Pwani, Manyara waongoza ukusanyaji mapato

NA GODFREY NNKO

UCHAMBUZI wa taarifa za mapato kwa kuzingatia ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kimkoa, unaonesha Mkoa wa Pwani umeongoza kwa kukusanya asilimia 118 ya lengo la mwaka, ikifuatiwa na Mkoa wa Manyara asilimia 114.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhesshimiwa Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri Bashungwa, Mkoa wa Katavi unafuatia kwa asilimia 112 na Songwe kwa asilimia 111.

“Mkoa wa Lindi umekua wa mwisho kwa kukusanya asilimia 87, ukifuatiwa na Mikoa ya Mtwara na Geita asilimia 93,”amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Amefafanua kuwa, katika eneo hilo ufanisi umeongezeka kwa kuwa katika mwaka wa fedha 2020/21, Mkoa wa Lindi ulikuwa wa mwisho kwa kuwa na asilimia 78, na sasa mkoa huo umepanda na kufikia asilimia 87.

“Kwa kuzingatia wingi wa mapato (pato ghafi), Mkoa wa Dar es Salaam umekusanya mapato mengi zaidi kuliko mikoa mingine, kwa kukusanya Shilingi Bilioni 167.5, ikifuatiwa na Mkoa wa Dodoma Shilingi Bilioni 89.4, na Mkoa wa Pwani Shilingi Bilioni 48.7.

“Mkoa wa Rukwa umekuwa wa mwisho kwa kukusanya Shilingi Bilioni 9.4, ukifuatiwa na Mkoa wa Katavi kwa kukusanya Shilingi Bilioni 13.6, na Mkoa wa Simiyu Shilingi Bilioni 14.0,”amefafanua Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Pia amesema kuwa, uchambuzi unaonesha kuwa mikoa hiyo imeongeza ufanisi ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2020/21 kwani Mkoa wa Rukwa ambao ulikuwa wa mwisho ulikusanya Shilingi Bilioni 8.2, Mkoa wa Katavi Shilingi Bilioni 9.7 na Mkoa wa Simiyu Shilingi Bilioni 11.4.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri amesema kuwa,mikoa hiyo inakuwa ya mwisho kutokana na uchache wa halmashauri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news