DC Mkasaba awapongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu Sensa inayoendelea nchini

NA DIRAMAKINI

WANANCHI wa Wilaya ya Kusini Unguja wamepongezwa kwa mwitikio wao mkubwa wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi pamoja na ushirikiano wanaotoa kwa Makarani wa zoezi hilo linaloendelea nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Rajab Yussuf Mkasaba ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipofanya ziara ya kuangalia harakati za zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linavyoendelea katika Shehia mbalimbali za wilaya hiyo.

Katika ziara yake hiyo, Mkuu wa Wilaya huyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kutoa shukurani kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa kujitokeza kwa wingi na kuwapa ushirikiano mkubwa Makarani wa Sensa ya Watu na Makazi hatua ambayo inawarahisihia kufanya shughuli zao hizo.

Amesema kuwa, hatua hiyo inatoa faraja kwa wilaya na mkoa huo kwa kuona kwamba mafanikio makubwa zaidi yatapatikana pamoja na kufikia lengo lililokusudiwa kwani hatua hiyo ndio chachu ya maendeleo endelevu ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua idadi ya wakazi wote nchini.

Mkasaba ametoa wito kwa wananchi wote ambao bado hawajapata fursa ya kuhesabiwa kuendelea kufanya subira kwani Makarani wa Wilaya hiyo watahakikisha wananchi wote wanapata haki yao hiyo ya msingi kwa kuhesabiwa popote pale walipo kama walivyoahidiwa na Serikali.

Nao Masheha wa Wilaya hiyo kwa nyakati tofauti walieleza jinsi zoezi hilo linavyoendelea kwa mafaniko makubwa sambamba na kuwepo kwa amani, usalama na utulivu mkubwa.

Makarani wa Sensa ya Watu na Makaazi wa Wilaya hiyo kwa upande wao walieleza jinsi zoezi hilo linavyokwenda vizuri pamoja na ushirikiano mzuri wanaopata kutoka kwa wananchi hali ambayo inawarahishia kwa kiasi kikubwa kufanikisha shuguuli zao hizo kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hayo, Makarani hao walieleza mafanikio waliyoyapata katika dodoso la Jamii kwenye Wilaya hiyo, zoezi ambalo lilifanyika Agosti 21 hadi 22, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news