WAZIRI BITEKO:TANZANIA KUWA KITOVU CHA BIASHARA YA MADINI

NA STEVEN NYAMITI-WM

SERIKALI imepanga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini kwa kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza katika sekta hiyo na kufungua fursa nyingi za kuchimba madini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko alipokutana na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini leo Julai 20, 2022 mkoani Kigoma ili kujadili mambo mbalimbali katika uchimbaji wa madini.

Dkt.Biteko amesema, mataifa mengi yanakuja nchini kujifunza kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini na hasa sekta ndogo ya wachimbaji wadogo.

Amesema, Serikali imeendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji katika Sekta ya Madini kuweza kuwekeza katika uchimbaji wa madini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara hiyo.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan wachimbaji wadogo wapo kwenye moyo wake, tena anawaita wachimbaji wangu wadogo, anawapenda na kuwathamini sana, anatamani kuona changamoto walizonazo wachimbaji hao kote nchini zinamalizwa kwa haraka," amesema.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa, Sekta ya Madini ina wajibu wa kutoa ajira kwa Watanzania, kukuza uchumi wa nchi na kujenga utajiri na kuwaondolea umaskini watu.
Amesema, changamoto ya soko kuu la madini la mkoa linaloendelea kujengwa Serikali itakamilisha ujenzi wa soko ili watu wengi waweze kuleta madini yao kuuzwa Kigoma hususan nchi za jirani.

Kuhusu mikopo kwa wachimbaji wa madini, Dkt.Biteko amesema Serikali imefanya kazi kubwa kuzungumza na taasisi za kifedha ili yaanze kukopesha wachimbaji wadogo na tayari taasisi hizo zinatoa mikopo kwa wachimbaji.

"Serikali itaendelea kufanya utafiti kwenye maeneo yanapochimbwa madini nchini ili wachimbe na kupata manufaa,"ameongeza. 
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe.Thobias Andengenye amewapongeza wachimbaji wa mkoa wa kufanya kazi na kuendelea kuutangaza mkoa kwa uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Kigoma, Lister Balegele amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha uchimbaji madini wenye viwango vya kutoa tija katika soko la ndani na nje ya nchi na kudhibiti uchimbaji holela wa madini usiofutata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Naye, Afisa Madini Mkazi wa Kigoma Mhandisi Pius Lobe amesema, mkoa wa Kigoma una jumla ya leseni 429 za uchimbaji mdogo wa madini, leseni mbili za uchimbaji wa kati wa madini, leseni tisa za utafutaji mkubwa wa madini, leseni nane za biashara ndogo ya madini na leseni 11za biashara kubwa ya madini.

Mkoa wa Kigoma una aina mbalimbali za madini katika maeneo mbalimbali ikiwemo madini ya ujenzi, madini ya metali,viwandani na ya vito.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news