HGWT yapokea wasichana 32 waliokimbia ukeketaji wilayani Serengeti

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara limepokea wasichana 32 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Serengeti waliokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao.

Ambapo kwa sasa wasichana hao wanapatiwa hifadhi katika Kituo cha Nyumba Salama Hope Mugumu kinachomilikiwa na shirika hilo kilichopo Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara. 

Huku idadi ikitajwa huenda ikaongezeka kutokana na mwaka huu kugawanyika kwa mbili hivyo koo mbalimbali zinafanya mila hiyo na ikizingatiwa kwamba wanafunzi wako likizo hivi sasa, hivyo baadhi ya wazazi na walezi wanatumia mwanya huo kufanya ukatili huo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kituo cha Nyumba Salama Hope Mugumu, Daniel Misoji wakati akizungumza na DIRAMAKINI leo Agosti 9, 2022 kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly.

"Tumepokea mabinti 32 waliokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao kutokea maeneo mbalimbali ya Serengeti ikiwemo Nyamoko, Machochwe, Rung'abure na Kebanchabancha. 

"Bado tunaendelea kupokea, nisema tu kwamba hiki ni kipindi cha likizo wapo wazazi na walezi wanatumia huu mwanya wa likizo kuwakeketa mabinti niwaombe waache. ukeketaji haufai sote kwa pamoja tuungane kuutokomeza.

"Tuwafichue mbele ya vyombo vya sheria wale wote ambao wana mpango wa kuwafanyia ukeketaji mabinti kabla hawajafanya tuweze kudhibiti mapema kwa sababu wapo katika jamii tunaishi nao. 

"Mwaka huu unagawanyika kwa mbili kwa hiyo ukeketaji utafanyika kwa kiwango kikubwa, lakini tukiunganisha nguvu kwa pamoja tutaweza kudhibiti taarifa zitolewe Polisi haraka, ofisi za serikali za vijiji, ofisi za maendeleo ya Jamii na kwa watu wa kuaminika ambao ni haraka kuchukua hatua wakifahamishwa,"amesema Misoji.

Pia, amewaomba watu wanaofanya kazi hiyo ya kukeketa (Ngariba) kama njia ya kujipatia kipato waache mara moja kazi hiyo, bali watumie njia halali ambazo zinakubalika kisheria kujipatia kipato. 

Huku akiwahimiza wazee wa kimila Wilayani Serengeti kuwa sehemu muhimu ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuumaliza ukeketaji kwa kutoa matamko ya kukemea mila hiyo.

"Zipo kazi za kufanya ikiwemo kilimo, biashara, ufugaji na ushonaji mtu akizifanya kwa ufanisi anaweza kufanikiwa kimaisha badala ya kukeketa kwani mwisho wake ni mbaya,"amesema Misoji.

Elizabeth Peter ni Mkazi wa Mugumu ambapo amesema uwepo wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania wilayani humo limesaidia kwa kiwango kikubwa sana kunusuru watoto wa kike kufanyiwa ukeketaji kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwapa hifadhi wasichana wengi ambao kila mwaka hukimbilia kituoni hapo kupata hifadhi na kuendelezwa kielimu. 

Huku akiomba Serikali kuendelea kuwawajibisha vikali wazazi na walezi wanaofanya ukeketaji.

"Polisi Dawati la Jinsia na Watoto wamekuwa wakitoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia sehemu mbalimbali ndani ya Wilaya yetu ya Serengeti wakishirikiana na Shirika la Hope, lakini bado wapo watu ambao hawatii sheria za nchi. 

"Wanakumbatia mila ya ukeketaji. Watu hawa wakikamatwa wafikishwe mahakamani na wananchi tufike mahakamani kutoa ushahidi kusudi wafungwe maana tukiwaacha wataendelea kukwamisha ndoto za watoto wa kike. Wanawakeketa kuwaandaa kuwaozesha hakuna kingine,"amesema Jesca Mwita mkazi wa Misitu Mugumu katika mazungumzo na DIRAMAKINI.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Longinus Tibishubwamu akizungumza na DIRAMAKINI leo Agosti 9,.2022 amethibitisha kukamatwa kwa ngariba mmoja aitwaye Rhobi Mahando Magoko maarufu kwa jina la Mokehanga mwenye umri wamiaka 50 mkazi wa Kebanchabancha Wilaya ya Serengeti na Kijiji cha Nyabisaga Tarime akidaiwa kujihusisha na ukeketaji akihama hama mkoani humo na kwamba taratibu za kiupelelezi zikikamilika atafikishwa mahakamani, kwani kitendo hicho ni kinyume cha sheria za nchi.

Amewataka wazazi na walezi mkoani Mara kutowakeketa watoto wa kike badala yake wawalinde na kuwathamini kwani vitendo vya ukatili wa kijinsia vinamadhara kwao ikiwemo kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza na hatari ya kifo pamoja na ulemavu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news