Wizara ya Fedha yaomba trilioni 14.94/-, yataja vipaumbele vyake

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Fedha na Mipango imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha shilingi trilioni 14.94 kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Hayo yamesemwa leo Juni 7,2022 bungeni jijini Dodoma na Waziri Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi.
Mheshimiwa Waziri amesema, kati ya fedha hizo shilingi trilioni 13.62 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 1.32 ni matumizi ya maendeleo kwa mafungu yake nane kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2022/2023.

Vipaumbele 2022/23

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa, katika mwaka 2022/23, Wizara ya Fedha na Mipango kupitia mafungu yake nane inatarajia kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo, shabaha na vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) wa kila Fungu na Taasisi zake.
Aidha, malengo, shabaha na vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya mwaka 2022/23 vimeibuliwa kutoka kwenye Mpango Mkakati wa Wizara 2021/22-2025/26, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22- 2025/26 na Ilani ya Chama Tawala (CCM).

"Ni kwa kuzingatia ukusanyaji, kutafuta na kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali, kuhudumia kwa wakati deni la Serikali pindi linapoiva, kufanya tathmini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ikiwa ni maandalizi mahsusi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050.

"Kufanya tathmini ya mfumo na muundo wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ili kuwezesha kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo, kurejesha Bahati Nasibu ya Taifa,kufanya tafiti katika sekta za uzalishaji ili kuibua fursa za uwekezaji, uwezeshaji na vyanzo vya
mapato ya Serikali katika muda mfupi, kati na mrefu.

"Kuendelea kutekeleza maagizo ya Serikali ya kutafsiri sheria za wizara na taasisi zake kwa lugha ya Kiswahili na kuhuisha Mwongozo wa Taifa wa Usimamizi wa Viashiria Hatarishi,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwingulu.

Matumizi

Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa,kwa upande wa matumizi ya maendeleo,wizara inatarajia kujielekeza katika maeneo kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa
Fedha za Umma Awamu ya Sita (PFMRP VI).

Pia kuandaa na kujenga ghala la takwimu (Data Warehouse),kuratibu na kusimamia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, kuziwezesha taasisi za wizara, hususan taasisi za elimu na mafunzo kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia na kuendelea na ujenzi wa jengo la wizara katika Mji wa Magufuli, Mtumba jijini Dodoma.

"Aidham kuendelea na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mhakikimali na Hazina Ndogo katika mkoa wa Geita, Njombe na Songwe na ukarabati wa jengo la wizara lililopo jijini Dar es Salaam, Hazina Ndogo Morogoro, Kigoma na Ruvuma,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Vipaumbele vya Taasisi

Amesema, wizara inatekeleza baadhi ya majukumu yake kupitia taasisi za elimu na mafunzo na elimu ya juu, bodi za kitaalamu na kitaaluma, usimamizi wa fedha, kodi, bima, ununuzi na ugavi, michezo ya kubahatisha, uwekezaji na uwezeshaji pamoja na takwimu.

Taasisi za Mafunzo ya Elimu ya Juu

"Mheshimiwa Spika, taasisi za Mafunzo ya Elimu ya Juu zinatarajia kudahili jumla ya wanafunzi 73,074, ikiwemo ngazi ya cheti 14,017, stashahada 19,427, shahada 37,450 na uzamili 2,180,"amesema Waziri Dkt.Nchemba.

Aidha, amesema chuo kinatarajia kuendeleza wahadhiri 196, ambapo ngazi ya uzamivu ni 158 na Uzamili 38 pamoja na kuendeleza shughuli za ushauri na utafiti.

Waziri Dkt. Nchemba amesema kuwa,shabaha za Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa mabweni manne yenye ghorofa moja moja ambayo yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 400, nyumba nne zenye uwezo wa kuhudumia familia nane za wafanyakazi.

Sambamba na maktaba moja katika kampasi ya Gieta, kuendelea na ukarabati wa miundombinu katika kampasi ya Dar es Salaam na ujenzi wa jengo la taaluma likijumuisha ofisi zenye uwezo wa kuhudumia wahadhiri 40 na madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,520 kwa wakati mmoja katika kampasi ya Mwanza.

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Chuo cha Uhasibu Arusha-IAA kinatarajia kutekeleza yafuatayo, kukamilisha ujenzi wa mabweni manne yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,000 katika kampasi kuu Arusha, kukamilisha ujenzi wa jengo la utawala linalojumuisha madarasa 16, mabweni mawili yenye uwezo wa wakuchukua wanafunzi 1,000 na jengo moja la utawala katika kampasi ya Babati na kufanya mapitio ya mitaala 10,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

IRDP

Waziri Dkt.Nchemba amesema, kwa mwaka 2022/23, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kimepanga kufanya tafiti saba na kutoa huduma za ushauri elekezi kwa kuzingatia mahitaji ya wadau.

Jambo lingine ni kuwezesha mafunzo kwa watumishi 396,kukarabati nyumba 13 za watumishi katika kampasi kuu ya Dodoma na kuendelea na ujenzi wa bweni la wanafunzi na Maktaba katika Kituo cha Mafunzo, Kanda ya Ziwa Mwanza.

TIA

Amesema, katika mwaka 2022/23, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imepanga kujenga jengo moja la utawala katika kampasi ya Misungwi, Mwanza na kampasi ya Kigoma, kujenga ukumbi moja wa mihadhara, maabara ya kompyuta moja na maktaba moja katika Kampasi ya Mbeya.

Waziri amesema, lengo lingine ni kuboresha miundombinu na huduma mtandao (internet service) katika maktaba za kampasi zote.

EASTC

Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, katika mwaka 2022/23, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) kimepanga kuendelea na ujenzi wa jengo la utawala, kuendeleza wahadhiri 28 na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 20.

NBAA

Aidha, amesema katika mwaka 2022/23, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (NBAA) inatarajia kusajili wataalamu 3,500 wa ununuzi na ugavi, kuendesha mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa wataalamu 6,500 na kuendesha mitihani ya kitaaluma kwa watahiniwa 4,000.

Aidha, Bodi ya NBAA inatarajia kusajili wahasibu 1,125 katika ngazi mbalimbali, kuanza ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu jijini Dodoma, kufanya ukaguzi wa ubora wa uandaaji wa taarifa za fedha kwa taasisi 75 na kutoa mafunzo ya diploma ya viwango vya uandaaji wa taarifa za fedha serikalini kwa wahitimu 500.

TRA

Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa,katika mwaka 2022/23, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa Kuhuisha Mkakati wa Muda wa Kati na Mrefu wa Ukusanyaji Mapato; kutunga upya Sheria na Kanuni za Ushuru wa Stempu na Bidhaa; kuanzisha Maabara ya Forodha.
Viongozi na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara uliofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), aliyewasilisha Bungeni Jijini Dodoma, Makadirio ya Mapato na Matumizi ambapo ameliomba Bunge kuiidhinishia Wizara yake Bajeti ya shilingi trilioni 14.94 (sh. tril 13.62 matumizi ya kawaida na sh. tril 1.32 matumizi ya maendeleo), kwa mafungu yake 8 kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Pia kutengeneza na kutekeleza Mfumo Unganifu wa Kusimamia Mapato ya Ndani na kuboresha Kituo cha Udhibiti na Ufuatiliaji wa Mifumo.

Aidha, amesema taasisi za rufaa za kodi zitaendelea kusajili, kusikiliza na kutoa maamuzi ya maombi, mashauri na rufaa za kodi ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.

Michezo ya Kubahatisha

Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa,katika mwaka 2022/23, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha inatarajia kutoa leseni 7,697 kwa waendesha michezo ya kubahatisha, ambapo 1,923 ni leseni mpya na 5,774 ni leseni zitakazohuishwa, kufanya ukaguzi kwa waendesha michezo ya kubahatisha 83.

Sambamba na kufanya mapitio ya Sheria na Kanuni za Michezo ya kubahatisha na kurejesha Bahati Nasibu ya Taifa.

Masoko

Amesema, kwa mwaka 2022/23, Mamlaka ya Mosoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inatarajia kuanza kusimamia masoko ya mitaji kwa kutumia mfumo wa vihatarishi (Risk Based Supervision), kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu masoko ya mitaji, dhamana na bidhaa pamoja na kuongeza idadi ya bidhaa katika soko, hususan hisa, hatifungani na vipande katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

Taasisi za Benki

Waziri Dkt.Nchemba amesema, ili kuchochea na kudhibiti ustawi wa viashiria vya uchumi jumla, Benki Kuu ya Tanzania imepanga katika mwaka 2022/23 kukuza wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ili kuendana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi.

Pia kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kudhibiti na kupunguza kiwango cha mikopo chechefu pamoja na kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa
kipindi kisichopungua miezi minne.

TADB

Amesema, katika mwaka 2022/23, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imepanga kutoa mikopo ya takribani shilingi bilioni 78 kwa sekta ya viwanda, hususan viwanda vya mafuta ya kula na sukari katika mkoa wa Kigoma, Shinyanga na Manyara.

Waziri Dkt.Nchemba anasema kuwa, mikopo hiyo inatarajia kupunguza upungufu wa mafuta ya kula na sukari hapa nchini.

Aidha, amesema benki imepanga kutoa mkopo wa takribani shilingi bilioni 130 kwa ajili ya ununuzi wa pamba na
kahawa.

TIB

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Benki ya TIB imepanga kutoa mikopo ya takribani shilingi bilioni 47 kwa sekta ya viwanda, maji, nishati, madini, mafuta na gesi, huduma na utalii pamoja na kilimo; kukuza mizania ya benki kufikia shilingi billioni 902.63.

"Kupunguza ukwasi kwa kuongeza mtaji wa benki kwa shilingi billioni 373 na kuuza hati fungani zenye thamani ya shilingi billioni 300,"amesema.

TCB

Waziri Dkt.Nchemba amesema kwua, katika mwaka 2022/23, Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imepanga pamoja na mambo mengine kuboresha uwezo wa benki wa kuzalisha mapato ili kufikia shilingi bilioni 185.6.

Pia kukuza faida ya benki kabla ya kodi ili kufikia shilingi bilioni 21.4, kutoa mikopo salama ya shilingi bilioni 709; kukusanya amana za wateja shilingi bilioni 974, kukuza mali za benki ili kufikia shilingi bilioni 1,257 na kukuza
thamani ya hisa na kufikia shilingi bilioni 128.

Taasisi za Bima

Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika mwaka 2022/23, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inatarajia kufanya uchambuzi wa mikataba ya bima mtawanyo kwa kampuni 30 za bima nchini, kufanya ukaguzi wa kampuni 30 za bima, madalali 70, benki wakala 26 na mawakala 278.

Pia kufanya upekuzi wa kina ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kampuni 10, kutoa elimu ya bima kwa watu takribani milioni 1.5 kuhusu huduma za bima na kuhamasisha kampuni za bima kuandaa bidhaa za bima kwenye sekta ya kilimo.

NIC

Amesema Shirika la Taifa la Bima (NIC) linatarajia kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa huduma za bima; kubuni bidhaa mpya nne za bima, kuhamasisha na kufuatilia uandikishaji wa bima kwa taasisi za umma 100 ambazo hazijakata bima na NIC na kuandaa Mfumo wa Usimamizi wa Vihatarishi (Enterprise Risk Management Framework).

Taasisi za Uwekezaji na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

Waziri Dkt.Nchemba amesema kuwa,katika mwaka 2022/23, Kampuni ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS) inatarajia kutekeleza kuongeza rasilimali za mifuko kwa kiwango cha asilimia 15, kuongeza idadi ya wawekezaji kwa asilimia tano.

Sambamba na kuhamasisha taasisi za Serikali, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Mashirika na vikundi mbalimbali vya kijamii kama vile SACCOS kujiunga na mifuko ya UTT AMIS.

SELF

Aidha, Mfuko wa SELF amesema, unatarajia kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya shillingi bilioni 43.5 kwa wajasiriamali 28,255 na kuhakikisha kiwango cha urejeshaji wa mikopo kinafikia asilimia 95 na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa walengwa 4,000.

Usimamizi wa Takwimu Rasmi

"Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inatarajia kuratibu na kuwezesha Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022, kufanya utafiti wa Sekta isiyo rasmi na utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto na kuendelea kutoa takwimu za msingi za uchumi kila mwezi, robo mwaka na nusu mwaka kulingana na aina ya takwimu,"amesema Waziri Dkt.Nchemba.

PPRA

Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika mwaka wa fedha 2022/23,Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) inatarajiakuanza ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu jijini Dodoma na ofisi ya kanda jijini Dar es Salaam.

Pia kuwezesha mafunzo kwa watumishi 940 kutoka katika taasisi nunuzi 170 na wazabuni 1,200 ambao wamejisajili katika mfumo wa TANePS, kufanya mapitio na ujenzi wa mfumo mpya wa usimamizi wa ununuzi wa umma na kufuatilia utekelezaji wa Mikataba ya Ununuzi katika Taasisi Nunuzi 530.

GPSA

Waziri amesema kuwa,katika mwaka 2022/23, Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) unatarajia kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkoa wa Kigoma, kituo cha mafuta katika mikoa ya Njombe, Pwani, Arusha na Wilaya ya Kahama na ujenzi wa ghala katika Wilaya ya Korogwe, Masasi na Dodoma.

Aidha, amesema PPAA imepanga kuandaa mfumo wa kielektroniki wa usajili na usimamizi wa rufaa za ununuzi wa umma na kufanya mapitio ya kanuni za rufaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news