'Maboresho sheria za habari nchini ni muhimu, kuna vipengele vipo kimtego'

NA MWANDISHI WETU

WAKILI wa Kujitegemea, Bw. James Marenga amesema, mwandishi wa habari anaruhusiwa kuandika maneno yanayodhaniwa kuwa kashfa iwapo yametoka ndani ya Bunge ama kwa rais.
Lakini pamoja na ruhusa hiyo kutoka katika sheria ya sasa, bado hana ulinzi kwa maana maneno hayo hayo yanaweza kugeuzwa na akashtakiwa.

Ameyabainisha hayo leo Agosti 9, 2022 wakati akiliwakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika mazungunzo na wahariri wa magazeti ya Mwananchi jijini Dar es Salaam.

Wakili Marenga amekutana na Lilian Timbuka, mhariri wa habari Mwananchi pia Samuel Kamdaya, Mhariri wa Habari wa The Citizen kuzungumzia mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari nchini pia kukabidhi mapendekezo ya sheria hizo.

“Mfano ndani ya Bunge kuna maneno makali ama ya kashfa yametamkwa au rais kamwita waziri wake mpumbavu ama vyovyote vile. Mwandishi anaweza kuandika maneno hayo na asishitakiwe kabisa, lakini nje ya hapo, maneno hayo yanakuwa jinai na wala si madai. Hii ni hatari sana,”amesema Wakili Marenga.
Amesema, sheria hiyo hiyo haimpi kinga mwanahabari kama habari hiyo itakwaza viongozi wa juu. "Unaweza kuandika ila inategemea itapokelewa vipi. Ndani ya sheria hizo, kuna maeneo mwandishi anaweza kujikuta anaingizwa mkenge hata kwa nia njema ya habari aliyoiandika kwa taifa lake. Ndio maana tumeona kuna kila sababu ya kufanyia maboresho,”amesema Wakili Marenga.

Pia amesema, kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.
“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo.

“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasehma sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,”amesema Wakili Marenga.

Post a Comment

0 Comments