Serikali yaridhishwa na ujenzi ofisi ya DC wa Mkalama

NA FRED KIBANO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameridhishwa na ujenzi wa jengo na ubora wake Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkalama mkoani Singida lililojengwa na Wakala wa Majengo (TBA) baada ya kulizindua likiwa limekamilika kwa asilimia 100. 
 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi hiyo kutawaletea wananchi huduma karibu kwani awali wananchi walikuwa wakiipata huduma ya utawala katika Wilaya jirani ya Iramba.
Aidha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa agizo kwa watumishi kuacha kukaa ofisini siku zote za wiki na badala yake watenge siku tatu kati ya sita kwenda vijijini kuwaelimisha wananchi kuhusu mambo yanayofanywa na Serikali pamoja na kupokea kero zao na kuzifanyia kazi.

“Mkurugenzi hili ulichukue, kuanzia sasa watumishi wasikae ofisini wiki nzima, waende vijijini kukutana na wananchi kwa wiki yenye siku sita, siku tatu zote waende vijijini kukutana na wananchi kuwaelimisha nini Serikali inafanya na itafanya nini na wasikilize changamoto zao na kuzifanyia kazi,” alisema Mhe. Majaliwa.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Mradi wa jengo la Mkuu wa Wilaya Mkalama Meneja Ujenzi Wakala wa Majengo (TBA) Mhandisi Khadija Salum Abdala amesema mradi wa jengo hilo unajumla ya thamani ya shilingi bilioni 1.3 lakini mpaka sasa jumla ya shilingi Bilioni 1.2 zimetumika na kukamilisha mradi huo kwa asilimia 100.

Aidha, Mhandisi Khadija Salum Abdala amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 2018, lina jumla ya Ofisi 19 na ukumbi wa mikutano unaoweza kuchukua takribani watu 100, majiko mawili, stoo ya kutunza kumbukumbu na pia miundombinu yake imezingatia watu wenye mahitaji maalum ambapo moja ya faida yake itakuwa ni kutoa huduma kwa wananchi.

Awali akitoa maelezo yake Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Isack Mtinga ameishukuru Serikali kwa kuwapatia miradi mbalimbali kwani kwa kipindi chake tu Wilaya imepokea shilingi Bilioni mbili za barabara lakini pia ameiomba Serikali kuwajengea barabara ya Mkalama hadi Iguguno kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 42 ili kusaidia shughuli za kiuchumi wilayani humo na mikoa ya jirani.

Akitoa salamu za Wizara kuhusu kazi za Serikali zilizofanyika Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema, katika sekta ya afya pekee Wilaya ya Mkalama kwa baadhi ya miradi imepokea shilingi Bilioni 2.3 kwa hospitali ya Wilaya, milioni 300 ujenzi wa jengo la Dharura, milioni 350 kwa ajili ya vifaa tiba na mashine ya mionzi na pia jumla ya watumishi 20 wa kada ya afya wameajiliwa Wilayani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news