vya utoaji elimu na kutoa elimu kwa makundi maalumu ya Bodaboda, Bajaji, Vyama vya wafanyabiashara, vyama vya wasafirishaji pamoja na Jeshi la Polisi.

"Hadi Aprili 2022,TIRA imefanya ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani 19,221, kutoa elimu ya bima kwa umma kupitia vipindi tisa vya redio na runinga na makundi mbalimbali ya kijamii ambapo zaidi ya wananchi 514,112 wamefikiwa.

"Kati ya hao, 3,214 ni askari polisi wa usalama barabarani, 344 watumishi wa Serikali, 75 waandishi wa habari na watumishi wa vyombo vya habari na 510,479 madereva wa bodaboda, watu wenye ulemavu wa usikivu, wakulima na vyama vya ushirika,"amefafanua Mheshimiwa Waziri.

Pia amesema, katika mwaka 2021/22, Shirika la Bima la Taifa lilipanga kujenga mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Taarifa za Bima ili kuweka mazingira wezeshi na shindani.

Hadi Aprili 2022,amesema shirika limefanikiwa kuanza kuunda na kujenga Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Taarifa za Bima na kuanza kusimika mfumo wa Enterprise Resource Management System (ERMS) kwa ajili ya kusimamia taarifa za kihasibu.

Mifumo hiyo kwa pamoja anasema, inatarajiwa kuongeza ufanisi na uwazi katika utunzaji wa taarifa za wateja, ulipaji wa madai, utunzaji sahihi wa taarifa za kihasibu pamoja na kuwezesha wateja kukata bima na kuwasilisha madai yao kwa njia ya kielektroniki.

Uwekezaji na Uwezeshaji

Waziri Dkt.Nchemba amesema,wizara inasimamia taasisi mbili za Uwekezaji na Uwezeshaji ambazo ni Kampuni ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS) na Mfuko wa Huduma Ndogo za Fedha (Self Microfinace Fund).

Katika mwaka 2021/22,amesema UTT AMIS ilipanga kuongeza rasilimali za mifuko kwa asilimia 15,kuongeza idadi ya wawekezaji kwa asilimia tano na kutoa huduma kwa wawekezaji kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

"Hadi Aprili 2022, UTT AMIS ilifanikiwa kuongeza rasilimali za mifuko pamoja na huduma ya usimamizi wa mitaji binafsi kutoka shilingi bilioni 619.57 mwezi Julai 2021 hadi shilingi bilioni 927.45 mwezi Aprili 2022, sawa na ongezeko la asilimia 49.69.

"Katika kipindi hicho, idadi ya wawekezaji katika mifuko iliongezeka kutoka 172,242 hadi 194,632, sawa na ongezeko la asilimia 12.99. Kutokana na maboresho ya mifumo ya TEHAMA, asilimia 46.10 ya mauzo ya vipande katika kipindi hicho yalifanyika kwa njia ya kidijitali.

SELF

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Mfuko wa Huduma Ndogo za Fedha - SELF ulipanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 34.32 kwa wajasiriamali wadogo 17,852 na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo wapatao 265.

"Hadi Aprili 2021, mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 32.97, sawa na asilimia 96 ya lengo na kunufaisha wajasiriamali wadogo 13,744 na kutoa mafunzo kwa wajasiriamli wadogo 2,397,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.SOMA BAJETI YOTE HAPA>>>

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news