Diamond Platnumz aiangukia Serikali, asema kwenye muziki kuna fedha

NA DIRAMAKINI

MSANII wa Kimataifa na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB),Nasibu Abdul Juma Issack (Diamond Platnumz) ameiomba Serikali kupitia Baraza la Sanaa nchini (BASATA) kuangalia namna ya kutengeneza misingi sahihi ambayo itasaidia wasanii na wawekezaji wafahamu kuwa, muziki ni biashara na sio kusaidiana.

"Tuna wawekezaji wengi, lakini wanasema sheria za Tanzania haziwasaidii katika muziki, haziwalindi wawekezaji ni wakati sasa umefika walezi wetu BASATA watengeneze misingi sahihi ambayo itasaidia wasanii na wawekezaji na muziki utambulike ni biashara sio kusaidiana.

"Tunao wasanii wazuri mfano Aslay ana talent (kipaji) kubwa sana, ana uwezo mkubwa sana, lakini angekuwa mikononi mwangu au mwa mwekezaji yeyote mwingine akamwekezea fedha angefika mbali sana;

Diamond ambaye ni msanii wa kizazi kipya ameyasema hayo hivi karibuni wakati msanii hicho, Elias Barnabas maarufu Barnaba, akitambulisha albamu yake mpya yenye nyimbo 18 katika tamasha alilolipa jina la Love Sounds Different.

Katika hafla hiyo ambayo ilifanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, DIRAMAKINI ilishuhudia mgeni rasmi alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson.

Albamu hiyo imeandaliwa na Diamond Platnumz ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 18 tangu kuanza kazi ya muziki kwa mwanamuziki Barnaba.

Baadhi ya wanamuziki mashuhuri walioshirikishwa kwenye albamu hiyo ni Diamond Platnumz, Ali Kiba, Marioo, Rayvanny, Lunya, Lody Music Kusah, Dayoo, Khaligraph Joned, Mbosso, Lady Jaydee, Khadija Kopa na Platform.

"Lakini mwekezaji akiona kama kina Diamond wanazinguliwa wanajiuliza, je? Mimi, ndugu zangu wa serikalini naomba mtutengenezee utaratibu mzuri ambao utasaidia kufanya biashara hii ifanyike kwa ufanisi. Muziki unaingiza fedha nyingi sana.

"Sheria na kanuni zinazotengenezwa na BASATA haziwapi wao nmna nzuri ya kufanya biashara na watu...msingi ni biashara tutumie unaweza kuleta fedha ambayo itatupa heshima kwenye nchi yetu,"ameeleza Diamond Platnumz.

Yeye na Barnabas

"Nilimjua Barnabas miaka ya nyuma, leo tunaposherehekea miaka 18 ya Barnabas na uzinduzi wa albamu yake. Kwa Niaba ya taasisi ya Wasafi ninashukuru kwa ushirikiano wake katika kusukuma gurudumu la sanaa, talent yake ni kubwa sana.

"Nilikutana naye amekodisha teksi, mimi napanda daladala najifanya mwanafunzi ninalipa shilingi 50. Hakuna mtu niliyekuwa ninamuwaza kama Barnabas nilikuwepo, kila nikikaa namuwaza.

"Wakati ule naandaa wimbo wangu wa Nenda Kamwambie mtu wa kwanza kumtafuta nimshirikishe alikuwa ni Barnabas hata nilipokwenda pale THT (Tanzania House of Talents) mtu ambaye nilitamani anipenyeshe pale alikuwa ni yeye sikutaka mtu mwingine.

"Nilikwenda THT nikamkuta Hamza, nikafanya majaribio bahati mbaya sikupita nilipofanya majaribio, lakini niliwaza kwamba endapo ningemkuta Baranabas hakika ningepita.

"Ndugu zangu Mungu anaweza kuwa na kitu amekuandalia, ile safari ilikuwa na maana kubwa sana tumekuwa tukishirikiana kwa mambo mengi baina ya Barnabas na Wasafi. Barnabas hajasaini Wasafi, mimi nilipofikia siwezi kumsaini Barnabas ni mtu ambaye sisi sote tuliotoka, tumekuwa tunamwangalia Barnabas anaimbaje.

"Mimi na Barnabas tumesema, kwa nini tusitengeneze kitu ambacho watu wakafuta dhana ambayo mnapokuwa wasanii wakubwa lazima muwe na chuki kati yenu. Lazima mtofautiane, kwa nini msishirikiane mkafanya kitu ambacho kinafaida kitaonesha upendo, kuleta watu karibu.

"Wenzetu Wanaigeria wanajifanya hawapatani, lakini hawagombani,wanatuchora tu sisi huku muziki wao unapanda Mimi namshukuru sana Barnabas kuipa heshima taasisi ya Wasafi tuendelee kushirikiana milango iko wazi. Kwenye tasnia wenzetu wa Magharibi wameenda mbali sana, tusiwe tunatofauti za kiukweli, tusiwe tunakwazana kiukweli hata kama kuna kukwazana lazima tuwe tunashirikiana kwenye biashara,"amesema Diamond kama alivyokaririwa na  DIRAMAKINI katika hafla hiyo.

Kauli ya Diamond kwa Spika

"Mheshimiwa Spika muziki ni biashara kubwa sana, tazama wasanii waliokuja jinsi walivyopendeza, wana magari mazuri huko nje ya gharama sana, muziki unalipa kodi Serikalini, itambulike kwamba muziki huu hauwezi kwenda mbali hauwezi kuingiza fedha pasipo kuwekezwa ndani yake...na katika watu kuwekeza unagharimu fedha nyingi sana.

"Msanii sasa hivi mpaka atoke kwenye level kubwa unapoteza si chini ya shilingi milioni 300 hadi 350, lakini pia lazima uwe mvumilivu si chini ya miaka mitatu,"ameeleza Diamond kama alivyokaririwa na DIRAMAKINI.

Atamani Serikali ifanye

"Changamato ambayo natamani sana Serikali itusaidie, ihakikishe inatengeneza mazingira ya wawekezaji ili waje kuwekeza kwenye muziki kwa sababu tuna wasanii wengi wenye talent, utashangaa mtu anasema mbona msanii fulani hatumsikii?...sio kwamba hasikiki, talent yake anayo, lakini wawekezaji wa kuwekeza wanakuwa hawapo.

"Tazama humu ndani Mheshimiwa Spika, wasanii wengi wakubwa, wazuri wenye talent nzuri, lakini mtu anaonekana kama amefulia, lakini hapana. Sisi kama wasanii, msanii anapowekezewa fedha habaki tena kama mtu wa kawaida bali anakuwa ni brand, anaweza kuingiza fedha nyingi sana.

"Lakini kwa bahati mbaya sisi wasanii zinapoanza kuingia hizo fedha msanii anataka ale fedha peke yake anamkimbia mwekezaji, anaanza kusema mara mwizi, tapeli bahati mbaya wawekezaji wengine wanaacha,"amesema Diamond kama alivyokaririwa na DIRAMAKINI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news