Waziri Mkuu:Tunataka kuona miradi inayotokana na makusanyo ya ndani

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam na ya wilaya ya Kinondoni ambapo pamoja na mambo mengine ameagiza makusanyo ya fedha za ndani yatumike katika ujenzi wa miradi ya maendeleo badala ya kutegemea fedha zinazotoka Serikali Kuu pekee. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa kingo za Mto Ng’ombe na mfereji wa kiboko katika eneo la Tandale kwa Mtogole Mkoani Dar es salaam akiwa katika ziara ya wilaya ya Kinondoni, Julai 11, 2022. Kushoto kwake ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge na kushoto ni Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Mwaka 2020/2021 mlikusanya zaidi ya shilingi bilioni 40, pamoja na makusanyo hayo makubwa lakini hatuoni mradi mkubwa unaotekelezwa kupitia fedha hizo. Makusanyo ya mapato na matumizi yasimamiwe vizuri na fedha hizo zitumike katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.” 

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Julai 11, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na wa wilaya ya Kinondoni katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Dar Es Salaam. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Mwenge Mkoani Dar es salaam akiwa katika ziara ya wilaya ya Kinondoni, Julai 11, 2022. Kulia ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge na watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar esalaam, Amos Mkala. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 

Katika ziara hiyo yenye lengo la kukutana na viongozi na watumishi wa umma mkoani Dar Es Salaam ili kuwakumbusha wajibu wao na kuwahamasisha kufanya kazi wa bidii, Waziri Mkuu amewasisitiza wasimamie vizuri maeneo yao na wafanye kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Sinza/Ng’ombe na Mfereji wa Kiboko katika eneo la Mtogole ambapo amewataka wananchi wa maeneo hayo kutunza mazingira na wahakikishe hawamwagi taka ndani ya mfereji huo. 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Kinondoni ufanye maboresho ya mradi huo kwa kujenga madaraja madogo madogo yatakayowezesha mtu kutoka upande mmoja wa mto kwenda mwingine, pamoja na kuweka taa katika barabara hiyo. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Mwenge Mkoani Dar es salaam akiwa katika ziara ya wilaya ya Kinondoni, Julai 11, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 

Baada ya kukagua mradi huo, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa soko la wamachinga katika eneo la Mwenge pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Manispaa ya Kinondoni. 

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa ambaye ameambatana na Waziri Mkuu katika ziara hiyo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba TAMISEMI kwa kushirikiana na viongozi wa mkoa huo watahakikisha maelekezo aliyoyatoa wanayafanyia kazi. 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Amos Makala alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za jamii ikiwemo ya afya na elimu. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Mwenge Mkoani Dar es salaam akiwa katika ziara ya wilaya ya Kinondoni, Julai 11, 2022. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makala. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 

“Mkoa umepokea jumla ya shilingi bilioni 4.5 zinazotokana na tozo ya miamala ya simu kwa ajili ya kuendeleza miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya, fedha hizi zimegharamia ujenzi wa majengo mapya ya wagonjwa wa nje na zahanati, upanuzi wa miundmbinu ya zahanati na vituo vya afya” .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news