Huyu ndiye Mwafrika aliyetimuliwa New Africa Hotel Dar, ukifika Kariakoo lazima usikie Mtaa wa Aggrey

NA DIRAMAKINI

BILA ubishi, mmoja wa watu mashuhuri katika historia ya Waafrika na Wamarekani wenye asili ya Kiafrika ni Dkt. James Emmanuel Kwegyir Aggrey, anayejulikana kama Aggrey wa Africa.

Sio tu Afrika inaweza kumdai, bali pia Diaspora ya Afrika. Aggrey alizaliwa Oktoba 18, 1875, huko Anomabo nchini Gold Coast (sasa Ghana) na Princess Abena Anowa na Okyeame Prince Kodwo Kwegyir.

Aggrey akawa mmishonari aliyekamilika, mwalimu, Mwana majumui wa Afrika, na msomi wa umma. Alipata elimu yake ya awali huko Gold Coast.

Mnamo 1898, Aggrey alisafiri kwa meli hadi Marekani ili kujengewa uwezo kuwa mmishonari. Alihudhuria Chuo cha Livingstone, HBCU cha kibinafsi, huko Salisbury, North Carolina.

Alihitimu mwaka 1902 na kupata digrii tatu za kitaaluma. Aggrey alikuwa anajua kuzizungumza na kuandika lugha mbalimbali kutoka Ghana na Ulaya kwa ufasaha.

Mwaka 1903 Aggrey alitawazwa kuwa mhudumu katika Kanisa la African Methodist Episcopal Zion Church. Alimuoa Rosebud (Rose) Douglas, mwanamke Mwafrika kutoka Virginia, mwaka 1905.

Wanandoa hao walikuwa na watoto wanne akiwemo Abna Azalea Aggrey, Kwegyir Aggrey, Rosebud Douglass Aggrey, na Orison Rudolph Aggrey ambaye baadaye alikuja kuwa Balozi wa Marekani nchini Senegal na Gambia na baadaye Romania.

James Aggrey alipata shahada yake ya udaktari katika Theolojia mwaka 1912, ikifuatiwa na ya Osteopathy (ubobezi katika sayansi ya tiba mbadala) mwaka 1914, aliendelea na masomo zaidi katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Alihudumu katika Kitivo na Utawala katika Chuo cha Livingstone kwa miongo miwili. Katika kipindi hicho kama sehemu ya Tume ya Phelps-Stokes kwa Afrika, Aggrey alitembelea nchi mbalimbali mwaka 1921.

Katika ziara zote hizo rasmi alisisitiza umuhimu wa elimu kwa viongozi wa Afrika. Huko Gold Coast, Aggrey alimshawishi Gavana wa Mkoloni wa Uingereza, Gordon Guggisberg kwamba Chuo cha Achimota (hapo awali kilikuwa Chuo cha Prince of Wales) kinapaswa kujikita katika elimu.

Akiwa katika ziara hizo, Dkt.Aggrey alikumbana na ubaguzi wa rangi Afrika, hivyo miaka hiyo alitoa hotuba Afrika Kusini kuhusu uwiano wa rangi akisema;

“Funguo nyeusi za piano hutoa sauti nzuri na funguo nyeupe hutoa sauti nzuri, lakini mchanganyiko wa hizo mbili hutoa sauti bora zaidi.Waafrika wabaki kuwa Waafrika wazuri na sio wakala duni wa Wazungu."

Mnamo 1924, Aggrey alijiunga na Tume nyingine ya Phelps-Stokes kwa Afrika, alianzisha Shule ya Achimota huko Gold Coast mwaka 1924 na alihudumu kama Makamu Mkuu wake kutoka 1925 hadi 1927. Alirudi Marekani mnamo Mei 1927 kuhubiri, kufundisha na kukamilisha kitabu katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Miongoni mwa nchi alizotembelea ni Uganda, Kenya, Tanganyika, Malawi na Msumbiji. Katika nchi hizo alikuwa akihamasisha zianze kudai uhuru wao, alifika Tanganyika na kuitembelea Zanzibar.

Ni wazi kuwa, Dkt.Aggrey ameacha historia kubwa barani Afrika ikiwemo Tanzania. Katika maisha yake alikumbana na kila aina ya ubaguzi toka kwa Wazungu.

Mfano akiwa Tanganyika (kwa sasa Tanzania) alikumbana na ubaguzi mkubwa wa rangi katika hoteli ya New Africa Hotel (kwa sasa Four Points by Sheraton Dar es Salaam) iliyopo maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam ambayo ilijengwa na Wajerumani baada ya kukabidhiwa Tanganyika kufuatia Mkutano wa Berlin mwaka 1884 hadi 85.

Enzi za ukoloni wa Mjerumani na Mwingereza, ilikuwa ni marufuku kwa Mwafrika kukanyaga hotelini hapo labda tu kwa kibali maalum au kama ni mfanyakazi wa hoteli hiyo.

Marehemu Dkt.Aggrey alikuja Tanganyika mwaka 1924 kama Mjumbe wa Phelps-Stokes Fund Commission kuja kuangalia jinsi ya kuwaendeleza Waafrika kielimu.

Katika tume hiyo,alikuwa Mwafrika pekee kwenye baada ya kuundwa na Carolyne Phelps Stokes, ambaye alifariki mwaka1909 na kuacha fedha nyingi na kuacha usia uliosema, "I bequeath the same to My trustees to be used for the education of Negros, both in Africa and the United States, North American Indian and needy and deserving white students".

Ni kutokana na wosia huu ndipo ilipoundwa tume hiyo ambayo ilizuru mataifa kadhaa ya ya Afrika ambapo ujumbe ulifika Tanganyika na Zanzibar toka Machi 1924 hadi April 1924.

Baada ya ujumbe wa tume hiyo kuwasili jijini Dar es Salaam, wajumbe waliamua kufikia New Africa Hotel ambayo ilikuwa moja ya hoteli chache kubwa na ya kuheshimika nchini wakati huo.

Katika hali ya kusikitisha,Dkt.Aggrey akiwa Mwafrika pekee katika tume hiyo, alikataliwa kupewa chumba katika hoteli hiyo huku sababu kuu ikiwa ni kutokana na asili yake (Mwafrika).

Uamuzi huo, ulimpa siamnzi, lakini hakukata tamaa na akaendelea na harakati zake za kuwasaidia Waafrika wenzake kwa kadri alivyoweza.

Aidha, baada ya kukataliwa chumba, ilimbidi atafute chumba kwenye hoteli nyingine ambapo akiwa jijini Dar es Salaam aliwashawishi akina Cesil Matola, Kleist Syekes kuunda chama ili iwe rahisi kupigania haki zao kwa pamoja kama Waafrika.

Kwa kuwa, Kleist alikuwa kijana msomi mwenye kuzungumza Kijerumani na Kiingereza fasaha alichukua muda, na kuamua kufanya uamuzi wa kuunda chama African Association (AA) mwaka 1929 kwa lengo la kuwapigania Waafrika.

Aidha, AA baadae ilibadilishwa na kuwa Tanganyika African Association (TAA) mwaka 1948 hadi kuwa chimbuko la Tanganyika African National Union (TANU) mwaka 1954. Kutokana na mchango mkubwa wa mawazo na juhudi za Dkt.Aggrey ndipo Waafrika wakaona si mbaya kuendelea kumuenzi, kwa hapa Tanzania, alipewa Mtaa wa Agrey jijini Dar es Salaam kwa heshima yake.

Dkt.James Emmanuel Kwegyir Aggrey aliugua kutokana na maradhi yaliyomkabili na akafariki Julai 30, 1927 akiwa na umri wa miaka 52.

Urithi wake unajumuisha heshima nyingi alizopewa yeye na mkewe Rose aliyefariki mwaka 1961.Dkt.James E Kwegyr Agrey, msomi na mzaliwa wa Ghana ambaye alisoma Ghana na Marekani,pia alifanya kazi huko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news