Siku Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair alipokalia kaa la moto baada ya kuunga mkono vita nchini Iraq

NA CHARLES REGESIAN

LILIKUWA jambo la kushangaza Dunia pale Marekani na washirika wake walipoamua kuivamia Iraq kijeshi mwaka 2003.

Mshangao ulitokana na ukweli kwamba wakati Marekani inaingia vitani dhidi ya Iraq, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikuwahi kuridhia mpango huo.

Hii basi itoshe kusema kwamba aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo ,George Bush alikuwa na ajenda binafsi kuhusu vita hiyo.

Katika maelezo ya awali Bush aliitangazia Dunia kwamba Iraq haikuwa salama kwa sababu mtawala wake,Saddam Hussein alikuwa akimiliki silaha za maangamizi kwa kauli yake hiyo akafanikiwa kuihadaa Dunia kwamba Saddam alikuwa anamiliki silaha hizo.

Uingereza chini ya Waziri Mkuu Tony Blair, nayo ikaunga mkono hoja ya kuivamia Iraq kijeshi na hivyo kupeleka maelfu ya wanajeshi nchini humo. 

Kilichofuata baadaye ni kasoro kibao kuhusu mpango mzima wa vita hiyo, ikaja kubainika kwamba Saddam hakuwa na silaha hizo,hivyo hoja ya kwamba anavamiwa kuhusu silaha ikakosa mashiko.

Lakini kwa vile dhamira ilikuwa ni kumwangamiza Saddam, wababe hao wa Dunia wakaleta hoja nyingine kwamba Saddam alikuwa na ushirika na mtandao wa Al Qaeda unaoratibiwa na Osama Bin Laden. 

Hizo zote zikawa ni propaganda ambazo kimsingi leo hii zinawaweka pabaya Bush na mshirika wake Blair. 

Wapo wanaodhani pia kuwa si ajabu Bush aliamua kumvaa Saddam na kufuta utawala wake kulipa kisasi cha vita ya Ghuba ya mwaka 1991 ambayo baba yake George H. W. Bush alishindwa.

Vita ya Iraq iligeuka na kuwa shubiri kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair ambaye alilaumiwa kwa kuridhia kupeleka majeshi nchini humo, Waingereza walichachamaa na kudai kuwa kitendo kilichofanywa na Blair wakati huo ni cha kipuuzi kabisa,siku chache baada ya Blair kujitetea kuhusu kuingia katika vita hiyo, Waziri wa zamani katika Serikali yake,Clare Short alimwita bosi wake huyo wa zamani kuwa ni mpuuzi asiyejua kujenga hoja.

Blair aliwahi kusema kuwa, alipeleka majeshi Iraq kwa vile aliamini kuwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11, mwaka 2001 kulikuwa na uwezekano wa magaidi kuwa washirika wa Iraq. 

Lakini kwa mujibu wa Short, kama suala hilo lilikuwa na tija kwa Uingereza kwa nini aliyekuwa Waziri wa Fedha,Gordon Brown hakuhusishwa nalo?.

Kutokana na hilo Short, alisema kwamba, Blair alikuwa na lake jambo katika msimamo wa kuivamia Iraq kijeshi, ndipo alipoamua kuachia ngazi mwaka 2003 ili asiwe miongoni mwa viongozi katika Serikali ya Blair. 

Blair alisisitiza kuwa Saddam alikuwa tishio katika Mashariki ya Kati na kwamba njia pekee ilikuwa ni kumdhoofisha kama walivyofanya,hata hivyo hoja hiyo bado ni dhaifu.

Utetezi wake kwamba Saddam alikuwa na ushirika na Osama bin Laden nao ni danganya toto, kwani katika kipindi hicho, wawili hao hawakuwa na uhusiano wowote wa kufanya jambo katika msimamo wa pamoja. 

Hii ni kusema kwamba kauli tata alizotoa Blair kwa kipindi kile ni matapishi ambayo daima yataendelea kumchafua,Waingereza hawakutaka majeshi yao yaendelee kuwepo nchini Iraq.

Mwaka 2007 Blair alihitimisha uwaziri Mkuu wake wa Uingereza aliodumu nao kwa miaka 10 kofia ya uwaziri mkuu aliiachia Juni 7, mwaka 2007. 

Siku tatu baada ya kuachia madaraka ya Chama cha Labour. Blair aliingia madarakani Mei mwaka 1997 akiweka historia mpya katika siasa za Uingereza baada ya kufanikiwa kukiangusha Chama cha Conservative kilichokuwa kikiongozwa na John Mayor.

Kabla ya kukibwaga Chama cha Conservative, Blair alishaanza kuwa tishio katika siasa. 

Katika mkutano Mkuu wa Labour mwaka mmoja kabla ya kuingia madarakani,Blair aliahidi vitu vitatu akavitaja kuwa ni elimu,elimu na elimu. 

kauli mbiu hiyo ikazidi kumpa wafuasi wengi ambao Kimsingi walishamchoka Mayor, na chama chake na kutokana na ushawishi mkubwa aliokuwa nao akafanikiwa kuingia ofisini na kuweka historia nyingine ya kuwa mtawala mdogo katika cheo hicho nchini Uingereza akiwa na umri wa miaka 44.

Kushinda kwa Labour katika uchaguzi huo kulihitimisha miaka 18 ya utawala wa Conservative na hayo yalikuwa matokeo mabaya kwa chama hicho tangu mwaka 1832. 

Blair alipoingia madarakani aliachana na sera za kizamani zilizofuatwa na waliomtangulia. 

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Uingereza kupata Waziri Mkuu mwenye umri mdogo baada ya Lord Liverpool mwaka 1812.

Blair aliukwaa uwaziri mkuu huo miaka mitatu baada ya kuchaguliwa kukiongoza Chama cha Labour akichukua nafasi ya John Smith aliyefariki dunia ghafla. 

Blair alikuwa Waziri Mkuu pekee wa Chama cha Labour aliyekalia nafasi hiyo kwa muda mrefu. Alishinda kwa kishindo chaguzi tatu za kuwania nafasi hiyo.Mei 10 mwaka 2007 aliwaambia wapiga kura wake katika jimbo lake la uwakilishi la Sedgefield kwamba hana nia tena ya kuendelea na nafasi yake.

Blair alizaliwa Mei 6 mwaka 1953 Edinburgh, Scotland anatajwa kuwa mmoja wa wanasiasa aliyeondoka madarakani akiwa na mzigo mkubwa wa lawama mgongoni. 

Kikubwa kilichomtafuna Blair ni msimamo wake juu ya vita ya Iraq, raia wa kawaida na viongozi wa vyama vya upinzani hawajaacha kusema kuwa lilikuwa kosa kubwa sana kwa Blair kuunga mkono vita ya Marekani nchini Iraq.

Lakini hakuwa na namna ya kulikwepa hilo kwani Blair ni rafiki wa karibu na aliyekuwa Rais Bush wa Marekani aliyeanzisha vita dhidi ya iraq mwaka 2003. 

Bush aliingiza majeshi yake nchini Iraq kwa mabavu akikosa ridhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kuridhia kwake kuingia katika vita hiyo kulimweka Blair sehemu mbaya kisiasa kwani wanaharakati wengi walishinikiza kuachana na mpango huo.

Hata hivyo, Blair aliyejiunga na Chama cha Labour baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Oxford mwaka 1995 alikuwa akitetea uamuzi wake wa kuingia vitani. Alisisitiza kuwa vita ilikuwa haikwepeki kwa vile Saddam alikuwa mhimili wa ugaidi.

Wakati fulani mwaka 1984 alipokuwa msemaji wa masuala ya fedha katika kambi ya upinzani alionesha ukali wa hali ya juu dhidi ya Benki ya England. 

Kila alipopata nafasi ya kusema alionesha kuumizwa na mfumo aliouita mbovu katika Serikali ya Uingereza. Haishangazi kumuona Blair akiendelea kutetea takataka zake kwa sababu ana sifa kubwa ya kujibu maswali ya papo kwa hapo.

Kiongozi huyo licha ya kupitia pingamizi mbalimbali za kisiasa anabaki kuwa aliyefanikiwa kuchezesha siasa kwa uwezo wa hali ya juu. 

Hilo halina ubishi kwani katika chaguzi tatu aliibuka kidedea na hivyo kuwaacha wapinzani wake midomo wazi. Alifanikiwa pia kuongeza mapato kwa Uingereza na kuinua nafasi za ajira kwa watu wake huku akiunga mkono vita dhidi ya ugaidi.

Kama ilivyosemwa awali Blair alipakwa matope kwa uhusiano wake na George Bush, wengi hawakupenda alivyofuata Sera za Marekani katika Mashariki ya Kati,hasa suala la mgogoro kati ya Israe-Lebanon na Israeli-Palestina,hata hivyo alijitahidi kujenga urafiki na mataifa mbalimbali na alikuwa nguzo kuu katika ongezeko la wanachama wa Umoja wa Ulaya kutoka 15-27.

Aliweka uhusiano mwema na watawala wa duniani kama vile Silvio Berlusconi wa Italia, Angela Merkel wa Ujerumani na Nicolas Sarkozy wa Ufaransa. 

Kwa ufupi huyo ndiye Blair Baba wa watoto wanne Euan, Nicky,Kathryn na Leo. Alifunga pingu za maisha na Cherie Booth, Machi 19 mwaka 1980.

Katika ngazi ya kifamilia Blair ni Waziri Mkuu pekee kupata mtoto halali wa ndoa akiwa madarakani katika Serikali ya Uingereza baada ya kupita miaka 150, mtoto huyo ni Leo, aliyezaliwa Mei 20 mwaka 2000 mwingine alikuwa mtoto wa Lord John aliyemzaa Francis Russell Julai 11, mwaka 1849.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news