Hope for Girls and Women in Tanzania watumia Maadhimisho ya Serengeti Cultural kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara linatumia maonesho ya Utalii wa Kiutamaduni (Serengeti Cultural Centre) kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya ukeketaji na aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia.
Ambapo maonesho hayo yanafanyika katika Uwanja wa 'Right to Play' uliopo Mugumu wilayani humo yamezinduliwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Mheshimiwa Cosmas Qamara Julai 27, 2022 na yalianza tangu Julai 25, 2022 na yatafungwa Julai 29,2022.

Afisa Mwelimishaji Jamii Kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuely Goodluck amewataka wananchi wilayani humo kusimama kidete kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukeketaji kipindi hiki ambacho wanafunzi watakuwa likizo ambapo koo mbalimbali zimejipanga kukeketa kutokana na mwaka kugawanyika kwa mbili.
Goodluck amesema, jukumu la kutokomeza ukeketaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia zinapaswa kufanywa na kila mtu kwa kutambua madhara yatokanayo na kitendo hicho ambacho Serikali na wadau mbalimbali kwa pamoja wamekuwa wakipiga vita kwani kinawanyima fursa ya kusoma na kufikia ndoto zao.

"Sote tunajua wanafunzi watakuwa likizo. Niwahimize wazazi na walezi na jamii kwa ujumla tuwalinde watoto wa kike kwa juhudi zote, mkiona maandalizi ya binti kukeketwa toeni taarifa mapema polisi, kwenye Shirika la Hope kupitia namba ambazo nimewapa, toeni katika ofisi za Serikali zilizopo jirani kwa haraka zaidi kusudi hatua zichukuliwe na binti aokolewe mapema kabla hajakeketwa. Mwaka huu unagawanyika kwa mbili kwa hiyo koo nyingi zitakeketa na tayari tumeshaona dalili baadhi ya maeneo. 

"Kwa kushirikiana na Serikali, tumejipanga vyema kudhibiti na pia wananchi tupeni ushirikiano wa dhati kusudi watoto wa kike wasikeketwe.

"Na ndio maana tulizunguka tukitoa elimu katika shule takribani 48 za msingi tukishirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ili kufikisha elimu ya madhara ya vitendo hivyo kwa wanafunzi na tukaunda klabu za wanafunzi 'wapinga ukatili,"amesema Goodluck.
"Na pia tunaendelea kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika kata 22 za Serengeti tukishirikiana na polisi lengo ni kuwapa elimu wananchi mtambue kwamba ukeketaji, ndoa za utotoni hazifai na ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu lazima tuelewe hivyo niwaombe kwa pia kwa kuwa mmefika katika banda na tumeelimishana madhara nendeni mkawe mabalozi kwa wenzenu ambao hawajafika hapa,"amesema Goodluck.

Elizabeth Hosea ni mkazi wa Mugumu amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ambapo amesema kuwa, itachochea ushiriki wa kila mwananchi wilayani humo kuunga mkono juhudi za kumaliza vitendo hivyo. Huku akiomba adhabu kali zitolewe kwa wanaokutwa na hatia kuwakeketa mabinti.

"Wapo wazee wa kimila niwaombe waendelee kukomesha ukeketaji wao wakiongea kwa kutoa makatazo wanaaminika sana katika koo zao. Waunge mkono juhudi za serikali ili watoto wetu wa kike wasome na kuwa viongozi bora wa baadaye watakaoleta manufaa kwa taifa kiuchumi na kijamii kama tunavyomuona Rais wetu Mheshimiwa Samia Hassan akililetea taifa letu maendeleo makubwa kutokana na kupewa fursa ya elimu na kujengewa msingi bora na wazazi wake,"amesema Elizabeth.

"Nimshukuru Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly amezidi kusimama kwa ushupavu kupitia shirika analoliongoza kupambana na ukatili ambazo nyumba salama Kituo cha Hope Mugumu kinatoa hifadhi kwa mabinti wanaokimbia makwao kukwepa ukeketaji na pia amekuwa akiwaendeleza kielimu huu ni upendo mkubwa sana. Lazima aungwe mkono katika kuhakikisha kwamba ukeketaji na mila mbaya zinaachwa,"amesema Jesca Marwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara akizungunza akiwa katika banda la Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutokomeza ukeketaji wilayani humo. Huku akiwataka wananchi kutokeketa wasichana bali wajikite kuwasomesha na kuwapatia haki zao kusudi watimize ndoto zao katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Pia, Mheshimiwa Qamara amewataka wazazi na walezi wilayani Serengeti kuwafanyia tohara salama watoto wa kiume badala ya kuwafanyia tohara isiyo salama ambayo ina madhara makubwa kiafya huku akisisitiza kwamba serikali haitwafumbia macho watakaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Akizungumzia maonesho hayo ya 'Serengeti Cultural Centre', Kamara amewataka waandaji wa maonesho hayo kwa mwakani kuyaboresha yaweze kushirikisha wageni kutoka sehemu mbalimbali na nje ya nchi kwa kuweka mikakati thabiti katika kuendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
"Mikakati ya maonesho haya kwa mwakani tuanze mapema, mwakani maonesho haya yawe mazuri hata tukimwalika Mheshimiwa Waziri ayakute yakiwa kwenye ubora unaotakiwa. 

"Kuanzia Oktoba mpango kazi wetu lazima tukutane tuanze maandalizi mapema, fursa kama hii ya kutangaza tunatangazaje, kama hatutakuwa na mipango bora kuonesha bidhaa zetu? Na mimi nitakuwa sehemu ya maandalizi ya maonesho haya ya Utalii wa Kiutamaduni,"amesema Kamara.

Post a Comment

0 Comments