Simbaya avaa viatu vya Karsan ukurugenzi UTPC

NA DIRAMAKINI

MKUTANO wa mashauriano kati ya Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) na SIDA umeanza leo mkoani Dodoma, ambapo viongozi mbalimbali wa klabu wamehudhuria wakiwemo wawakilishi kutoka Sida.
Mkutano huu, umefunguliwa rasmi na Rais wa UTPC, Bw. Deo Nsokolo ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi, ametangaza rasmi kupatikana kwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa UTPC ambaye ni Bw. Kenneth Simbaya.

Pamoja na mambo mengine, Nsokolo ameishukuru Sida kwa kuendelea kuisaidia tasnia ya habari nchini kupitia UTPC kwani Sida wamekubali kuifadhili tena UTPC kwa muda wa miaka mitatu.

Ameongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho UTPC inapita kwenye mabadiliko makubwa ya uongozi, inahitaji ushirikiano mkubwa baina ya viongozi wa UTPC na wanachama wake.

Pia alimshukuru sana Mkurugenzi anayemaliza muda wake Bw. Abubakar Karsan kwa weledi na umahiri kuitumikia UTPC na wanachama wake kwa uadilifu mkubwa.

Deo Nsokolo amemaliza hotuba yake kwa kumkaribisha Mkurugenzi mpya wa UTPC, Bw. Kenneth Simbaya na kuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha malengo yote yaliyopangwa.

Hivi karibuni, baada ya kuutumikia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) kwa zaidi ya miaka 19 kama mkurugenzi mtendaji, Abubakar Karsan alitangaza rasmi kustaafu kuitumikia taasisi hiyo.
Karsan ameitumikia taasisi hiyo kama Mkurugenzi mtendaji toka mwaka 2003, ambapo alisema atastaafu rasmi kuitumikia UTPC ambayo ameeleza imekuwa taasisi imara na kubwa nchini.

Akifungua mkutano wa kupitia kanuni za maadili ya vyombo vya habari mtandaoni jijini Mwanza hivi karibuni, Karsan alitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari na kubainisha kuwa, ameamua kwa hiari yeye mwenyewe kustaafu.
“Toka mwaka jana niliomba mimi mwenyewe kwenye bodi ya wakurugenzi nistaafu, nikapumzike na niweze kuwaachia vijana, lakini bodi ilikataa wakaniomba niendelee mwaka mmoja hadi mwaka 2022,” alisema Karsan.

“Niliwakubalia bodi na sasa ule mwaka mmoja utamalizika mwezi Desemba, mwaka huu, nami nakwenda kupumzika ili niwaachie wengine waweze kuendeleza taasisi hii,”alieleza Karsan.
Alisema kuwa, tangu kuanzishwa kwa UTPC wamepitia changamoto nyingi sana, ambazo zimefanya taasisi hiyo kusimama na kuwa imara zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news