Kibaha yaongoza ukusanyaji mapato, Bumbuli yaburuza mkia

NA GODFREY NNKO

UCHAMBUZI umeonesha kuwa, katika mwaka wa fedha 2021/22, halmashauri 100 zimekusanya kwa asilimia 100 au zaidi ya lengo la mwaka, halmashauri 78 zimekusanya kati ya asilimia 80 hadi asilimia 99 na halmashauri saba zimekusanya kati ya asilimia 58 hadi 79.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhesshimiwa Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Amefafanua kuwa, halmashauri zilizofikia malengo ya mwaka zimeongezeka kutoka halmashauri 57 katika mwaka wa fedha 2020/21, hadi kufikia halmashauri 100 katika mwaka wa fedha 2021/22. “Hakuna Halmashauri iliyokusanya chini ya asilimia 50 kwa miaka yote miwili mfululizo.

“Ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kwa kigezo cha asilimia ya makusanyo, unaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imeongoza katika halmashauri zote kwa kukusanya asilimia 247 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Mlele asilimia 185, na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro asilimia 158.

“Ongezeko hili la asilimia limetokana Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kufanya mauzo ya eneo la uwekezaji, ambayo hayakuwa sehemu ya bajeti ya halmashauri hiyo,”ameeleza Mheshimiwa Waziri.

Pia amesema,Halmashauri ya Wilaya ya Mlele imekuwa na ongezeko la mapato kutokana na kushamiri kwa shughuli za kilimo na uwindaji, baada ya kukamilika kwa barabara ya Tabora hadi Mpanda. Aidha, Kumekuwa na ongezeko la ushuru wa huduma kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Rufiji.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 58 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe asilimia 67, na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 70 ya makisio yake ya mwaka.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema kuwa, katika kuzipima halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), jumla ya halmashauri 35 zimekusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 5.

Amefafanua kuwa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote, kwa kukusanya Shilingi Bilioni 75.3 ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Shilingi Bilioni 47.3, na Halmashauri ya jiji la Dodoma Shilingi Bilioni 45.1.

Aidha, halmashauri nne zimekusanya chini ya Shilingi Bilioni 1 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imekua ya mwisho kwa kukusanya Shilingi Milioni 599.7, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Shilingi Milioni 692.1, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Shilingi Milioni 792.3, na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Shilingi Milioni 880.2.

“Halmashauri hizo, pamoja na kuendelea kukusanya chini ya Shilingi Bilioni moja, zimeonekana kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato,”amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news