Meena:Mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 yakifanikiwa yataleta athari chanya

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Neville Meena amesema kuwa,iwapo mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 yatafanikiwa yataleta athari chanya kwenye sheria zingine za habari kwa kuwa, sheria hiyo ndio injini ya sheria nyingine.
Ameyasema hayo Agosti 27, 2022 wakati akizungumza na Radio Abood (Abood FM) ya mkoani Morogoro.

“Sheria iliyopo haikukubalika toka mwanzo. Kama mabadiliko ya sheria ya huduma za habari yatafanikiwa hata kama sio vipengele vyote kwa pamoja, ilaleta athari kubwa katika sheria zingine,” amesema Meena.

Kauli hiyo ilitanguliwa na maelezo kwamba, kwa sasa harakati za mabadiliko zimejikita katika Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kwa kuwa, serikali imeeleza kuanza na sheria hiyo.

Meena amesema, ni jambo la kupongeza kwa hatua ambayo Serikali imechukua na ilipofika mpaka sasa, kwani yapo ambayo wamekubaliana na yapo ambayo hawajakubaliana na wanaendelea na majadiliano
“Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) wakati alipozungumza na BBC. Alisema yapo ambayo wameishakubaliana na mazungumzo bado yanaendelea. Sisi tunaamini kuwa, kuna athari chanya itatokea kwenye uandishi wa habari,”amesema Meena.

Amesema, wadau wa habari wameanzisha mchakato huo kwa kuwa, wana nia nzuri na tasnia ya habari na kwamba, Serikali imeona nia hiyo ndio maana imeingia kwenye mazungumzo.

“Sisi tuna nia nzuri na mjadala huu na ninaamini tutafika pazuri na kuifanya tasnia ya habari kuwa salama kwa wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe,"ameeleza Meena.

Post a Comment

0 Comments