Rais Dkt.Mwinyi ateta na ujumbe kutoka Iran, waahidi neema Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inawahitaji wawekezaji kutoka Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran, kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali za Uchumi wa Buluu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislam ya Watu wa Iran, Mhe. Hossein Amir Abdollahian (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu jijini Zanzibar na Ujumbe wake kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo (Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na Ujumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Hossein Amir Abdollahian ambapo pamoja na mambo mengine mkutano huo ulibainisha maeneo mbalimbali ambapo nchi hiyo inalenga kuisaidia Zanzibar.

Amesema, Zanzibar ina sera nzuri za uwekezaji, huku ikiwa na mahitaji makubwa ya kupata wawekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu ili kuimarisha uchumi wake.

Aidha, amewataka wataalamu wa nchi hiyo kuja nchini kuangalia namna ya kuimarisha sekta za uvuvi pamoja na biashara.

Dkt.Mwinyi alilipongeza Taifa hilo kwa ushirikiano wa kihitoria kati yake na Zanzibar pamoja na kusaidia juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, vyuo vya amali, kilimo, matibabu na madawa.

Amesema Zanzibar ina mahitaji makubwa ya nishati ya umeme, ambapo hivi sasa inapata huduma hizo kupitia Waya wa chini ya Bahari (marine cable) kutoka Tanzania Bara, hivyo amepongeza azma ya Iran inayolenga kushirikiana na Zanzibar kupitia sekta hiyo.

Aidha, Dkt.Mwinyi alishukuru Iran kwa kuazimia kushirikiana na Zanzibar katika suala la upatikanaji wa fursa za masomo nje ya nchi (scholarship), na kusema ni jambo jema litakalowawezesha wanaafunzi wa Zanzibar kujifunza, hususan katika masomo ya Sayansi.

Rais Dkt.Mwinyi aliiomba Iran kuleta watendaji wake ili kukaa pamoja na wenzao wa Zanzibar ili kuona kwa namna gani wataweza kusaidia uimarishaji wa sekta za viwanda ili kutoa fursa za ajira kwa vijana pamoja na kutaka wataalamu wa nchi hiyo kuja kuanzisha viwanda hivyo.

Amepongeza juhudi zilizoanza kuchukuliwa na Taifa hilo za kusaidia uimarishaji wa sekta ya kilimo kwa kuipatia Zanzibar zana na vifaa mbalimbali ikiwemo matrekta pamoja na ‘Power Tiller’ ili kuendeleza kilimo cha kisasa.

Aidha, alitoa shukrani kwa mwaliko aliopewa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ebrahim Raissi wa kulitembelea Taifa hilo hapo baadae.

Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu, Hossein Amir Abdollahian alibainisha maeneo mbalimbali ambapo Taifa hilo linalenga kushirikiana na Zanzibar, ikiwemo suala la kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Watu wa Jamii ya Shirazi walioko Iran na wale wa Zanzibar.

Alieleza kuwa, Iran ina azma ya kuanzisha ushirikiano na Zanzibar katika suala la upatikanaji wa nishati na kusema nchi hiyo ina uzoefu mkubwa katika suala la nishati ya umeme, huku akatolea mfano wa mradi mkubwa unaoendelea kutekelezwa na Taifa hilo nchini Iraq unaohusisha umeme wa Megawati 4000.

Hossein alisema eneo jingine ambalo taifa hilo linalenga kushirikiana an Zanzibar ni la upatikanaji wa fursa za masomo nje ya nchi, ili kuwawezesha wanafunzi wa Zanzibar kwenda nchini humo kujifunza katika nyanja mbalimbali za kitaalamu.

Aidha, alieleza eneo jingine ambapo Iran inaweza kushirikiana na Zanzibar ni juu ya ujenzi wa miundombinu, ukihusisha ujenzi wa barabara, njia za reli pamoja na viwanja vya ndege.

Kuhusiana na sekta ya biashara, Waziri huyo alisema ni eneo ambalo Taifa hilo liko tayari kushirikiana na Zanzibar, na kusema nchi hiyo inashika nafasi ya tano duniani.

Katika hatua nyengine, Waziri Hossein alitoa mapendekezo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuitaka kuandaa Kamati ya Jumuiya ya Wafanya Biashara kwa lengo la kubainisha maeneo yanayopasa kushirikiana.

Aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili hizo katika sekta za Utalii, Uchumi wa Buluu, Afya, pamoja na kuandaa majukwaa yatakayofanikisha kufanyika uchambuzi ili kubaini fursa za ushirkiano.

Aidha, alitoa pendekezo linalotoa nafasi ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Zanzibar pamoja na kutoa fursa ya kuwakutanisha na wenzao wa Iran kwa lengo la kupata uzoefu katika nyanja za elimu ya juu pamoja na Sayansi.

Alisema Taifa hilo lina azma ya kuanzisha Chuo Kikuu hapa nchini ili kutoa fursa kwa wanafunzi wazalendo kujifunza nyanja mbalimbali ambazo Serikali ina mahitaji makubwa, kama vile sekta ya mafuta na gesi asilia.

“Pendekezo jingine ni la kubadilisha uzoefu katika shughuli za mabunge hususan katika Dilomasia ya Uchumi,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news