Waziri Bashungwa azindua 'Mwalimu Special' huku akitoa maelekezo kwao

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa walimu wote nchini kujiwekea malengo binafsi katika masomo wanayofundisha na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa.
Bashungwa ameyasema hayo leo Julai 18, 2022 katika warsha ya kutambua maboresho na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya walimu na benki ya NMB iliyofanyika wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Katika warsha hiyo, Waziri Bashungwa amezindua programu maalumu ya walimu inayojulikana kama 'Mwalimu Special'.

Pia amekabidhiwa madawati 111 kwa ajili ya kupunguza uhaba wa mdawati shuleni ndani ya Halmashauri ya Wilaya Karagwe.

“Viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya shule, kata, halmashauri na mikoa mjiwekee malengo yenu na kujisimamia ili kuhakikisha wanafunzi wote kwenye eneo wanaloliongoza wanapata umahiri uliokusudiwa kwa masomo yote kila mwaka," amesema Bashungwa.

Ameagiza kila kiongozi wa elimu katika ngazi ya shule, kata, halmashauri na mikoa afuatilie ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kushauriana na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa kwa masomo yote, badala ya kukaa ofisini.

Aidha, Bashungwa amesema wa mwaka wa fedha wa 2022/23, Mkoa wa Kagera kupitia mradi wa SEQUIP umetengewa Sh bilioni 5.79 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, shule mpya za sekondari katika kata zisizo na shule.

Hata hivyo, Waziri Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha 2021/22, Mkoa wa Kagera kupitia mradi huo umepokea fedha kiasi cha Sh bilioni 7.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari za kata na mkoa.

Naye Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikalini wa NMB, Bi. Vick Bishubo amesema, programu ya mwalimu special itatoa fursa kwa walimu kupata mikopo ya vitendea kazi mfano pikipiki, elimu ya kifedha na ujasiriamali, bima, fursa za ajira kupitia programu ya uongozi na elimu huhusu huduma za kidigitali za NMB.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news