CCWWT yampongeza Rais Samia kwa kuwaheshimisha wajane nchini

NA DIRAMAKINI

CHAMA Cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) kimeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuliona kundi la wajane kwa jicho la pekee hasa baada ya kuundwa wizara ambayo pamoja na mambo mengine, kundi la wajane limetajwa kama sehemu ya kusimamiwa na wizara hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa chama hicho, Bi.Rabia Ally Moyo na Katibu wa chama, Bi.Sabrina Tenganamba wakati wa uzinduzi wa chama hicho mkoani Mbeya ambapo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.Dorothy Gwajima alishiriki.

"Mhe. Waziri sisi tumefarijika sana na ujio wako hapa na kuongea na sisi wanawake wajane na kula chakula pamoja nasi, tunaahidi kukupa ushirikiano wetu na yote uliyoyaelekeza tutayatekeleza ikiwepo kuundwa uongozi wa wajane kwa mikoa yote,"alisema Katibu wa chama hicho,Bi.Sabrina Tenganamba huku akisema kwa sasa chama hicho kimefika mikoa nane na kinatarajia kusambaa nchini kote.

Dkt.Gwajima katika hafla hiyo amewataka wanawake wajane wawe na uongozi ngazi zote ili waweze kukusanya changamoto zao kwa kila ngazi husika kisha zijumuishwe ili Serikali ione ni zipi za kushughulikiwa ngazi husika na zile za Kitaifa zifikishwe ngazi hiyo.

Waziri Dkt.Gwajima ametoa wito huo Agosti 8, 2022 jijini Mbeya alipofika kuwatembelea wajane wa Kata za Iganzo na Isanga na kula pamoja nao chakula cha jioni.

Pia amewaagiza maafisa ustawi na maendeleo ya jamii washirikiane na chama hicho ili kuweza kuharakisha zoezi hilo.

"Nimesikiliza risala yenu, hivyo, niwatake kwanza muunde na kusimika uongozi wa ngazi zote na baada ya hapo mshirikiane na maafisa ustawi na maendeleo kuainisha changamoto zenu,"amesema Waziri Dkt Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amewaambia wanawake hao kuwa, Mhe.Samia Suluhu Hassan ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameandaa mambo mazuri kwa ajili ya wanawake wa Tanzania wakiwemo wajane hivyo ni wajibu wa wao kuwa na utayari wa kuandaa mipango yenye tija.

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Gwajima, amewaagiza Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii kuwafikia wajane hao na kuwasiliza kisha kuainisha matatizo mbalimbali yanayowakabili na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Awali akimkaribisha Waziri ili azungumze na wajane hao, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Amina Mfaki alisema Serikali imeendelea kuwa na mipango mizuri dhidi yao ikiwepo mnikopo ya asilimia 10, hivyo akawataka kujiunga katika vikundi na wawasilishe maombi yao kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Wakati huo huo, Katibu wa chama hicho amesema kuwa, uundwaji wa chama hicho umelenga kuwaunganisha wanawake wote wajane nchini ili kurahisisha kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake wajane hasa zile za kisheria.

“’Wanawake wajane wengi wetu wanakabiliwa na changamoto kubwa katika familia zao ikiwemo ya kunyang’anywa mali na kunyanyapaliwa hivyo chama hiki kitakuwa na jukumu hilo la kuangalia chamgamoto hizo na kuzikabili,”alisema.

Bi.Tenganamba alisema,wajane wengi wamekuwa wakifariki kutokana na changamoto mbalimbali hasa ya msongo wa mawazo baada ya kupitia manyanyaso mengi na kuishi maisha magumu ukilinganisha na alipokuwa akiishi na mmewe kabla ya kufariki.

Post a Comment

0 Comments