Nyumba Salama Butiama na Hope Mugumu Nyumba Salama yapokea ujumbe kutoka Ubalozi wa Ufaransa

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Kitengo cha Ushirikiano na Utamaduni kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Cecile Frobert ametembelea Kituo cha Nyumba Salama Butiama na Hope Mugumu Nyumba Salama vinavyotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao.
Vituo hivyo, vinamilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) ambalo linapambana na ukatili wa kijinsia mkoani Mara chini ya Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly. Ambapo aliweza kuzungumza na mabinti hao (wasichana) na kuwatia moyo wasome kwa bidii na kuwa na malengo thabiti ya kufikia ndoto zao bila kurudi nyuma.

Pia, amepongeza juhudi zinazofanywa na Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutetea wasichana na wanawake katika kujenga ustawi bora na usawa kwa maendeleo endelevu ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Cecile Frobert amesema, katika kutambua juhudi na mchango unaofanywa na Rhobi Samwelly katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu Rhobi ameweza kupewa tuzo ya Marianne Initiatives kutoka kwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kutambua mchango wake akiwa miongoni mwa wengine kutoka mataifa mbalimbali ambao pia walipewa tuzo.
Frobert ameongeza kuwa, Ubalozi wa Ufaransa utaendelea kuunga mkono juhudi za Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuzidi kuliwezesha katika kufanikisha mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani Mara ili kujenga ustawi bora na usawa kwa ajili ya maendeleo.

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly amesem kuwa, ataendelea kusimamia haki za binadamu na usawa wa Jinsia hasa kuwasaidia wasichana na Wanawake ambao bado wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa Kijinsia licha ya serikali na wadau mbalimbali kupambana na vitendo hivyo.
Rhobi amesema, anashukuru kupata tuzo ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ya 'Marriane Initiatives' ambayo imempa hamasa, ari, na nguvu ya kuzidi kufanya kazi ya kupambana na ukatili wa Kijinsia ikiwemo mila zisizofaa ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na vitendo vinavyorudisha nyuma juhudi za Wanawake na wasichana kuwa katika hali nzuri za kufikia malengo yao. 

Huku akiiomba jamii kuunga mkono juhudi za serikali za kuutokomeza ukatili wa Kijinsia kwa manufaa ya maendeleo ya nchi.

Post a Comment

0 Comments